ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, February 4, 2014

TIKETI ZA ELEKTRONIKI MARUFUKU

Rais wa TFF, Jamal Malinzi.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesitisha matumizi ya tiketi za kielektroniki kwenye viwanja vinane mpaka itakapotolewa taarifa nyingine.

Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana, zilisema TFF imeamua kufanya hivyo baada ya kubaini madudu mengi katika tiketi hizo.

Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ambao unatumika kwa tiketi hizo, haukutumia tiketi hizo katika mechi yake ya juzi dhidi ya Kagera Sugar ya Kagera.

Hata hivyo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Boniface Wambura alipotafutwa kuzungumzia hilo, simu yake ya mkononi iliita bila majibu na hata ujumbe ufupi wa maneno aliotumiwa, hakuujibu.

Lakini Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF Kanda ya Kaskazini (Tanga na Kilimanjaro), Khalid Mohamed alisema mfumo huo sio tu unachanganya, lakini pia mashine zimeharibika.

“Sisi jana (juzi) hakukuwa na mechi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, lakini katika mechi zijazo, hatutatumia tena mfumo wa kielektroniki, maana sio kwamba hatutaki, lakini hata hizo mashine zenyewe mbili zilizofungwa zimeharibika,” alisema Mohamed.

Lakini mtoa habari wetu alithibitisha jana kuwa licha ya kusimamishwa kwa tiketi hizo, pia jana kulikuwa na kikao kuzungumzia suala hilo ambalo limegonga vichwa tangu kuanza kutumika katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ulioanza Januari 25, mwaka huu.

Juzi, Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana na kuiagiza Sekretarieti, Benki ya CRDB na Bodi ya Ligi kufanya kikao cha dharura kwa ajili ya mapitio ya tiketi hizo ambazo zimekuwa na malalamiko.

Viwanja vilivyofungwa mfumo wa tiketi za kielektroniki ni Azam Complex, Kaitaba Bukoba, Jamhuri Morogoro, Kumbukumbu ya Sokoine Mbeya, Shekhe Amri Abeid Arusha, CCM Mkwakwani Tanga na CCM Kirumba Mwanza.

CHANZO HABARI LEO

No comments: