ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 18, 2015

Asimamishwa kazi kwa kumtumia JK ‘meseji’


Moshi. Mhasibu wa Hospitali ya Rufaa KCMC, Paul Mhumba amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kutuma ujumbe wa simu ya mkononi (sms) kwa Rais Jakaya Kikwete.
Kuvuja kwa ujumbe huo na nambari ya simu iliyotuma, kumeibua hisia tofauti kuhusu usiri wa ofisi ya Rais katika kushughulikia malalamiko nyeti ya wananchi na kuwaweka njiapanda watoa habari za siri.
Mhumba, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (Tughe) Tawi la KCMC anadaiwa na Menejimenti ya KCMC kuwa ndiye aliyetuma ujumbe huo.
Katika barua yake ya Mei 5, yenye kumbukumbu PF.4515/22, KCMC ilidai uchunguzi umebaini kuwa Mhumba ndiye mtumaji wa ujumbe huo.
“Uongozi umepokea taarifa iliyotumwa mwishoni mwa Aprili na mwanzoni mwa Mei mwaka huu kwa njia ya ujumbe wa simu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Jakaya Kikwete,” ilidai.
KCMC imedai katika barua hiyo, taarifa hiyo ya sms ilibeba ujumbe unaohusiana na matumizi mabaya ya fedha za hospitali hiyo unaofanywa na baadhi ya viongozi na Shirika la Msamaria Mwema (GSF).
Mbali na tuhuma hizo, lakini pia KCMC inadai taarifa hiyo ilimweleza Rais kuwa KCMC na GSF linalomiliki hospitali hiyo, zinajitosheleza kwa mapato, hivyo hakuna haja kwa Serikali kuendelea kuipatia ruzuku.
Pia, menejimenti imedai taarifa hiyo ilidai wafanyakazi wa KCMC wanatumikishwa kama watumwa, hivyo ni maombi yao (watumishi) Serikali ilegeze masharti ili ajira zao zichukuliwe na Serikali.
“Uchunguzi umeonyesha kuwa taarifa hiyo (kwa Rais), umeituma kwa kutumia simu ya kiganjani ambayo ulikabidhiwa kama mojawapo ya zana ya kuleta ufanisi katika majukumu yako,” imedai.
Mei 8, KCMC ilimwandikia barua Mhumba yenye kumbukumbu PF.4515/28 iliyotiwa saini na Profesa Raimos Olomi ikimjulisha kuwa amesimamishwa kazi kuanzia Mei 8 hadi Mei 14.
Katika barua hiyo, Profesa Olomi alidai menejimenti imepokea taarifa ya kutofanyika kwa kikao cha kamati ya nidhamu baada ya Mhumba kumkataa mwenyekiti kutokana na kukosa imani naye.

Pia, kikao hicho hakikufanyika baada ya Mhumba kuomba kamati hiyo iahirishwe kwa sababu mwakilishi wake hakuwapo na kikao kingine kupangwa Mei 15.

Chanzo: Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

duh -- kazi kweli!

Anonymous said...

SISIMIMU MAJANGA KWELI LAKINI WATASHINDA KWA UFISADI WAO NA PESA ZAO ZA SEMBE ZITAWAHONGA WENGI SANA.MAFISADI HAWA MUNGU ATALAANI KUNA SIKU