Marafiki zangu, mapenzi si mateso ya moyo. Hatupaswi kuwa kwenye uhusiano wa kimazoea tu. Lazima tuangalie, tupo kwenye mstari sahihi? Baada ya utambuzi huo, sasa tunaweza kuamua kuendelea au lah!
Wiki jana nilimalizia pale nilipoanza kutoa ushauri kwa wote kuhusu namna nzuri ya kumtambua mwenzi aliye sahihi. Kwanza kabisa nilisema, mwenzi huyo ni wa ndoto zako? Lazima awe na sifa zile ulizokuwa ukizihitaji.
Sasa tuendelee..
SURA NI KIGEZO?
Kuna baadhi ya watu utawasikia wakisema: “Mpenzi wangu ananivutia sana, yaani ni mzuri sana. Najua hata nikitoka naye, marafiki zangu watanisifia kwa kuchagua vizuri...”
Hizi ni fikra potofu ndugu zangu. Mapenzi ya kweli hayapo kwenye sura wala umbile la mtu. Vipo vigezo vya muhimu kabisa vya kuzingatia tofauti na uzuri wa sura.
Sura hubadilika ndugu zangu, binadamu wanazeeka - kuna kuugua na matatizo mengine ambayo yanaweza kubadilisha mwonekano ambao ulikuvutia awali. Je, yakitokea ndiyo utakuwa mwisho wa kumpenda?
Kama leo hii unamuoa kwa sababu umevutiwa na matiti yake madogo, akishazaa na kunyonyesha kisha yakaanguka, ndiyo mwisho wa kumpenda? Umempendea ngozi yake nyororo, akipata aleji ya mafuta, ngozi ikaharibika na kuwa na mabakamabaka utakuwa mwisho wenu?
Wewe mwenye mpango wa kuolewa na mwanaume mwenye kigezo cha kifua cha kimapenzi, kesho akifutuka na kuwa na kitambi utamuacha? Ndugu zangu, kiukweli ni kwamba kigezo cha uzuri wa sura na umbile si sahihi kabisa katika kuchagua mwenzi.
ANAJALI, ANAHESHIMU HISIA ZAKO?
Je, mwenzi wako mtarajiwa ni faraja kwako? Anakusaidia unapokuwa na matatizo makubwa ya kiafya? Yupo nawe bega kwa bega katika maswaibu yanayokukuta? Lazima awe na mapenzi ya dhati na wewe.
Lazima mwenzi wa maisha yako awe anakupenda kweli kweli. Ambaye anaweza kuifanya siku yako kuwa bora. Ndugu zangu, unaweza usione umuhimu wa jambo hili, lakini nataka kuwaambia kwamba, mwenzi ambaye hata kutumia neno baby, sweetie, dear na mengineyo ni shida, ni tatizo.
Anza kumfuatilia kuanzia sasa hivi utagundua kulingana hata na kauli zake tu. Lazima awe na maneno matamu ambayo yatakutuliza jazba zako wakati ukiwa na mambo binafsi yanayokukwaza.
Nawe ambaye unatarajia kuingia kwenye ndoa na mwenzako, jifunze kuwa na maneno matamu. Kuwa mtu wa karibu na mwenzako muda wote, sikiliza shida zake, kuwa mshauri wake mkuu. Hapa nasisitiza, sizungumzi na jinsi moja. Wote wanahusika.
UNAMPENDA KWA DHATI?
Kama niivyotangulia kusema, huwezi kuingia mkataba wa maisha na mtu ambaye humpendi kwa dhati. Lazima wewe pia umpende na ujali hisia zake.
Achana na utamaduni wa kuingia kwenye ndoa ukiwa mguu nje, mguu ndani kwa mategemeo kwamba eti utampenda ukiwa tayari mmeshaoana!
Hakuna kitu kama hicho rafiki yangu. Lazima nafsi yako ikuhakikishie kuwa, kweli umempenda ndipo mambo mengine yafuate. Mapenzi hayalazimishwi. Acha kujaribujaribu!
Kama unampenda, utajua tu, kama humpendi usipoteze muda wa mwenzako, kaa pembeni.
KUNA KISICHOSAHAULIKA?
Kati ya mambo ambayo yanaongeza mapenzi ya dhati kwa wawili ni pamoja na kufanyiwa kitu kisichosahaulika. Je, kuna kitu ambacho umefanyiwa na mwenzako huwezi kukisahau? Chunguza hili kwa makini. Hapa sizungumzii zawadi za sketi au suruali. Manukato au mikufu. Yapo mambo makubwa, ambayo ukitafakari na kukumbuka namna mpenzi wako alivyokusaidia unaona kweli anastahili kuwa mwenzi wako wa maisha katika ndoa takatifu.
Hakuna majaribio kwenye ndoa ndugu zangu. Ni maagano. Ni kifungo, ni kitanzi! Umejiandaaje? Tafakari kabla ya kuamua. Nakutakia mwaka mpya mwema wenye mafanikio makubwa katika uhusiano wako.
Wiki ijayo tutaanza mada kuhusu Sikukuu ya Wapendanao ‘Valentine’s Day’, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano na Maisha anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vitatu; True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
1 comment:
Safi sana. Ungeniwekea hii wakati naolewa ningesema adios. Tatizo tunaingia tu kwenye ndoa bila kufafakari na kuishia talaka. Penzi ni penzi halifichiki.
Post a Comment