ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 3, 2014

JK Avunja Ukimya-Aamua kuwatetea mawaziri mizigo

*Aamua kuwatetea mawaziri mizigo
*Amshangaa Mbowe kulazimisha Serikali tatu
*Aeleza anavyokerwa na malumbano ya urais
RAIS Jakaya Kikwete amewakingia kifua mawaziri mizigo huku akishangazwa na malumbano yanayoendelea kutaka wafukuzwe kazi.
Amesema kwamba, uamuzi wa kuitwa na kuhojiwa kwa mawaziri hao katika kikao cha Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC), kulitokana na hoja zilizoibuka kwa wananchi na kwamba kuitwa kwao hakukumaanisha kwamba wanatakiwa kufukuzwa kazi.
Kutokana na hali hiyo, amesema mawaziri hao mizigo, wamepewa maelekezo ya utendaji kazi huku wakifuatiliwa juu ya utekelezaji wa maagizo ya chama.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana jijini Mbeya, alipokuwa akihutubia katika kilele cha miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, alisema Kamati Kuu ya CCM imetimiza wajibu wake, hivyo Serikali inafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa.
“Pale mawaziri wanne walipoitwa na Kamati Kuu baada ya ziara ya Mkoa wa Ruvuma na Mbeya, matatizo yaliyohusu sekta zao yalizungumzwa na uamuzi kufanywa kuhusu hatua za kuchukuliwa.
“Najua wapo watu waliotaka mawaziri hao wafukuzwe kazi, kwa vile halikufanyika hilo, basi likageuzwa kuwa suala la malumbano, ni vema ieleweke kuwa, kuitwa kwao katika Kamati Kuu hakuna maana ya wao kufukuzwa.
“Wao waliitwa kwa sababu ya kuwepo matatizo yaliyoonekana yanatakiwa yapatiwe ufumbuzi, yamezungumzwa na maelekezo yametolewa kuhusu cha kufanya.
“Kamati Kuu imetimiza majukumu yake na uliobaki ni wajibu wa Serikali, Kamati Kuu itaendelea kufuatilia na kama hakuna maendeleo, inaweza kuchukua hatua zipasazo dhidi ya mhusika na huko hatujafika,” alisema Rais Kikwete.
Kauli ya Rais Kikwete inakuja katika kipindi ambacho kumekuwa na mijadala kuhusu uteuzi wa baraza lake la mawaziri, hasa baada ya mawaziri walioonekana kupwaya katika utendaji kurejeshwa tena katika baraza lake.

1 comment:

Anonymous said...

Na mimi nakuunga mkono mheshiwa rais. Tuiache "mizigo" ipige mzigo.