Advertisements

Monday, October 13, 2014

KUNA MADHARA YA KUISHI PAMOJA KABLA YA KUOANA?

Leo ningependa kuzungumza na wewe msomaji wangu ambaye japokuwa bado hujaoa au kuolewa, unaishi na yule umpendaye, mnapika na kupakua pamoja kwa ahadi kwamba siku zijazo, mtafunga ndoa na kuwa mume na mke halali. Je, kitendo hicho ni sahihi? Kuna madhara gani ya kuishi pamoja kabla ya kuoana?

Mila na desturi za Kitanzania, zinaelekeza kwamba mwanaume au mwanamke akifikia umri wa kuoa au kuolewa, hatua ya kwanza ni uchumba rasmi. Katika kipindi hiki cha uchumba, wawili wapendanao husomana kwa muda, baada ya hapo ndoa hufuatia ambapo mwanaume na mwanamke huenda kuishi pamoja, wakiwa na baraka za pande mbili za wazazi.

Hata hivyo, kadiri muda unavyozidi kusonga mbele, maadili yanamomonyoka, mila na desturi hazifuatwi tena na matokeo yake, mapenzi yanageuka na kuwa janga kubwa kwa jamii.
Si ajabu siku hizi kuwakuta mwanaume na mwanamke wakiishi kwa kipindi kirefu, wakiwa wapenzi wa kawaida tu, yaani mwanaume hajamchumbia mwanamke wala kufanya taratibu zozote zinazostahili lakini anaishi naye kama mkewe, wanapika na kupakua pamoja.

Hali kadhalika wanawake, mwanaume hajakutolea posa wala hajawahi kuja kujitambulisha kwenu, mmekutana tu barabarani kisha mkakubaliana kuishi pamoja kama mume na mke, wazazi wako hawajui chochote, ndugu zako hawamjui mtu unayeishi naye! Kila kitu kinafanyika kienyeji tu ilimradi mnakidhi haja zenu za kimwili.

MADHARA YA KUISHI PAMOJA BILA NDOA

1. HAMUWEZI KUOANA
Upo ushahidi wa kutosha kwamba watu walioishi kwenye uhusiano wa kimapenzi usio halali kwa kipindi kirefu, waliishia kutendana na kuachana bila kutimiza ile ndoto waliyokuwa nayo kwa kipindi kirefu ya kuja kufunga ndoa na kuishi kihalali.

Kama umekubali kuishi naye kienyeji, elewa kwamba kitakachofuata baadaye mkishachokana, itakuwa ni visa visivyoisha na mwisho mtaachana. Kama kweli mnapendana kwa dhati, fuateni taratibu zote zinazostahili ili muingie kwenye uhusiano unaotambulika na pande zote mbili.

2. HATAIONA THAMANI YAKO
Hii inawahusu zaidi wanawake. Kuna usemi wa wahenga usemao kwa nini ufuge ng’ombe wakati unao uwezo wa kupata maziwa ya bure? Mwanaume ambaye anaishi na wewe kienyeji, hawezi kuiona thamani yako na hataona umuhimu wa kukuoa kwa sababu kila anachokitaka (tendo la ndoa) anapata kwa urahisi.

Heshima ya mwanamke ipo kwenye utu wake, ili mwanaume akuthamini, ni lazima uoneshe kwamba unaijua thamani yako na upo tayari kuilinda. Kuijua thamani yako ni pamoja na kukataa kuishi kienyeji na mwanaume ambaye hajajitambulisha kwenu wala hajafuata taratibu zinazotakiwa. Kama kweli anakupenda, atakuwa tayari kufanya chochote ili muishi pamoja kihalali.

3. MUME WA KWELI HAPENDI MTEREMKO
Wanaume wana kasumba moja, wanapokuwa wenyewe katika mazungumzo yao, hupenda kuelezea jinsi walivyohangaika kumpata mwanamke fulani mpaka wakafikia kufanya mambo makubwa ilimradi wakubaliwe. Kwao kumhangaikia mwanamke kwa kipindi kirefu, ni ushujaa.

Wanaume wengi ambao wanatafuta wake wa kuishi nao, hawapendi wanawake ambao wanajirahisi au ambao wanawapata bila jasho. Sasa ikiwa wewe mwanamke kabla hata mpenzi wako hajakuchumbia tayari umeshahamishia nguo zako kwake, atajisifia nini mbele za wenzake?

Ataamini wewe ni mwanamke mwepesi ambaye mwanaume yeyote anaweza kukupata kwa urahisi. Muache mumeo mtarajiwa ahangaike kukupata ikiwa ni pamoja na kuja kwa wazazi wako au ndugu zako.

GPL

1 comment:

Anonymous said...

Umetisha lakin nna swali