ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 6, 2014

CCM, Chadema, CUF wanavuruga Bunge, asema Dovutwa

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Fahmi
Dodoma. Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Fahmi Dovutwa alichafua hali ya hewa baada ya kuvituhumu vyama vya CCM, Chadema na CUF kuwa ndiyo vinavuruga Bunge kwa sababu ya misimamo yao.
Hali hiyo ilitokea wakati mjumbe huyo akichangia mjadala wa Rasimu ya Kanuni za Uendeshaji wa Bunge Maalumu la Katiba juzi.
Dovutwa alitoa shutuma hizo baada ya mjumbe mwingine, Julius Mtatiro kueleza kuwa amepitia Rasimu ya Kanuni lakini hakuona mahali panapoeleza mpangilio wa ukaaji wakati wa kupiga kura.
Hali hiyo ilimfanya Dovutwa, kusimama na kutoa tuhuma kuwa baadhi ya wajumbe wamehongwa na kwamba kuruhusu mpangilio maalumu ni kukaribisha mgawanyiko.
Alisema kukaa kwa mpangilio huo kutawapa nafasi viongozi mbalimbali kushinikiza wajumbe wao katika maamuzi ya mambo mbalimbali.
“Ukaaji wa sasa umezingatia masilahi ya nchi, utashi na matakwa ya wananchi. Watu wa CCM, CUF na Chadema ndiyo mnaharibu mkutano (Bunge),” alisema Dovutwa.
Dovutwa alisema vyama hivyo vinatofautiana katika masuala mbalimbali na misimamo yao ndiyo imetawala bunge hilo.
“Mnatulazimisha tuwasikilize nyie tu. Kwa hiyo Mwenyekiti usikubali, kikao hiki kizingatie masilahi mapana ya makundi mbalimbali,” aliongeza Dovutwa.
Baada ya kutamka hilo, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kupitia Kanuni, Amon Mpanju alisimama na kumtaka Kificho kulisaidia Bunge hilo kwenda na utaratibu aliowatangazia juzi wajumbe, ambao wanatakiwa kuwasilisha hoja zao kwenye kamati kisha kutolewa uamuzi.
“Naomba uamuzi ukishafanyika, kiti chako kisiruhusu mtu mwingine kuingilia maana mchakato hautafika mwisho. Nawaomba wajumbe wenzangu tusilete michango inayoweza kuleta hisia za mgawanyiko miongoni mwetu,” alisema Mpanju.
Mtatiro alisema hakupendezwa na mchango wa Dovutwa na kutahadharisha ukweli hauwezi kukwepeka kwa kuwa kuna watu wanaotoka katika makundi mbalimbali.
“Wakati wa kupiga kura tunahitaji theluthi mbili ya wajumbe wa Tanzania Bara na idadi kama hiyo kwa wajumbe kutoka Zanzibar kwa hiyo ili kurahisisha kazi hiyo, wajumbe kutoka Zanzibar wakae upande wao na wale wa Bara wakae upande wao,” alisema Mtatiro.
Hata hivyo, akijibu hoja hiyo mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kupitia Kanuni, George Simbachawene alimtaka mjumbe huyo kusubiri maelezo juu ya kifungu kinachoelezea jinsi ya upigaji wa kura.
“Kikishatolewa uamuzi ndiyo tutafanya uamuzi, lakini nadhani upigaji kura utaongozwa na utaratibu maalumu. Sidhani kama mapendekezo ya Mheshimiwa Mtatiro tunaweza kuyachukua maana hatujui jinsi gani tutapiga kura,” alisema.
Mwananchi

No comments: