Zanzibar. Kabla na baada ya kuandikwa kwa Katiba Inayopendekezwa, wananchi wa Zanzibar wamebaki katika kizungumkuti kupambanua, kupima na kupembua ni nani kati ya Rais, Dk Ali Mohamed Shein na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Sharif Hamad anasema kweli na kustahili kusikilizwa kwa kina cha ufahamu.
Hiyo inatokana na kauli za kukinzana ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi hao wakuu kupitia majukwaa ya vyama vyao vya siasa kuhusu Katiba Inayopendekezwa ambayo kwa sasa inasubiri Kura ya Maoni Aprili mwakani kama ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete.
Itakumbukwa kuwa ushindani wa kauli na hoja katika masuala makubwa ya kisiasa kutoka kwa viongozi wa vyama vya siasa ulianza mwaka 1992, wakati huo CUF kikipigania kuitishwa mkutano wa kitaifa wa Katiba, jambo halikufanywa na kiongozi yeyote, si wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi wala Benjamin Mkapa.
Pamoja na tume kadhaa zilizoundwa na Serikali ya Muungano na kutoa mapendekezo yake ikiwamo ya Jaji Francis Nyalali na Jaji Robert Kisanga kushauri uitishwe mkutano wa kitaifa wa Katiba na maboresho mengine, hakuna kilichofanyika.
Hata hivyo, mambo mengine ya msingi ambayo yaliibua mjadala mkubwa kutoka kwa wanasiasa ni kufanyiwa marekebisho kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wakitaka Tume Huru ya Uchaguzi, kufutwa sheria 40 za ukandamizaji, kuitishwa kura ya maoni kuhusu Muungano pia wakitoa Azimio la kutaka kuachiwa huru kwa Seif Sharif Hamad ambaye kabla ya 1992 alikuwa gerezani.
Chaguzi za mwaka 1995, 2000, 2005 hadi ule wa 2010 zilifanyika chini ya Katiba ya mwaka 1977 na kusababisha manung’uniko na lawama kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani huku CCM ikiendelea kushinda kila uchaguzi katika urais.
Hata hivyo, utawala wa Rais Jakaya Kikwete ndiyo uliokuja na mpango wa uundwaji wa Katiba Mpya na kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikuwa na jukumu la kukusanya maoni ya wananchi, kuitishwa mabaraza ya wilaya ya Katiba, uteuzi wa wajumbe wa Bunge la Katiba na kufanyika bunge lenyewe.
Kabla ya hapo, kwa upande wa Zanzibar kilio cha upinzani chini ya CUF kilikuwa ni kutaka muungano wa serikali tatu, baadaye ikaibuka hoja ya kutaka Muungano wa mkataba kabla ya kukubaliana na hoja ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba ya Muungano wa shirikisho wa Serikali tatu.
Hata hivyo, licha ya pendekezo hilo la Tume kukubaliwa na kuungwa mkono na vyama vya upinzani, hali ilikuwa tofauti kwa CCM na kilele cha msimamo wa chama hicho tawala kilikuwa ushauri wa Rais Kikwete alipokuwa akifungua Bunge Maalumu la Katiba alipoweka bayana kwamba chama chake kinataka kuendelea kwa mfumo wa Muungano wa serikali mbili kwa madai kwamba hauna gharama, una usalama zaidi, pia si hatarishi katika kuelekea kuvunja Muungano wenyewe. Kwa upande wa Zanzibar, hoja za pande mbili za CCM na CUF ikawa ni kulilia mafuta na gesi asilia ziliondolewe katika orodha ya mambo ya Muungano, fursa ya kukopa nje, kujiunga na taasisi za kimataifa na Rais wake awe katika itifaki ya Serikali ya Muungano kama sehemu ya mkuu wa nchi ikiwamo na nafasi za uongozi kwenye taasisi za muungano chini ya fomula maalumu.
CUF na viongozi wake wakiongozwa na Maalim Seif wakasema hawatakubali lolote hadi Zanzibar itakapokuwa na bendera yake, sarafu, benki kuu, mambo ya nje, polisi, uraia, uhamiaji na hati yake ya kusafiria.
Madai hayo yalipingwa vikali na CCM ikiongozwa na Dk Shein aliyesema madai hayo kiuhalisia yana ajenda ya siri na kulenga kuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa maelezo kuwa, kuhitaji hayo yafanyike ni kuunda dola mpya ndani ya dola iliyopo.
Maalim Seif na CUF wakasema bila ya mambo hayo kuwamo kitafanya kila linalowezekana kulikwamisha jambo hilo hasa kwa kutegemea nguvu ya turufu kwenye uamuzi wa theluthi mbili ndani Bunge la Katiba.
