Mtikila anapinga kuanzishwa Mahakama ya Kadhi, kwamba ni kinyume cha Katiba ya nchi.
Kadhalika, Mtikila ameiomba mahakama itoe amri kwamba wale walio kwenye mamlaka ya Serikali akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Dk. Mary Nagu; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na wenzao watoe sababu kwa nini wasifungwe kifungo kisichopungua miaka mitano endapo watashindwa kujieleza.
Pia, Mtikila kupitia hati yake ya madai iliyopewa usajili namba 14 ya mwaka huu, ameomba Mahakama itoe amri vigogo hao kufungwa kifungo hicho kutokana na kuchezea Katiba ambayo ni sheria mama ya nchi.
Katika hati hiyo, Mtikila pia anaiomba, mahakama itoe amri kwamba Mahakama ya Kadhi na Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC), zitangazwe kuwa ni haramu nchini.
Pamoja na mambo mengine, Mchungaji Mtikila anadai kuwa hatua serikali kuandaa muswada wa Kiislamu na kuuwasilisha bungeni na kitendo cha Bunge kukubali badala ya kuukataa ni sawa na uhaini, kinachofanywa na wale walioupeleka muswada huo.
Anadai kuwa kitendo hicho ni sawa na uvunjifu mkubwa wa viapo vya viongozi hao. “Viapo ambavyo Pinda na wenzake waliapa wakati wa kushika madaraka ya umma vinakiuka ibara ya 19 ya katiba ya nchi inaosisitiza kwamba masuala ya dini na kuabudu yatakuwa ni ya mtu binafsi na kwamba uendeshaji wa mambo au taasisi za kidini hazitakuwa sehemu ya mamlaka ya nchi,” anaeleza katika madai yake.
Hati hiyo inaeleeza kuwa mamlaka ambazo zimepigwa marufuka na Katiba kujiingiza, kujihusisha au kuchezea mambo kama ya kadhi na uanachama wa taasisi za kidini au uanachama wa uislamu ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu au viongozi wote wa kiserikali ambao baada ya kula viapo hujifunga kulinda katiba ya nchi na si vingevyo.
Mtikila anaendelea kueleza kupitia hati hiyo kwamba muswaada wa mahakama ya kadhi na uanachama wa OIC havikubaliki katika ardhi ya Tanzania kwa sababu zinabagua na ni ukiukaji mkubwa wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alieleza kuwa sababu nyingine ya kufungua kesi hiyo ni kwa ajili ya kuilinda katiba ya nchi kwamba ibara ya 26 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, inasema kwamba kila mtu ana haki kwa mujibu wa taratibu zilizoanishwa na kuchukua hatua za kisheria kwa lengo la kuhakikisha kwamba Katiba ya nchi inalindwa.
Alidai kuwa ametumia haki hiyo kufungua kesi hiyo akiitaka mahakama itoe adhabu kwa mamlaka za nchi zilizochezea Katiba na wengine.
Mtikila anaiomba Mahakama kumwamuru walalamikiwa kulipa gharama zote za kesi pamoja na amri nyingine itakayoona zinafaa.
KUTIKISA BUNGE
Wakati Mkutano wa 19 wa Bunge ukianza leo, baadhi ya wabunge wameeleza kuwa mambo makuu matatu yanatarajia kulitikisa Bunge hilo likiwamo muswada wa Mahakama ya Kadhi iwapo utawasilishwa na kwamba busara na hekima visipotumika litaleta mpasuko mkubwa nchini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na NIPASHE mjini Dodoma, wabunge hao walisema mbali na mahakama hiyo, mambo mengine yanayoweza kuibua mvutano bungeni ni mchakato wa kura ya maoni kwa ajili ya katiba inayopendekezwa na mabehewa feki yaliyonunuliwa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).
Mbunge wa Lushoto (CCM), Henry Shekifu, alisema kama muswada wa Mahakama ya Kadhi utapelekwa bungeni utaleta mvutano mkali na kwamba kinachohitajika ni hekima itumike ili kufikia muafaka.
“Suala la Mahakama ya Kadhi bila shaka likiletwa bungeni litakuwa moto sana kwa sababu masikio ya wananchi ni kutaka kusikia nini kitaamuliwa katika suala hili,” alisema.
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alisema serikali inatakiwa kuliangalia suala la Mahakama ya Kadhi kwa undani zaidi kabla ya kulifikisha bungeni.
Kafulila alisema kinachotakiwa kufanyika kwanza ni pande zote zinazovutana katika suala hilo na serikali ichukue hatua kusuluhisha ili ziafikiane kabla ya kukimbilia kulipeleka bungeni.
Alisema suala lingine ambalo wabunge watataka kupata majibu kutoka serikalini ni ununuzi wa mabehewa feki yaliyonunuliwa na TRL.
“Tunasikia kuna tume iliundwa kuchunguza suala hili, lakini hadi sasa majibu ya tume hiyo bado hayajawekwa wazi, tutataka kujua kwa nini suala hilo limekuwa hivi,” alisema Kafulila.
Kuhusu kura ya maoni kwa ajili ya Katiba inayopendekezwa, alisema inasikitisha kuona fedha za umma zinapotea bure kufanya maandalizi wakati inafahamika kuwa suala hilo kamwe haliwezi kufanyika kutokana na muda uliobaki kuwa mfupi.
Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse, alisema serikali isifanye mchezo katika suala la Mahakama ya Kadhi
“Tangu uhuru serikali iliweka wazi kuwa haina dini, sasa suala la kuleta muswada wa Mahakama ya Kadhi ni kutaka kuondoa amani iliyopo katika nchi,” alisema.
Alisema serikali isifanye dhihaka katika suala hilo na kuwa inachotakiwa kufanya ni kuwaeleza ukweli Waislamu na Wakristo kwamba suala hili haliwezekani kuliko kuwahadaa, hali inayoweza kuleta machafuko nchini.
Hata hivyo, Ofisa Habari wa Bunge, Propers Minja, akizungumza na NIPASHE, alisema katika ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge kuhusiana na mambo yatakayofanyika katika mkutano huo suala la Mahakama ya Kadhi halimo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa, mkutano huo utakuwa mahsusi kwa ajili ya kushughulikia miswada ya sheria.
Imeeleza kuwa miswada ya sheria sita itawasilishwa kwa mara ya kwanza na 15 kwa mara ya pili.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliviambia vyombo vya habari kuwa muswada wa Mahakama ya Kadhi utawasilishwa katika Mkutano wa 19, akisema hatua hiyo imechukuliwa na serikali baada ya kukutana na wadau wote.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment