Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akiwa na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa nchi za Kiarabu Bw. Lakhdar Brahimi, wakati Katibu Mkuu alipotanganza mbele ya waandishi wa habari kuhusu kujiuzuru kwa Bw. Brahimi kama msuluhishaji mkuu wa mgogoro wa Syria. Katibu Mkuu Ban Ki Moon alisema amekubali kwa masikikitiko makubwa kujiuzuru kwa Bw. Brahimi na hasa katika kipindi hiki ambacho hakujapatikana muafaka katika mustakabari mzima wa mgogoro wa Syria. Bw. Lakhdar Brahimi mwanadiplomasia mzoefu na anaye heshimika katika Jumuiya ya Kimataifa anakuwa mwanadiplomasia wa pili kuachia ngazi akitanguliwa na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Kofi Annan aliyekuwa mjumbe wa kwanza kupewa dhamana ya kutafuta suluhu ya mgogogoro wa Syria.
Na Mwandishi Maalum
Ban Ki Moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
kwa masikitiko makubwa ametangaza
kukubali kwake kujiuzuru kwa
mwakilishi maalum wa Umoja wa mataifa na Muungano wa nchi za Kiarabu, Lakhdar
Brahimi aliyekuwa akisimamia mazungumzo ya kutafuta Amani nchini Syria.
Akitangaza mbele ya
waandishi wa habari kuhusu kujiuzulu kwa
Bw. Brahimi ambaye pia alikuwapo kwenye mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema mwanadiplomasia huyo mzoefu ataachia wadhifa wake ifikapo Mei 31.
Huku hali ikiendelea kuwa ya sitofahamu na kutokuwapo
kwa mwanga wowote wa maridhiano au kumalizwa kwa mgogoro nchini Syria, Ban Ki
moon anasema kujiuzuru kwa Mwakilishi huyo maaulum ni pigo kwa watu wa Syria na ni kielelezo cha kushindwa kwa Umoja wa Mataifa.
Bw. Brahimi aliteuliwa Agosti 17 mwaka 2012 akichukua nafasi ya Katibu Mkuu
Mstaafu wa Umoja wa Mataifa Bw.
Kofi Annan aliyeteuliwa mwanzoni kabisa mwa mgogoro huo na baada ya muda mfupi
alitangaza kujiuzuru.
Bw. Brahimi ameelezea masikitiko ya kuondoka kwake huku akiiacha Syria katika
hali mbaya. Lakini akaelezea matumaini yake kuwa, Katibu Mkuu, Ban Ki Moon,
atafanya kila ubinadamu iwezekanavyo kufanya kazi na Baraza kuu la Usalama
la Umoja wa Mataifa, pande zinazopigana
nchini Syria pamoja na nchi
jirani kumaliza mgogoro huo.
“ Ninahakika kuwa
mgogoro huu utamalizika, lakini wadau wote wanatakiwa kulizingatia hili je ni
vifo vingapi zaidi, ni uharibifu kiasi gani
utokee kabla Syria haijawa Syria
mpya” akasema Bw. Brahimi.
Naye Katibu Mkuu
akasema, kwa miaka miwili Bw. Brahimi amejitahidi sana kumaliza ukatili
na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini
Syria. “ Kwa kweli, mwanadiplomasia huyo
mwenye asili ya Algeria ( 80). Amepitia changamoto nyingi kuanzia taifa lenyewe ya Syria, eneo la Mashariki ya Kati na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla na ambayo imegawanyika vibaya juu ya namna ya kuumaliza mgogoro wa Syria.
Takwimu zinaonyesha kwamba tangu mgogoro wa Syria ulipoanza mwezi
Marchi 2011 zaidi ya watu 100,000 wamepoteza maisha na zaidi ya 680,000
wakiwa ni majeruhi. Aidha zaidi ya watu
milioni 9.3 wanahitaji misaada ya kibinadamu ndani ya
Syria, ikiwa ni pamoja na
watu milioni 6.5 ambao ni wakimbizi wa ndani. Vile vile mgogoro huo wa
Syria umesababisha kuwapo kwa wakimbizi
zaidi ya milioni 2.5 ambao wametafuta
hifadhi katika nchi jirani.
Katika kumuelezea zaidi Bw. Brahimi, Katibu Mkuu amemtaja kama mmoja ya watu
mashuhuri wanaotambuliwa duniani na mwana-diplomasia mwenye uwezo mkubwa na mtetezi mkubwa wa Misingi na
Katiba ya Umoja wa Mataifa.
Ban Ki moon akaongeza
kuwa, kwa Baraza Kuu la Usalama la Umoja
wa Mataifa na ambalo ndilo limepewa dhamana ya kusimamia usalama na amani. Pamoja
na nchi zenye ushawishi mkubwa kuhusu hali ya Syria
kushindwa kumpatia ushirikiano wa kutosha Bw. Brahimi, ni kushindwa kwetu sote.
Katibu Mkuu amesema
ataendelea kutegemea uzoefu na ushauri wa Bw. Brahimi na kwamba kutoka na kazi
nzuri aliyoifanya anastahili kupumzika.
Na akazitaka pande zote
zinazohusika na mgogoro wa Syria pamoja na mataifa yenye ushawishi kwenye
mgogoro huo , kujiangalia upya na kutafakari nini kinachotakiwa kufanywa ili
kuwarejeshea matumaini wananchi wa Syria.
No comments:
Post a Comment