ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 7, 2015

Wagombea urais CCM wafunguka kauli ya Rais Kikwete

Rais Jakaya Kikwete akitoa mhadhara katika kituo cha Kimataifa cha Woodrow Wilson jijini Washington DC, nchini Marekani. Picha na Ikulu

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa nafasi hiyo ni kadhia na kazi ngumu, baadhi ya wanasiasa waliotangaza nia ya kuwania nafasi hiyo wamesema wanafahamu changamoto hizo na kwamba kauli hiyo inazidi kuwapa nguvu na hamasa ya kuendelea na mchakato huo.
Wiki iliyopita, Rais Kikwete akiwa Marekani, wakati akihutubia kwenye taasisi ya Wood Wilson International Center for Scholars alielezea mafanikio na changamoto alizokumbana nazo wakati wa uongozi wake wa miaka 10 unaomalizika Oktoba, mwaka huu na kusema:
“Wakati unaingia Ikulu unakuwa na shauku kubwa sana pamoja na furaha ya ushindi, lakini hakika urais ni kadhia kubwa. Ukipata fursa ya kuwa rais kwa awamu mbili kama mimi nadhani zinatosha kabisa. Nimefanya mengi kwa nchi yangu atakayekuja ataendeleza nilipoishia.”
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja wakati makada wa CCM wakipigana vikumbo kuwania urais.
Miongoni mwa wanasiasa waliotangaza na waliotajwa katika kinyang’anyiro hicho cha kurithi kiti kitakachoachwa wazi na Rais Kikwete ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Pia wamo, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Msimamo wa January
Akizungumza jana kuhusiana na kauli hiyo ya January alisema kauli hiyo inampa hamasa kwa nia yake ya kutaka kuwania urais.
“Nilitangaza nia hiyo huku nikiwa nafahamu kwa asilimia 100 uzito wa jambo hilo... kufahamu changamoto hizo ndiyo moja ya vitu vilivyonisukuma kuchukua uamuzi huo,” alisema.
Alisema moja ya changamoto ambazo ameshakumbana nazo alisema: “Kwanza mimi nina bahati sana. Wakati nikiwa msaidizi wa Rais kipindi anagombea nafasi hiyo, nilipata fursa ya kutembea naye nchi nzima na kuona mambo mengi.”
Mbunge huyo wa Bumbuli, alisema haikuwa kazi rahisi kufanya kampeni za kuhamasisha Watanzania wampigie kura Rais Kikwete... “wakati ule tulikuwa tunatembea katika maeneo mbalimbali nchini. Ukiwa umesimama jukwaani unaona sura za watu zilivyojawa na shauku… pale nilijifunza na kuona ukubwa wa changamoto za uongozi.
Nimebahatika pia kuona changamoto mbalimbali ambazo uongozi wa sasa umekumbana nazo kwa kipindi nilichowatumikia hadi sasa. Hiyo ni nafasi nzuri ya mimi kujifunza na kufahamu ni namna gani ninaweza kukabiliana nazo.
“Kutokana na uzoefu wangu wa kufanya kazi na kiongozi huyo naamini kwamba zipo nyakati ambazo Watanzania tungepitia shida nyingi, lakini kutokana na busara na hekima yake nchi imeendeshwa vyema,” alisema na kuongeza: “Ndiyo maana nasisitiza kuwa nchi yetu inahitaji kiongozi mwenye hekima na busara.”
Naibu Waziri huyo ambaye alitangaza nia ya kuwania urais Julai mwaka jana, huku akisema kuwa huu ni wakati wa kupisha fikra mpya kuongoza dola alisema nafasi hiyo ina sura mbili kwamba urasi ni kama taasisi na upande mwingine ni mtu mwenyewe.
“Nawaonea huruma wale wanaodhani kuwania nafasi hiyo ni sherehe. Nafasi hii inahitaji mtu mwenye afya nzuri, hekima na busara ya hali ya juu kwani atakuwa anafanya uamuzi kwa nchi. Watu wanadhani urais ni ushabiki… hakuna kitu kama hicho.”
Mtazamo wa Sumaye
Sumaye ambaye aliwahi kunukuliwa na vyombo vya habari akisema wakati ukifika atatangaza rasmi nia yake, alisema: “Kama mtu ameamua kuwania nafasi hiyo ina maana anafahamu anachokitaka. Tunajua ziko changamoto na namna ya kukabiliana nazo kwa hiyo hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.”
Dk Kigwangalla
Akizungumzia kauli hiyo, Dk Kigwangalla alisema: “Kauli kama hiyo haiwezi kumvunja mtu moyo, ari itabaki palepale tu kwa aliyetangaza nia. Aliyetangaza nia anataka kutoa utumishi wake kwa nchi yake kama mimi.”
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

One who is roaming around most of the time, and therefore doing little in his office always finds delivery of presidential duties hard to accomplish. Ni yapi zaidi ya kuzurura na kuhani misiba hapa na pale aliyoyafanya JK kama rais?