Mara baada ya Bunge la Katiba kuundwa, ulizuka mtafaruku ambao ulisibabishwa kundi la Ukawa linaloundwa na CUF, Chadema, NCCR – Mageuzi na NLD kususia Bunge la Katiba kwa maelezo kwamba lilikuwa likiwaburuza wajumbe kufuata matakwa ya CCM katika kutunga Katiba Inayopendekezwa.
Hatua hiyo ilizua jambo jipya katika mchakato huo; Bunge la Katiba lingefanikiwa kupitisha Katiba Inayopendekezwa au lingekwama? Hiyo ilitokana na ukweli kwamba karibu nusu ya wajumbe kutoka Zanzibar walikuwa upande wa Ukawa.
Kama ilivyotarajiwa, kura mbili tu ndizo zilizofanikisha kupitisha Katiba hiyo ambayo ilikabidhiwa kwa Rais Kikwete na Dk Shein tayari kusubiri kupigiwa kura Aprili mwakani.
Katika katiba hiyo Inayopendekezwa, mambo ya Muungano yamepunguzwa kutoka 22 hadi 16, Zanzibar imepata ruksa ya kikatiba kujiunga na taasisi za nje, kukopa na mafuta na gesi asilia kuondolewa katika mambo ya Muungano.
Pia Zanzibar imepata nafasi ya kujiunga na jumuiya za kimataifa, pia Rais wake kuwa Makamu wa Pili wa Rais. Vilevile, kuundwa tume maalumu ya usimamizi na utatuzi wa kero za muungano ambayo itakuwa chini ya Makamu wa Rais wa Muungano ikitambuliwa kikatiba.
Baada ya mchakato huo; CUF iliitisha mkutano mkubwa wa hadhara na Maalim Seif kusema kitafanya kila linalowezekana kukwamisha katiba hiyo inayopendekezwa isipigiwe kura za ndiyo ikisema haifai na inameza mamlaka ya Zanzibar hasa kifungu kinachompa Rais wa Muungano madaraka ya kugawa mipaka ya wilaya na mikoa kwa kushauriana na Rais wa SMZ.
Akijibu mapigo hayo katika mkutano uliofanyika hivi karibuni kwenye Viwanja vya Kibandamaiti; Dk Shein alisema Katiba hiyo inayopendekezwa imebeba masilahi ya umma yatokanayo na makundi ya kijamii, yakilenga kuondoa kero katika muungano na kwamba wakati ukifika, itapigiwa kura za ndiyo.
Rais huyo wa Zanzibar alisema hayo baada ya kuwapandisha kwa zamu mawaziri watano wa SMZ na wawili wa Muungano wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd kuitetea Rasimu Inayopendekezwa kuwa ni bora na inayokidhi haja na matakwa ya wakati.Dk Shein amenukuliwa akisema anamshangaa makamu wake wa Kwanza kwa kuwa ndiye aliyetaka uwekwe utaratibu wa kisera wa uchimbaji na utafutaji wa mafuta na gesi asilia, lakini baada ya jambo hilo kuondoshwa katika orodha ya mambo ya Muungano, ameendelea kupinga na kutaka Katiba Inayopendekezwa isipigiwe kura za ndiyo.
Alikwenda mbali na kusema kuwa wananchi watakuwa wamefanya makosa kutoiunga mkono Katiba Inayopendekezwa kwa madai kuwa imeleta majawabu kulingana na maswali magumu ya muda mrefu kuhusu kero za Muungano, pia ikifungua pazia jipya la mafanikio ya kiuchumi kwa Zanzibar.
Hata hivyo, Dk Shein alisema hofu walionayo wapinzani ni kuona ishara ya kushindwa kwao mwaka 2015 na kusisitiza kuwa kiboko kilekile kilichowachapa mwaka 2010 ndicho kitakachowachapa tena mwakani ingawa CUF na viongozi wake wanasema Dk Shein na CCM yake watakwenda na maji katika uchaguzi mkuu ujao.
Dk Shein alisema viongozi na wagombea wa CUF wamezoea kulalamika na kudai huibiwa kura zao na kusisitiza kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2015 utazidi kuwa huru na wa haki zaidi kuliko zote zilizopita na kutamba kwamba huenda ikiwa ndiyo tamati ya CUF.
Hakuna shaka kwamba kupishana kauli kwa viongozi hao wakuu wa Zanzibar kutaongezeka mwakani wakati wa kampeni za kura ya ndiyo au hapana kwa Katiba Inayopendekezwa na hicho kitakuwa kipimo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment