ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 26, 2014

UMUHIMU WAKO KWA MWENZI WAKO UKO WAPI?-2

MADA iliyopo mezani ni namna ya kutambua na kudumisha umuhimu wako kwa mwenzi wako. Wiki iliyopita tulianza kwa kuona jinsi mtu anavyoweza kupoteza umuhimu kwa mwenzake baada ya kushushwa thamani.

Marafiki zangu, jambo kubwa unalotakiwa kufahamu ni kwamba suala la kupanda au kushuka thamani lipo mikononi mwako. Yapo mambo ambayo ukiyazingatia, mwenzako hawezi kukuchoka na kufikia hatua ya kukushusha thamani.

Tayari tumeshaona athari zake lakini hapa sasa nitakupa mbinu ambazo ukiwa nazo makini basi itakuwa rahisi kwako kubaki namba moja na mtu muhimu zaidi kwa mpenzi wako maana ni haki yako.

ANZIA MWANZO
Ni rahisi zaidi kulinda thamani yako kuanzia mwanzo wa uhusiano wenu. Ikiwa tayari mmeshakomaa halafu tatizo hilo likajitokeza, hutumika nguvu nyingi zaidi kulirekebisha kuliko kujizatiti kuanzia mwanzo wa uhusiano. Ni mambo gani hayo? Twende hapo chini.

KAULI...
Naomba ieleweke wazi kuwa mada hii ni maalum zaidi kwa wanawake. Kitu muhimu cha kwanza kabisa kwa mwanamke ambaye anataka kuilinda thamani yake kwa mpenziwe ni kupima kauli zake.
Acha kuropoka hovyo, pima maneno yako na ikiwezekana kama unadhani kuna jambo huna hakika nalo usizungumze kabisa.

Katika eneo hili, uwe makini zaidi mnapokuwa na watu wengine. Kama mwanamke usiwe mchangiaji hoja sana.
Utulivu wako unaweza kuwa silaha kubwa ya kukufanya ubaki na thamani yako kama mwanamke unayejitambua.

USIRUHUSU NGONO
Msichana mwenye kujitambua na kufahamu thamani yake sawasawa hawezi kuruhusu mwili wake ujulikane na mwanaume harakaharaka. Onesha unajitambua na usikubali kirahisi kuuacha mwili wako uchezewe.
Mpe hoja; kwanza mapema, hajakuoa wala kukuchumbia, haraka ya nini? Wakati unawaza kuhusu kutoa penzi lako, lazima ufikirie kuhusu athari zinazoweza kukupata kwa kukurupukia mapenzi. Mwanaume ambaye bado hamjachunguzana na huna hakika naye ya kutengeneza maisha, kichwani mwake hakuweki kwa asilimia kubwa.

Ukumbuke kwamba, ukipata matatizo yoyote – binafsi au yanayosababishwa na uhusiano wenu, anakuwa hana uwajibikaji wa asilimia kubwa kwa tatizo hilo. Utabaki wewe na matatizo yako!
Mwingine anaweza kujiuliza; itawezekana kweli kuwa na uhusiano bila kukutana faragha? Ni kweli kuna ugumu katika kipengele hiki hasa kwenye dunia tuliyonayo lakini asikudanganye mtu, ukiweza kusimamia kipengele hiki, thamani yako itapanda maradufu na kudumu kwa mpenzi wako.

Tafiti mbalimbali zinaonesha kwamba, wanawake ‘wagumu’ zaidi kukubali kutoa tendo la ngono au kukataa kabisa mpaka ndoa, huwa na nafasi kubwa zaidi ya kuingia kwenye ndoa.

Mtaalamu mmoja aliwahi kuandika kwenye kitabu chake; wanaume wanapenda kuwa na wanawake wao peke yao bila kuchangia na mtu. Wanaamini kukubaliwa haraka faragha humaanisha kuwa hata wakioa ni rahisi zaidi wanawake hao kutoa penzi nje ya ndoa kuliko wale wagumu au wanaokataa kabisa.
Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitatu, True Love, Let’s Talk About Love na All About Love.

No comments: