Monday, April 13, 2015

Ahadi ya Matumla, aibu nyingine katika ngumi



Bondia Xin Hua kutoka China (kushoto) akitambiana na Matumla Jr wa Tanzania 


Ni michezo ambayo imekosa udhamini wa uhakika na ambayo haijaungwa mkono na serikali kwa kiasi kikubwa kama ilivyo katika mchezo wa soka.

BAADA ya soka, michezo inayoongoza kupendwa na mashabiki wengi nchini ni ngumi, riadha na kikapu.
Ni michezo ambayo imekosa udhamini wa uhakika na ambayo haijaungwa mkono na serikali kwa kiasi kikubwa kama ilivyo katika mchezo wa soka.
Pamoja na hali hiyo, lakini wenye mapenzi ya kweli na michezo hiyo hawajakaa nyuma katika kutoa mchango wao na mara kwa mara juhudi za watu hao zimekuwa zikionekana.


Ni hivi karibuni tu tumesikia habari za maandalizi ya pambano la ngumi kati ya Mohammed Matumla na bondia kutoka China, Wang Xin Hua zilivyokuwa kwa kiwango cha juu.


Katika pambano hilo lililofanyika Machi 27 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, yalikuwapo mapambano mengine ya utangulizi lakini lile la Matumla na Xin Hua ndilo lililokuwa likisubiriwa kwa hamu.


Hata baadhi ya mashabiki wa ngumi ambao hawakuonekana muda mrefu siku hiyo walifika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee kushuhudia pambano hilo ambalo pia lilivuta mashabiki raia wa China wanaoishi nchini ambao walifika kwa ajili ya kumuunga mkono Mchina mwenzao, Xin Hua.


Pamoja na sababu nyingine nyingi, lakini sababu moja kubwa iliyolifanya pambano hilo lisubiriwe kwa hamu ni ahadi kwamba mshindi katika pambano hilo angekwenda nchini Marekani kupigana katika pambano la awali kati ya Floyd Mayweather Junior na Manny Pacquiao.


Mayweathter na Pacquiao wanatarajiwa kupanda ulingoni Mei 2 mwaka huu mjini Las Vegas, Marekani pambano linalotajwa kuwa la kukata na shoka dhidi ya mabondia waliojiwekea heshima ya kipekee katika mchezo wa ngumi.


Kwa mantiki hiyo, ahadi kwamba Mtanzania angekuwa miongoni mwa mabondia ambao wangepigana awali kabla ya Mayweather na Pacquiao kupanda ulingoni lilikuwa ni jambo kubwa na la kihistoria kwa Tanzania.


Ni wazi kwamba fursa hiyo ingemtangaza Matumla na Tanzania katika mchezo wa ngumi duniani kote kwa kuwa pambano la Mayweather na Pacquiao ni gumzo karibu kote duniani.


Hatimaye Matumla alipigana akaibuka na ushindi uliopokelewa kwa vigelegele na mashabiki wa ngumi waliokuwa kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee.


Kilichokuwa kikizungumzwa na mashabiki wengi baada ya ushindi huo ni safari ya Matumla kwenda Marekani hasa baada ya kujikatia tiketi kwa kumtwanga Mchina.Mashabiki wengine walipenda kumjua mpinzani wa Matumla angekuwa nani katika pambano lake la Marekani.


Hata hivyo, katika hali ya kusikitisha na ambayo pia inashangaza ubabaishaji umechukua nafasi yake na sasa ni dhahiri kwamba safari hiyo ya Marekani haipo na kwamba ahadi iliyotolewa ni sehemu ya ubabaishaji katika mchezo wa ngumi.


Matukio ya aina hii ya ubabaishaji yana historia ndefu katika mchezo wa ngumi lakini ambayo yamekuwa yakisikika mara kwa mara ni mabondia kunyimwa haki zao au kupunjwa.


Miaka kadhaa iliyopita kilio kikubwa cha mabondia ni kupunjwa haki zao na wengine walinyimwa mapambano kwa sababu tu ya kukataa kusaini mikataba kabla ya pambano.


Wako ambao walidiriki kuwabwatukia hadharani mapromota na wengine kuwakana mameneja hadharani baada ya kuhisi kufanyiwa ubabaishaji.


Kwa hali hiyo, kilichomkuta Matumla ni sehemu ya matukio ya ubabaishaji ambayo ni vizuri yakakomeshwa ili kuufanya mchezo wa ngumi upige hatua.
Credit:Mwanaspoti

No comments: