ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 6, 2014

`Hati ya Muungano siyo taarifa ya siri`

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba,John Mnyika.

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othuman Masood, amesema kuwa hati ya Muungano siyo nyaraka za siri bali ni ya umma na kila mmoja anaweza kuiona na kuwa nayo.

Mjumbe Masood alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kuwapo kwa mvutano kati ya mjumbe, John Mnyika kupendekeza kuwa kifungu cha 17 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kinaelezea utaratibu wa utendaji kazi waTume na Christopher Ole Sendeka aliyetaka hati hiyo kuwa siri.

Alisema kifungu cha 17 fasili ya nne kinaeleza kuwa moja ya nyaraka zilizopitiwa na Tume ni kuchambua na kupitia michango, mawazo, maoni,taarifa na mapendekezo yaliyokusanywa na kufanyiwa tathimini siku za nyuma ikiwemo hati ya Muungano ambayo ni rejea ya msingi katika mjadala wa Muungano.

Alisema Sheria hiyo ilieleza wajumbe kupata taarifa na nyaraka mbalimbali za kuwawezesha kutoa maoni na kuwasilisha mawazo mbalimbali na kwamba wanatunga kanuni kwa kuongozwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Mnyika alisema kifungu cha 19 fasili ya kwanza kimeorodhesha nyaraka ambazo wajumbe wa Bunge hilo wanapaswa kupewa na kwamba kati yake zipo walizopewa na ambazo hawajapatiwa ni hati ya Muungano, na kwamba inaonyesha katika kufanya kazi za kibunge wajumbe ili watimize kazi yao vizuri anaweza kuhitaji taarifa aisome.

”Kwa kuzingatai hali hiyo napendekeza kanuni ya nne iongezewe fasili ya sita itamke, “mjumbe yoyote wa Bunge Maalum anayo haki ya kupatiwa tarifa au nyaraka ya kumwezesha kufanya kazi yake kwa mujibu wa sheria na kanuni, itawawezesha kufanya kazi zao vizuri zaidi,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments: