ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 17, 2015

2,000 wakimbia kwao kwa hofu ya kukeketwa Tarime.



Wasichana 2,003 wamezokimbia familia zao na kwenda kuishi katika kituo cha Masanga Wilaya ya Tarime mkoani Mara kwa hofu ya kukeketwa na wazazi wao.

Hayo yalibainishwa na Mlezi wa kituo hicho, Germaine Baibika, wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa kupinga ukeketaji ulioandaliwa na Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) uliowashirikisha wadau wa kupinga ukeketaji na ndoa za utotoni.

Baibika alisema takwimu hizo ni tangu mwaka 2008 na idadi hiyo ni tangu walipoanza kupokea wasichana wanaokimbia ukeketaji.

Alisema wasichana wengi wanaokimbilia kwenye kituo hicho wanatoka wilaya za Tarime, Serengeti, Rorya, Loliondo na wengine nchi jirani ya Kenya.

Alitaja changamoto wanazopata katika kupambana na ukeketaji kuwa ni upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa kimila ambao wangependa kuona mila hizo zinadumishwa.

Alisema umaskini wa kupindukia kwenye baadhi ya kaya ndiyo husababisha kulazimika kukeketa watoto wao kwa matarajio kuwa watapata mahari watoto wao watakapoolewa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Watoto katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Benedict Misani, alisema wasichana na wanawake milioni 7.9 nchini wamekeketwa licha ya kuwapo sheria ambayo inazuia vitendo hivyo na kwamba hali hiyo inachangiwa na baadhi ya watendaji wa serikali kutokuwa tayari kumaliza tatizo hilo.

Alipongeza juhudi za wanaharakati binafsi ikiwamo CDF kwa kupinga ukeketaji na kuziomba asasi hizo kuendelea kushirikiana na serikali kubuni mikakati mipya ya kijamii itakayoleta suluhisho la kudumu kuhusiana na tatizo hilo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF), Konsuma Mtengeti, alisema asasi binafsi zinajitahidi kupambana na tatizo hilo lakini ukosefu wa utashi wa kisiasa ndiyo unaokwamisha kulimaliza.
SOURCE: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

hivi mtoto huwa anaolewa?na mtoto huwa anahesabiwa kwa umri wake au ukuaje wake?
acheni zenu nyinyi badala ya kuzungumzia katiba iliyochakachuliwa na wizi wa escro wakurudishiyeni pesa zenu mmebaki na ushamba huu.