Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,Pandu Ameir Kificho.
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Pandu Ameir Kificho, ameanza kupata wasiwasi kuhusu kasi ndogo wanayotumia wajumbe kufanya marekebisho ya Rasimu ya Kanuni za Bunge, kifungu kwa kifungu, kwamba itachelewesha uchaguzi wa mwenyekiti wa kudumu na ratiba zingine za Bunge hilo.
“Tumechukua muda mkubwa (mrefu) sana katika kuchangia marekebisho, nawaombeni twenda moja kwa moja kwenye hoja badala ya kuzunguka kwenye hoja.
“Wajumbe ambao hoja zao zinafanana na wengine, hawana haja ya kutaka kuwa kwenye orodha ili wachangie. Tunataka kazi hii ifanyike haraka ili twende kwenye uchaguzi wa mwenyekiti na makamu wake...tunataka kutumia muda mchache (mfupi) sana kwa kazi hii,” alisema.
Kificho alirudia kauli hiyo jana wakati wa mahojiano na Redio One akisema kuendelea kwa mijadala mirefu ya kununi kunatokana na bunge hilo kutokuwa na kanuni badala yake kutumia uzoefu wa vyombo vya bunge na maridhiano ya wajumbe.
Alisema kuendelea kujadiliwa kwa kanuni hizo taratibu na kuchukua muda mrefu ni kwa ajili ya kujenga misingi imara na umakini ili kupata kanuni zitakazoliongoza Bunge hilo na kupata katiba inayofaa Watanzania.
“Kwanza nikiri kuwa shughuli za kutayarisha kanuni zinaenda taratibu na mara kwa mara nimekuwa nikijitahidi kuwaambia wajumbe kuzingatia muda na kuwa na ufanisi wa kutayarisha kanuni hizo, hivyo muda unaweza utoshe ama usitoshe, lakini lengo siyo kujadili taratibu ili tuongezewe, ingawa tunaweza kuongezewa kulingana na kanuni zilizopo,” alisema Kificho.
Alisema kujadiliwa kwa kanuni hizo kwa muda mrefu haina maana kuwa wanataka kuongezewa muda wa kuendelea na mjadala huo badala ya siku 70 walizopewa, bali ni kutaka kupata makubaliano ya wajumbe kwenye kuandaa kanuni hizo.
“Bunge hili lina wajumbe wengi ukilinganisha na Bunge la kawaida, tulilolizoea, kwa hiyo umakini mkubwa unahitajika katika kujadili kanuni, lazima wajumbe wapewe nafasi ya kujadili na tukizingatia muda wajumbe wengi watakosa nafasi ya kujadili, hivyo kuwakosesha nafasi wajumbe kutakuwa hakuna demokrasia kwani itaonekana kanuni zimeandaliwa na makatibu pekee na siyo wajumbe,” alisema Kificho.
Aidha, aliwataka Watanzania kuendelea kuwa na subira wakati huu wa kuandaa kanuni ili kupata katiba inayowafaa, na kwamba lazima wajumbe wapewe nafasi ya kujadili kanuni zitakazoongoza vyema upatikanaji wa katiba.
Uchaguzi wa mwenyekiti wa muda uliomweka kwenye kiti hicho Kificho ulifanyika Februari 18, mwaka huu.
Baada ya kuchaguliwa, Kificho aliteua wajumbe 20 wataalamu wa sheria kuunda Kamati ya Muda ya Kumshauri Mwenyekiti wa Muda chini ya mwenyekiti wake, Profesa Costa Mahalu, na kuanzia Februari 19 hadi 20, pamoja na wajumbe wengine, walikuwa kwenye vikao vya kazi vya kuandaa Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum.
Februari 26, wajumbe wote walianza semina kuhusu Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalum kwa kugawiwa rasimu ya kwanza na baada ya kuichambua kwa siku kadhaa rasimu hiyo ilifanyiwa marekebisho na kuandikwa nyingine na waligawiwa nakala zake kuanzia Jumamosi iliyopita na majadiliano ya kuiboresha yalianza rasmi Jumatatu hadi sasa wamefikia hatua ya kujadili kifungu hadi kifungu.
Jumla ya vifungu 31 vilikuwa vimepitishwa kati ya vifungu 87 vinavyounda rasimu hiyo.
Kwa mujibu wa ratiba ya awali iliyotolewa na Bunge, uchaguzi wa mwenyekiti wa kudumu na makamu wake ulipangwa kufanyika Februari 21, mwaka huu na kesho yake wangekula kiapo na baadaye kufuatia kiapo cha wajumbe wote ambacho kingetumia siku tatu na ufunguzi rasmi wa Bunge Maalum ulipangwa kufanyika Februari 24, mwaka huu na siku ya pili yake Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, angewasilisha Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba kwenye Bunge Maalum.
Ratiba ilionyesha kuwa Februari 26, mwaka huu ungeanza mjadala wa kupitisha Rasimu ya Katiba.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, Bunge hilo linatarajia kutumia siku 70, na kama itaonekana halijamaliza kazi basi litaongezewa siku zingine 20.
Wakati muda ukizidi kuyoyoma hali inaonyesha muda wa kupitia rasimu ya katiba unaweza kuwa mrefu zaidi kiasi cha kuathiri shughuli nyingine za serikali kama kuwasilisha bajeti ya serikali ya mwaka 2014/15.
Kuazia mwaka jana utaratibu wa kuwasilisha bajeti ya serikali ulibadilika kutoka Juni hadi Aprili ili bajeti ya serikali iwe imekwisha kuwasilishwa yote ifikapo Juni 30 ya kila mwaka na mwaka wa fedha uanze rasmi Julai mosi.
Kwa kasi ya sasa ya Bunge Maalum la Katiba, kuna kila dalili kuwa bajeti ya serikali itachelewa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment