HAYAWI…hayawi
sasa yamekuwa! Habari ya mjini ni maandalizi kabambe ya harusi ya staa
wa Bongo Fleva na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) anayewakilisha Vijana Mkoa
wa Geita, Vicky Pascal Kamata ikidaiwa kuwa shughuli hiyo itatafuna
kiasi cha Sh. milioni 96, Ijumaa lina mkanda kamili.
Staa
wa Bongo Fleva na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) anayewakilisha Vijana
Mkoa wa Geita, Vicky Pascal Kamata akiwa na mchumba wake Charles Pai.
IJUMAA LAMNASA BWANA HARUSI
Habari
kutoka kwa chanzo cha ndani zilisema kuwa Vicky anatarajia kufunga
pingu za maisha Mei 24, mwaka huu na mchumba wake wa muda mrefu ambaye
Ijumaa limemnasa aliyejulikana kwa jina la Charles Pai.
Ilidaiwa kwamba mwanaume huyo ni kigogo ndani ya kampuni moja ya huduma za simu hapa nchini.
HARUSI YA REKODI
Kwa
mujibu wa mtonyaji wetu huyo ambaye naye ni miongoni mwa wanakamati,
harusi hiyo inatarajiwa kuweka rekodi ya aina yake Bongo.
“Sijawahi
kuona harusi ya kifahari kama ya Vicky, itafanyika tarehe 24 mwezi huu,
ina siku chache tu, huwezi kuamini mambo yote yamekamilika,” alisema
mpashaji wetu.
HOTELI YA NYOTA TANO
Imesemekana
kwamba baada ya ndoa hiyo kufungwa kanisani, shughuli itahamia katika
hoteli yenye hadhi ya nyota tano ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro
iliyopo Posta, Dar ambapo waalikwa watagonga mnuso wa maana na vinywaji
vya kumwaga.
Habari
zilieleza kuwa sherehe hiyo itahudhuriwa na mawaziri, wabunge wenzake,
vigogo mbalimbali serikalini na baadhi ya wasanii wenzake.
Ilidaiwa kuwa bajeti ya shughuli hiyo imefikia kiasi hicho kwani Vicky anataka iwe ya aina yake.
BAJETI MIL. 96
Kwa
mujibu wa mwanakamati huyo, kwa bajeti hiyo ya Sh. milioni 96, Vicky
atakuwa amevunja rekodi ya ndoa za mastaa zilizowahi kufungwa Bongo.
“Nakwambia
harusi ya Vicky haina mfano, itafunika harusi za vigogo na mastaa
wengi, itakuwa ya aina yake. Bajeti yake siyo ya kitoto.
“Watu wengi wamemchangia, achilia mbali na kuweka hela yake yeye binafsi na mchumba wake, kitu kama Sh. milioni 40. KUVUNJA UKIMYA NA UVUMI
“Hakika
mheshimiwa amejipanga kuvunja ukimya na uvumi mwingi juu ya maisha yake
ya kisiasa na jamii inayomzunguka,” alisema mtoa habari wetu na
kuongeza:
VIKAO NI DAR, DODOMA
“Huwezi
kuamini, vikao vingi vya harusi sisi wanakamati tunafanyia Dar. Lakini
mara nyingine tunafanyia Dodoma kwa sababu waheshimiwa wengi wanakamati
wako huko.
“Hata
kwenye vikao watu wanakunywa na kula je, siku yenyewe itakuwaje?
Unaambiwa msafara wa magari ya kifahari tupu na utakuwa kama wa rais
ukiongozwa na farasi.
VICKY ANASEMAJE?
Baada
ya kupata habari hizo, gazeti hili lilimsaka Vicky kwa udi na uvumba
ili kujua mchakato mzima wa harusi umekaaje lakini simu yake ya mkononi
iliita bila kupokelewa huenda ni kwa sababu ya kubanwa na vikao vya
Bunge la Bajeti vinavyoendelea mjini Dodoma huku bwana harusi akishindwa
kutoa ushirikiano.
Hata
hivyo, bado tunaendelea kumsaka Vicky au kama atasoma habari hii
tunaamini anaweza kupiga simu kwenye chumba cha habari na kufafanua
jambo lolote juu ya tukio hilo la kihistoria katika maisha yake, hivyo
endelea kufuatilia hapa kila siku (24/7).
No comments:
Post a Comment