ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 26, 2014

NEW YORK JAMJADILI TENA TEMBO, CHELSEA CLINTON AONGOZA MAJADILIANO, TANZANIA YASHIRIKI

 Picha  mbalimbli za Tembo zilipamba ukumbi  yalipofanyika majadiliano kuhusu tembo,  picha hizo  na ambazo zilikuwa kivutio kwa washiriki wa majadiliano hayo ziliandaliwa na National Geograpy
 Mkurugenzi Mtendaji wa  ABC HOME Paulette Cole akiwakaribisha wanajopo na wageni waalikwa katika majadiliano  kuhusu tembo,  majadiliano hayo yalifanyika siku ya jumanne usiku  Jijini New York. 
 Chelsea Clinton, Makamu Mwenyekiti wa Clinton Foundation,  na ambaye aliongoza majadiliano hayo  akiwatambulisha wanajopo, kutoka kushoto ni  Bw. John Heminway, Balozi Tuvako Manongi,    kati kati ni Chelsea  Bint wa Rais Bill na Hilary Clinton,  kulia kwa Chelsea ni   Bw. Bryan Christy na  anayefuatia  ni   Bw. Josh Ginsberg kutoka Wildlife Conservation Society. Heminway na Christy ni waandishi na watunga filamu na kwa pamoja wametengeneza filamu ijulikanayo kama  "The Battle for Elephants". Filamu   hiyo  itaonyeshwa  February 27 kupitia  Channel ya National Geograpy.
 Bw. Bryan Christy naye akieleza  jambo,  Bw. Christy ameshiriki katika kutengeneza filamu ya  The Battle for Elephants,  habari zaidi zinaonyesha kwamba   sehemu ya filamu hiyo  inahusu  Tanzania, na Bw. Christy   anaonekana kwenye filamu hiyo akipozi kama mnunuzi wa  meno ya tembo.
 Muwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika  Umoja wa  Mataifa,  Balozi Manongi, akielezea jambo wakati  wa majadiliano  kuhusu tembo na changamoto  zinazomkabili. Balozi Manongi alitumia fursa hiyo kuelezea  juhudi mbalimbali zinazofanywa na  Serikali katika  kukabiliana na vitendo vya ujangili na  udhibiti wa  biashara haramu ya pembe za tembo.

Na Mwandishi Maalum
 Zikiwa zimepita  wiki  chache tangu  kufanyika kwa  Mkutano  uliojadili kwa kina  kuhusu  ujangili dhidi ya tembo na biashara haramu ya pembe za  tembo  uliofanyika Jijini London,  Uingereza. Jana Jumanne,  hapa Jijini New York, Marekani, palifanyika  majadiliano mengine yakihusu pia sifa na uzuri wa mnyama tembo na  hatari inayomkabili.
Majadiliano  hayo   na ambayo yaliwavutia washiriki  wengi,  yaliandaliwa   kwa ushirikiano kati ya   National Geograpy na  ABC na yalifanyika  katika  jengo  lijulikanalo kama  ABC HOME    lilipo Broadway,  jijini New York.
Balozi Tuvako  Manongi,  Muwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  katika Umoja wa Mataifa, alikuwa kati ya wanajopo wanne walioalikwa kushiriki majadaliano hayo ambayo yaliongozwa na Chelsea Clinton,  Makamu  Mwenyekiti wa Clinton Foudantion.
Wanajopo  wengine  walikuwa ni  Bw. Josh Ginsberg  kutoka Wildlife Conservation Society,  Bw. John Heminway mwandishi na mtengeneza filamu ambaye pamoja na mwanajopo mwingine   Bryan Christy  wameshiriki katika kutengeneza filamu ijulikanayo kama  “The  Battle for Elephants” filamu hii inatarajiwa kuonyeshwa february  27 kupitia  Channel ya National Geograpy.
 Wanajopo hao wakiongozwa na Chelsea Clinton, walipata fursa ya kila mmoja wao kuelezea nini yeyé  kama mtu binafsi au kupitia taasisi anayoiwakilisha ametoa mchango  gani katika suala zima la uhifadhi wa Tembo na uthibiti wa  mauaji holela ya  Tembo na  biashara haramu   ya pembe za tembo.
Balozi  Manongi kwa upande  wake, alielezea  juhudi mbalimbali ambazo serikali inafanya katika  kukabiliana na  ujangili dhidi ya tembo, pamoja na biashara haramu  ya pembe , aidha alielezea dhamira na nia ya serikali  ya  kuendeleza  mapambano  ya kuwanusuru tembo kupitia awamu ya pili ya  Operesheni Tokomeza.
Balozi pia alijibu maswali mbalimbali na kutolea ufafanuzi hoja zikiwamo  kuhusu  kwanini operesheni tokomeza ilisitishwa,  na  je serikali  ilikuwa na mpango gani kuhusu shehena ya pembe za ndovu ambayo iko katika maghala.
Kwa ujumla wanajopo wote walikubaliana kwamba, mapambano dhidi ya  ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu ni vita  ngumu  hasa ikizingatiwa kwamba mtandao unaohusika na biashara ya pembe za  tembo ni mpana sana na unaohusisha watu wengi.
Na kwa sababu hiyo wamehimiza mambo kadhaa  yakiwamo,  ushiriki wa wadau kutoka makundi mbalimbali ya  kijamii kitaifa na kimataifa,  udhibiti wa soko na  hitajio la pembe za ndovu, utoaji wa elimu kwa umma, uwezeshwaji wa watendaji katika ngazi mbalimbali,  na uimarishaji wa sheria.
Kwa picha zaidi  bofya soma zaidi

 Hapana shaka kwamba Hatari ya kutoweka kwa tembo barani afrika,  ni jambo  linalowagusa wengi, washiriki wa majadiliano hayo walitumia fursa hiyo kujifunza siyo tu hatari ya kutoweka kwa  mnyama  huyo, lakini pia uzuri na sifa zake, na namna gani wanaweza kuchangia  kuhakikisha  hatoweki kabisa
 Sehemu ya washiriki waliohudhuria majadiliano hayo  ambapo pia walipata fursa ya kuuliza maswali kwa wanajopo
 Waandishi pia    walikuwepo nao walipewa changamoto ya kuandika habari zenye kuelimisha jamii kuhusu athari za  mauaji holela ya tembo  pamoja  na kuihamasisha kutambua wajibu  na nafasi yao katika  uhifadhi wa  wanyama walio katika hatari ya kutoweka.
 pichani ni  sehemu ya washiriki wa majadiliano hayo

1 comment:

Anonymous said...

Operation Tokomeza iliua watu. Irejeshwe kwa tahadhari kubwa sana. Zaidi pia wakubwa nao wakubali kufunga masoko na maduka yao yanayouza mapambo ya pembe za ndovu. Hapa DC ndipo penyewe!