ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 6, 2014

Kiapo Bunge la Katiba kutafuna Sh560 milioni

Dodoma/Dar. Kitendo cha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuapa mmojammoja badala ya makundi kama ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Kanuni za Bunge kitaligharimu Taifa zaidi ya Sh500 milioni, Bunge limeelezwa. 
Hayo yalielezwa juzi usiku na Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ali Kessy na Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe baada ya baadhi ya wajumbe kupinga pendekezo la Kamati ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo la kuapa kwa makundi ili kuokoa muda.
Katika maelezo yake, Kessy alisema kwa idadi ya wajumbe wote wa Bunge hilo ambao ni 629, ni wazi kuwa wakiapa mmojammoja, itawachukua siku tatu kumaliza na katika muda huo posho za wajumbe zitafikia Sh500 milioni.
“Jamani lazima tuwe na huruma na mkumbuke kuwa tunalipwa kwa kodi za Watanzania. Tukiapa mmojammoja tutachukua siku tatu na kwa siku hizo tutalipwa posho ambazo zitafikia Sh500 milioni. Ni bora tukaapa kwa makundi kama ilivyopendekezwa,” alisema Kessy.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbowe ambaye alisema: “Bunge hili limepangiwa muda maalumu wa kufanya kazi na mpaka sasa tumeshatumia siku 15. Tukiapa kwa muda wa siku tatu, ni sawa na kupoteza Sh500 milioni.
“Tunaelewa umuhimu wa watu kuweka historia, kamati imetuletea ushauri mzuri, ni vyema tungeufuata, nawaombeni turidhie maoni ya kamati maana tumekuja hapa kutunga Katiba siyo kanuni. Naunga mkono kuapa kwa makundi.”
Iwapo wajumbe wote watahudhuria vikao vya Bunge kwa siku tatu za kuapa, kwa siku moja watalipwa Sh188.7 milioni na kwa siku tatu watalipwa Sh566.1 milioni. Kila mbunge analipwa Sh300, 000 kwa siku.
Awali, kamati hiyo ilipendekeza kuwa wajumbe hao waape kwa makundi matatu ili kuokoa muda, lakini kutokana na michango ya wabunge, ilipitishwa kuwa kila mmoja aape kwa wakati wake.
Mapema, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Costa Mahalu alisema kamati yake ilipendekeza kuapa kwa makundi ili kuokoa muda na kwamba kama wajumbe wakiapa mmojammoja, shughuli hiyo itachukua siku tatu.
Akitoa ufafanuzi zaidi, mjumbe Ezekiel Oluoch alisema, “Nimewahi kuwa mbunge wa Bunge la Afrika kwa miaka minne. Sisi tuliapa hotelini kwa makundi, tena kwa kutumia karatasi zilizokuwa zimechapwa sala kulingana na dini ya mjumbe husika na tulikuwa wabunge kutoka nchi 53.”
Alisema kama kuna wajumbe wanaotaka kuapa mmojammoja ili familia zao ziwaone kupitia televisheni, ni bora wakasubiri kushinda ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby alipinga kiapo hicho cha mmojammoja kwa maelezo kuwa kitawaumiza wanyonge ambao ni walipa kodi kwani kitachukua muda mrefu kwa watu kulipwa fedha bila ya kufanya kazi yoyote.
“Sikubaliani na hilo, labda kama kuna watu wanaotaka kuchukua mikanda ya video, tunapaswa kuliangalia na kulihurumia taifa letu pia,” alisema Shabiby.
Kwa upande wake Felix Mkosamali, alisema suala la kuapa kwa pamoja halina madhara wala makosa kisheria na kwamba cha msingi ni dhamira.

Waliopinga
Pendekezo la kuapa mmojammoja lilipingwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Anne Makinda ambaye alisema kuapa ni sawa na kusali, hivyo ni vyema kila mjumbe akaapa mwenyewe. 
“Utaratibu wa mabunge yote ni kwamba wabunge wanaapa mmojammoja na siyo makundi. Hiki ni kiapo kati ya mhusika na Mungu wake,” alisema Makinda.
Mjumbe mwingine, Abdallah Bulembo alisema kila mjumbe lazima aape ili aweze kuonekana... “Wanaong’ang’ania kuapa kwa makundi walishaonekana kwenye televisheni. Sasa ni wakati wetu na sisi kuonekana,” alisema Bulembo na kuungwa mkono na mjumbe mwingine wa Bunge hilo, Zainab Kawawa.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alipinga kiapo cha pamoja ambacho alikiita kuwa ni kituko ambacho hakileti picha nzuri.
Lugola aliwataka wajumbe wenzake kuacha kufikiria habari za muda na gharama kwa maelezo kuwa ikitokea wakaapa kwa pamoja kuna uwezekano mkubwa kwa baadhi ya wajumbe kuendelea ndani ya Bunge hilo bila hata kuapa.
Kauli za wanasheria
Baadhi ya wanasheria nchini wameunga mkono mapendekezo ya kiapo pamoja wakibainisha kuwa hautaathiri ratiba na muda wa shughuli za Bunge.

Wakili wa Kujitegemea, Sengalawe Charles alisema kuna viapo vya njia mbalimbali ikiwamo kuapa mbele ya aliyekuteua au kwa maandishi mbele ya kamishna wa kiapo ambaye anaweza kuwa kiongozi au ofisa yeyote aliyepewa mamlaka hayo kisheria.
“Kiapo cha maandishi kinaweza kuwa sahihi kwa wajumbe wa Bunge kujaza fomu kila mmoja na kuziwasilisha kwa kamishna wa kiapo ili kusaini kuthibitisha na kukiri kiapo chake kimaandishi,” alisema.
Alisema mapendekezo ya utaratibu huo hayawezi kutumia muda mrefu unaoweza kuathiri ratiba na mpangiliao wa vikao vya Bunge kama kutumia utaratibu wa kuapa mbele ya aliyewateua,” alisema Charles.
Mwanasheria, Harold Sungusia wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHCR) alisema pamoja na utaratibu huo wa kujaza fomu, wajumbe wanayo nafasi ya kuapa kwa makundi kabla ya kujaza fomu hizo na kusainiwa.
“Kuna mambo ya kuzingatia, kwanza lazima anayeapa atambue anachokiapa na yule anayemwapisha atambue anamwapisha kwa dhamira ipi, hiyo itarahisisha kukubaliana na utaratibu wa kuapa hata kwa makundi na baadaye kila mmoja kujaza fomu na kusaini kwa nafsi yake,” alisema.
“Jambo jingine Bunge linaandaa ofisi ya majaji au mahakimu kwa muda hata wa siku mbili hapo Dodoma. Utaratibu huo bado hautaweza kutumia muda mwingi kama inavyojadiliwa. Kinachotakiwa Bunge lijipange tu.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Habel Chidawali (Dodoma) na Kelvin Matandiko (Dar).
Mwananchi

No comments: