ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, November 29, 2014

INGEKUWA MIMI WEREMA, NISINGESUBIRI KUTIMULIWA, NINGEJIUZULU


Jaji Frederick Werema akizungumza jambo

Kwako Jaji Frederick Werema.

Najua katika siku za hivi karibuni umekuwa katika wakati mgumu sana kutokana na kushiriki kwako kwa namna moja au nyingine katika sakata la mabilioni ya Escrow. Najua jinsi ulivyochanganyikiwa lakini sina namna nyingine zaidi ya kukufikishia ujumbe huu, hata kama utakuchukiza.

Mimi sikuzaliwa Oktoba 10, 1955 kama wewe. Sikusoma Shule ya Msingi Wegero wala Sekondari za Bwiru na Songea Boys kama wewe. Sikuchukua Shahada ya Sheria pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhitimu mwaka 1984 kama wewe kabla ya kwenda Amenican University, Washington kuchukua Shahada ya Uzamili na kuhitimu mwaka 1993.

Sijawahi kuwa jaji wa mahakama yoyote wala sikuapishwa Oktoba 20, 2009 kushika wadhifa mkubwa wa mwanasheria mkuu wa serikali kama wewe. Mimi ni mkulima, mwananchi wa kawaida ambaye sijui chochote kuhusu sheria wala utawala, kwa kifupi mimi ni lofa wa kutupwa ambaye sina hata uhakika wa mlo wangu wa kila siku.

Hata hivyo, licha ya umbumbu wangu, ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, kwa hili sakata la Escrow linaloendelea kutingisha nchi yetu kwa kiasi kikubwa, kuliko hata lile la Richmond kipindi kile, walahi nakuapia nisingesubiri kuwajibishwa, mapema kabisa ningeshakubali kujiuzulu kiroho safi ili kupisha wenzangu wenye uwezo zaidi yangu waiokoe nchi hii.

Hata kabla ya ‘tumbili’ hawajaanza kuchonga na kuniita majina ya hovyo, wakinituhumu kushiriki katika ‘karamu ya waovu’ ya Escrow, ningeshakuwa nimejipima mwenyewe na kufikia uamuzi wa kuepusha mbawa zangu.

Ndiyo! Kwa nini niendelee kung’ang’ania kukaa madarakani wakati kazi kubwa niliyopewa na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete siku ile aliyoniapisha, ya kuhakikisha nasimamia masuala yote yahusuyo sheria, ili kulinda mali za umma imenishinda?

Ningeshakuwa nimegundua ‘nilivyobugi’ kuanzia pale Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi aliponiandikia barua ya kuomba msaada wa kisheria kuhusu mgogoro wa IPTL na Tanesco na malipo ya mabilioni ya fedha yaliyokuwa yakitakiwa kulipwa kwa kampuni hiyo iliyoingia mkataba na Tanesco wa kuzalisha umeme wa dharura baada ya nchi kukumbwa na ukame mkubwa.

Ripoti za Mkaguzi ya Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ile ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) zote zinakutia kitanzini kwamba licha ya Maswi kuomba msaada wa kisheria kwako, uliamua kumpuuza na kwa kuona anakuwekea kiwingu, ukaanza kuwasiliana moja kwa moja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile ili kuhakikisha kuwa fedha hizo zinalipwa haraka.

Ripoti ya CAG inazidi kushindilia msumari kwamba ulishauri kuwa fedha hizo zilipwe kwa IPTL ili jambo hilo lifungwe na kuiwezesha serikali kujiepusha na mashauri yasiyo na tija kwake! Yaani kwako wewe, serikali kulipa isivyo halali shilingi bilioni 306 kutoka kwenye akaunti ya Escrow, siyo shauri lenye tija? Hauwezi kuwa ‘serious’, ningekuwa mimi ningeshauona ‘uozo’ nilioshiriki ndani yake, nikiwa najua au nikiwa sijui na haraka sana ningeshatangaza kujiuzulu, nisingesubiri aibu hii.

Kibaya zaidi, licha ya kuhalalisha mabilioni hayo kulipwa, ripoti inaweka kabaya kwamba ulimuandikia barua Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Profesa Benno Ndulu kuwa hakukuwa na kodi ya VAT katika fedha zilizokuwepo kwenye akaunti ya Escrow, ukasababisha hasara nyingine ya mabilioni ya fedha ambayo yalilipwa bila kukatwa kodi!

Siwezi kuthibitisha tuhuma kwamba ulipokea mlungula wa dola milioni 5 za mahakama ili kuupeleka mchakato huo ‘fastafasta’ kwa sababu mimi siyo mahakama wala sina ushahidi ila walahi nakuapia, ningekuwa mimi kwenye nafasi yako, nsingesubiri kuja kung’olewa kwa aibu, ningeshang’atuka tangu mwanzo.

Wasalaam. GPL

No comments: