VITA ni vita! Siku mbili zimekatika tangu sakata la picha ya pozi
inayodaiwa kuwa ni ya mheshimiwa Komba na msichana aliyetajwa kwa jina
moja la Angel kutoka kwenye baadhi ya vyombo vya habari Bongo, lingine
limeibuka!
Hili la safari hii ni zito pia. Lenyewe linamhusu mheshimiwa mmoja
ambaye anadaiwa ni mbunge wa Chadema. Na yeye anasemekana kwamba alipiga
picha katika pozi tata na ‘totoz’ ambaye jina lake halikupatikana.
Baadhi ya watazamaji wa picha hizo ambazo zimesambaa kwenye mitandao
mbalimbali ya kijamii, walisema kwa vile mheshimiwa Komba ni wa CCM na
mwenzake ni wa Chadema ni kama ngoma droo!
KWA NINI NGOMA DROO?
Maoni ya watu yanasomeka kwamba, vyama hivyo viwili ndivyo vyenye
ushindani mkubwa katika jamii hivyo viongozi wao kuning’inizwa kwenye
mitandao kwa madai hayo hakuna atakayesema mwenzake anahusika na hujuma
hiyo huku wale wa Cuf, NCCR-Mageuzi na vyama vikingine vikionekana
kuachwa nyuma kwenye ‘fasheni’ hiyo mpya.
“Ingekuwa mwingine ni wa CCM pia, si ajabu CCM wangesema Chadema
wanahusika, sasa ni CCM kwa Chadema. Hapo mnasemaje? Hamuoni kwamba
ngoma droo?” Alihoji mmoja wa wachangiaji hao kwenye mjadala huo wa
wanasiasa kuzidi kuchafuana kwa kasi.
MITANDAO YA KUCHAFUA
Habari zilizochimbwa na Ijumaa Wikienda zilidai kuwa, katika kipindi
hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015 kumeibuka kundi linalojiita
Umoja wa Kambi Huru ‘Ukahu’ ambao kazi yao kubwa ni kuwachafua wanasiasa
kwa habari za kweli au za kuwatungia.
“Kuna watu wanasema kuna Ukahu, yaani Umoja wa Kambi Huru wakiwa na
maana hawapo CCM wala Chadema. Wao kazi yao ni kuwachafua wanasiasa tu
kwa ajili ya kuelekea uchaguzi mkuu mwakani,” kilisema chanzo.
Kikaendelea: “Lakini nasikia hawa watu wanatumiwa na viongozi wa
wapinzani wa wanasiasa. Mfano, Komba kama ana mwanasiasa anataka ang’oke
kwenye jimbo lake mwakani, basi anawindwa kuanzia sasa ili achafuke na
watu wasimame wakisema yeye si msafi.
“Unaambiwa hao jamaa wa Ukahu, hata kama ulifanya madudu mwaka 2005, wao
wanayapata tu, kama huna wanakutengenezea madudu ya kufanana na wewe.”
WABUNGE WAJIPANGE, PICHA ZAIDI ZIPO
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa bado kundi hilo lina picha ambazo
baadhi ya wabunge walipiga au walitengenezewa wakiwa na vimwana ambazo
zimepangwa kutolewa moja baada ya nyingine kadiri siku zinavyokwenda
kuelekea uchaguzi mkuu.
WABUNGE WENGI KUANGUKA
Taarifa zanasema kundi hilo limejipanga kuhakikisha kwamba kwenye
mizengwe hiyo, katika kila wabunge 10, 4 hawatarudi kwenye majimbo yao
mwakani bila kujali vyama.
WABUNGE VIJANA WAKAE CHONJO
Ikazidi kudaiwa kuwa wabunge vijana, hasa wenye umri wa kuanzia miaka 25
hadi 50 ndiyo wapo kwenye tageti hiyo. Mheshimiwa Komba ana miaka 60,
mwenzake 44.
KISA NINI HASA?
Ijumaa Wikienda liliendelea kuchunguza zaidi na kubaini kwamba, kisa cha
mambo yote hayo ni kukomoana hasa kwa wale wanasiasa ambao wanatamani
kuwa wabunge kwenye majimbo ambayo wanaamini kuwatoa wahusika waliopo
sasa madarakani si rahisi.
“Mimi jamani najua siasa, wapo wanasiasa wanatamani sana majimbo ya
wenzao, sasa kwa vile wanajua kuwatoa si rahisi, wanapendwa sana ndiyo
maana wanatumia njia ya kuwachafua ili wapiga kura wasiwapende na wao
washike nafasi,” alisema mbunge kutoka jimbo moja la Mkoa wa Dar.
Akaendelea: “Siamini kama wabunge wetu wako hovyo kiasi hicho, kwamba
wanaweza kuwa wapo ndani ya vyumba vya gesti na wanawake halafu wakaamua
kupiga picha chafu, wana akili zao.”
GPL
No comments:
Post a Comment