Sunday, October 27, 2024

DKT NCHEMBA AHIMIZA MATUMIZI YA KISWAHILI MIKUTANO YA BENKI YA DUNIA NA IMF


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba madelu (Mb), akiteta jambo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Bi. Victoria Kwakwa (kushoto), Makao Makuu ya Benki ya Dunia, Jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo alijadili masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Tanzani na Benki hiyo.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba madelu (Mb), akiteta jambo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Bi. Victoria Kwakwa (kushoto), Makao Makuu ya Benki ya Dunia, Jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo alijadili masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Tanzani na Benki hiyo.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba madelu (Mb), akiwa katika picha na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Bi. Victoria Kwakwa Makao Makuu ya Benki ya Dunia, Jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo alijadili masuala kadhaa ya ushirikiano kati ya Tanzani na Benki hiyo.

Na Benny Mwaipaja, Washington D.C
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amerejea wito wa Tanzania kwa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kukifanya Kiswahili kuwa miongozi mwa lugha rasmi za mawasiliano katika mikutano ya Taasisi hizo kubwa za Fedha Duniani.

Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo alipoongoza Ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, Jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambako Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF na Benki ya Dunia inafanyika.

Amesisitiza kuwa Kiswahili ni lugha ya Afrika na pia ni lugha rasmi inayotumika katika Mikutano ya Umoja wa Afrika hivyo imefika wakati kwa Taasisi hizo kubwa za Fedha Duniani kukifanya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha zinazotambulika rasmi na kutumika katika Mikutano ya Benki ya Dunia na IMF.

Katika hatua nyingine, Dkt. Nchemba ameishukuru pia Benki ya Dunia kwa kuahidi kusaidia ujenzi wa mradi mkubwa wa Reli ya Kisasa SGR, unaoendelea nchini Tanzania kwa kuwa mradi huo ni miongozi mwa miradi ya kipaumbele ya kitaifa kutokana na umuhimu wake katika kukuza biashara na uchumi wa nchi na mataifa mengine yatakayounganishwa na Reli hiyo.

Aidha, Dkt. Nchemba, ametoa shukrani kwa uamuzi wa Benki ya Dunia, kubeba ajenda ya kuwawezesha na kuwajengea uwezo wakandarasi wa ndani ili waweze kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini Tanzania kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia na IMF badala ya mfumo wa sasa unaowanufaisha zaidi wakandarasi wa kigeni.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki, Bi. Victoria Kwakwa, aliahidi kuwa Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa kuiwezesha kutimiza malengo yake ya kimaendeleo na kiuchumi kupitia misaada ya kiufundi na kifedha.

Bi. Kwakwa ameeleza kuwa mradi wa Reli ya Kisasa wa SG, mradi wa kusambaza nishati ya umeme hususan vijijini, kuwawezesha wakandarasi kupata zabuni za miradi na mradi wa kuboresha elimu ni miongoni mwa mipango itakayopewa kipaumbele ili kuharakisha maendeleo ya watu na kuimarisha uchumi wa Tanzania.

Ameipongeza Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wa Kilele cha Nishati utakaofanyika Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi Januari mwakani (2025), ambapo itasainiwa mikataba ya ufadhili wa usambazaji wa nishati kwa nchi 15 za kwanza zilizoteuliwa kunufaika na mpango huo ikiwemo Tanzania, ambapo lengo la mkakati huo ni kuwafikia zaidi ya watu milioni 300 Barani Afrika kwa kuwaunganisha na umeme ifikapo mwaka 2030.



No comments: