ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 14, 2014

Usiku wa Mwambao Asilia Aprili 19


Na Andrew Chale
KUNDI la Dar Modern Taarab na Nadd Ikhwan (Malindi), wanatarajiwa kutoa burudani ya aina yake katika onesho maalumu la ‘Usiku wa Mwambao Asilia’, ndani ya ukumbi wa Travertine, Magomeni jijini Dar es Salaam, Aprili 19.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mlezi wa Heshima wa kundi la Dar Modern Taarab, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fabak Fashions, Asia Idarous Khamsin, alisema wadau wa muziki wa taarabu watafurahia usiku huo wa Mwambao Asilia kutoka kwa wanamuziki nguli wa miondoko hiyo hapa nchini na visiwani.
“Usiku wa Mwambao Asilia, utasheheni magwiji wakongwe wa muziki wa taarabu nchini, kutoka kundi la Dar Modern Taarab na Nadd Ikhwan, ambao wataporomosha nyimbo za taarabu asili za zamani na za sasa,” alisema Asia Idarous.
Aliongeza kuwa, pia usiku huo utapambwa na ‘surprise’, ikiwemo watu mbalimbali kupita kwenye zuria jekundu ‘red carpet’ na kupiga picha za ukumbusho na mastaa watakaohudhuria usiku huo.
Alisema katika usiku huo, kiingilio kitakuwa ni sh 10,000 ambako tayari tiketi zimeshaanza kuuzwa sehemu mbalimbali.
Asia, alizitaja sehemu hizo kuwa ni pamoja na duka la Fabak Fashions, Regency Park Hotel Mikocheni na Dar Modern Taarab Hall Magomeni Ifunda. Onyesho hilo pia limedhaminiwa na Times FM, Fabak Fashions na www.nakshi255.com

No comments: