ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 6, 2015

Mjue DK Willibroad Slaa: Katibu Mkuu wa Chadema

Historia yake
Dk Willibrod Slaa ni Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Slaa alizaliwa Oktoba 29, 1948 kijijini Kwermusi, Wilaya ya Mbulu (Oktoba atafikisha umri wa miaka 67). Slaa alisoma Shule ya Msingi Kwermusi iliyoko wilayani Mbulu mwaka 1958-1961 na baadaye Shule ya Kati (Middle School) ya Karatu kati ya mwaka 1962-1965.
Baada ya darasa la nne, Dk Slaa alijiunga na Seminari ya Dung’unyi mkoani Singida mwaka 1966-1969 na kusoma sekondari, kisha akaendelea na masomo ya juu ya sekondari katika Seminari ya Itaga mkoani Tabora mwaka 1970 na 1971, alikohitimu kidato cha sita.
Alipomaliza kidato cha sita katika Seminari ya Itaga alikuwa amekwishafanya maamuzi ya kufanya utumishi wa kanisa. Alijiunga na Seminari ya Kibosho mwaka 1972-1973 na kupata stashahada ya Falsafa iliyompa sifa ya kudahiliwa na Seminari Kuu ya Kipalapala iliyoko Tabora kati ya mwaka 1974 na 1977 na alipata fursa ya kubobea zaidi katika masomo ya falsafa na theolojia, huku pia akisoma Stashahada ya Theolojia katika Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.
Dk Slaa alianza kuwa kiongozi tangu alipokuwa mwanafunzi pale Kipalapala ambapo alichaguliwa kuwa Rais wa Wanafunzi, mapadri nilioongea nao wanasema alikuwa mmoja wa viongozi wazuri sana kupata kuongoza Kipalapala.
Baada ya safari ndefu ya kuusaka “utumishi wa Mungu” Slaa alipadirishwa (alipewa upadri rasmi) mwaka 1977 na baada ya utumishi wa miaka michache alijiunga na Chuo Kikuu cha Pontifical Urbaniana nchini Italia akisomea udaktari wa Sheria za Kanisa maarufu kama J.C.D. (Juris Canonici Doctor ) au I.C.D. (Iuris Canonici Doctor) kati ya mwaka 1979 na 1981. Katika mfumo wa Kanisa Katoliki, (J.C.D au I.C.D) ndiyo shahada ya juu kabisa katika masomo ya sheria ya kanisa.
Dk Slaa amefanya kazi mbalimbali katika taasisi za Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Amewahi kuwa Msaidizi wa Askofu na Mkurugenzi wa Maendeleo katika Jimbo la Mbulu. Amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kwa muda wa miaka tisa (mihula yote mitatu). TEC ndiyo chombo cha juu cha usimamizi wa mambo ya Kanisa Katoliki hapa Tanzania.
Kwa mujibu wa Profesa Kitila Mkumbo, mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katika utafiti wake juu ya Dk Slaa, anasema “…Dk. Slaa anaelezwa kama Katibu Mkuu mwenye ufanisi mkubwa zaidi tangu TEC ianzishwe. Miundombinu mingi ya Kanisa Katoliki nchini ilianzishwa na kukamilishwa katika kipindi ambacho Dk Slaa alikuwa Katibu Mkuu wa TEC.”
Dk Slaa alijitoa kwenye upadri mwaka 1991. Kwa mujibu wa taarifa za maaskofu kadhaa nilioongea nao, wanasema “Dk Slaa lifanya hivyo kwa kufuata taratibu kamili ndani ya Kanisa Katoliki na aliacha yeye mwenyewe bila kushinikizwa, kufukuzwa au kupewa onyo”.Mara kadhaa Dk Slaa alipoulizwa kwa nini aliamua kuachana na upadri, amekuwa akikaririwa akisema kwamba “kuna mambo ambayo alidhani dhamira yake ilipingana nayo na akaona asingeliweza kuendelea, japokuwa anasisitiza kuwa masuala hayo ni binafsi zaidi.”
Ndani ya Chadema amewahi kushikilia wadhifa wa Makamu Mwenyekiti, kabla hajachaguliwa kuwa Katibu Mkuu katika mwaka ambao Freeman Mbowe alichaguliwa kuwa mwenyekiti na wameendelea kuongoza kwa pamoja hadi hivi sasa.
Dk Slaa ni mwandishi mzuri wa vitabu, ameandika vitabu vitatu ambavyo ni Utimilifu wa Msichana (1977), Utimilifu wa Mvulana (1977) na Expediency and Exigency Liturgical Legislation (1981). Pia, kiongozi huyu anazungumza lugha nane kwa ufasaha; Kiswahili, Kiingereza, Kilatini, Kiitaliano, Kijerumani, Kihispania, Kireno na Kifaransa.
Dk Slaa aliwahi kumuoa Rose Kamili na kuzaa naye watoto wawili, Emiliana Slaa na Linus Slaa lakini waliachana muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Hivi sasa anaishi na “mchumba wake” Josephine Mushumbushi na wamepata mtoto mmoja.
Mbio za ubunge
Dk Slaa aliingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kwa mara ya kwanza mwaka 1995, akiomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa jimbo la Karatu mkoani Arusha kwa tiketi ya CCM na alishinda kwenye kura za maoni za chama hicho. Vikao vya CCM vilipokutana Dodoma vikamuengua na kumuweka mbunge aliyekuwa anamaliza muda wake, Patrick Qorro. Wananchi wa Karatu wameniambia kuwa iliwapasa wamshinikize Dk Slaa kuchukua fomu na kugombea ubunge kupitia chama kingine. Bahati ikakidondokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Dk Slaa alipambana na wagombea kutoka vyama vinne; CCM, UDP, CUF na NCCR na aliwashinda wote kwa kupata asilimia 52.6, akifuatiwa na Patrick Qorro wa CCM aliyepata asilimia 44.1. Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, Dk Wilibrod Slaa alishiriki kwenye uchaguzi akigombea kutokea Chadema kwa mara pili na kupata ushindi mkubwa zaidi kuliko mwaka 1995 na aliongoza hadi mwaka 2000. Na kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 pia aligombea ubunge kwa mara ya tatu jimboni Karatu na kushinda kwa asilimia 50.65 dhidi ya asilimia 49.0 za Patrick Tsere wa CCM.
Kati ya mwaka 2005– 2010 naweza kusema kuwa Dk Slaa ndiye alikuwa shujaa wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na namuona kama mbunge aliyefanya kazi kubwa kitaifa na kimataifa kushinda mbunge mwingine yeyote. Huu ndiyo wakati ambapo yeye na Zitto Kabwe na wabunge wengine wachache walikuwa mwiba usioshikika bungeni. Hoja zao nzito kuhusu ufisadi, rushwa, uwajibikaji duni wa serikali vilimfanya kila Mtanzania aone nini maana na umuhimu wa Bunge la Wananchi.
Mbio za urais
Dk Slaa aliteuliwa na Chadema kugombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010. Kwa sababu ya umahiri wake wa kujenga hoja na kuonyesha kuwa ana uwezo wa kipekee, aliibuka katika nafasi ya pili, akipata asilimia 27.05 za kura zote, kwa kuachwa na Jakaya Kikwete wa CCM aliyeongoza kwa kupata asilimia 62.83.
Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2015, Dk Slaa ni mmoja wa wanasiasa mahiri kutoka ndani ya vyama vya upinzani ambao wanatajwa kuwa na sifa, uwezo na vigezo vya kuongoza nchi.
Nguvu yake
Jambo la kwanza ambalo linampa nguvu Dk Slaa ni elimu yake. Huyu ni kiongozi mwenye stashahada tatu pamoja na shahada ya Uzamivu (PhD). Anayo Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Sheria ya Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha St. Urban, Rome. Pia ana stashahada ya Theolojia kutoka Kipalapala Seminari, Stashahada ya falsafa kutoka Kibosho Seminari, Stashahada ya Afya ya Macho kutoka Kituo cha Kimataifa cha Macho.
Pamoja na kwamba hakusoma katika mfumo wa kiserikali zaidi hapa Tanzania na amekuwa “Padri” katika kanisa, kwa kiasi kikubwa masuala ambayo ameyasimamia kutokana na elimu yake yamekuwa ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kimataifa zaidi. Mapadri wengi husoma falsafa na hawana tofauti yoyote na wasomi wa kawaida wanaosoma falsafa vyuoni na baadaye kuajiriwa katika kazi za kawaida.
Pili, Dk Slaa ana sifa kubwa sana katika kufanya kazi kwa juhudi “kuchapa kazi”. Mimi nimefanya naye kazi kwa miaka kama miwili hivi katika mazingira tofauti. Nimeshuhudia namna ambavyo hawezi hata kutoka nje kunyoosha mgongo kama mko vikaoni, mnaweza kujadiliana kutwa nzima na mkatoka hapo kukimbizana mahali kuhutubia wananchi asinywe hata maji. Slaa ana uwezo mkubwa sana kwenye eneo hili na kwa hakika nadhani nchi inahitaji Rais anayechapa kazi kufa au kupona.
Nguvu ya tatu ya kiongozi huyu ni uadilifu. Dk Slaa amewahi kufanya kazi katika maeneo mengi tu tangu akiwa Padri wa Kanisa Katoliki, hadi amekuwa mbunge kwa miaka 15 huku akiongoza Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa. Hata mara moja hatukuwahi kusikia harufu, tuhuma au maneno kuwa amekwapua “senti” za umma au amechukua fedha za rushwa mahali. Kazi alizofanya ni safi na salama na zinampa “mamlaka ya kimaadili” (moral authority) kusimama hadharani na kusema kuwa atapambana na rushwa na ufisadi. Naamini, watu wa aina yake, kwa sasa ni muhimu sana katika nchi na uongozi wa nchi.
Nne ni kuheshimika na umaarufu. Dk Slaa ni mmoja wa viongozi wa upinzani wanaoheshimika na kufahamika sana hapa nchini Tanzania. Lakini pia sifa hizo zinavuka mipaka ya Tanzania ambako nako amefanya kazi za utumishi muda mrefu huku akiendelea kupata mialiko mikubwa ya nchi kama Marekani, nchi za Ulaya, ambako amekaribishwa katika vyuo vikuu bora kabisa duniani na kutoa mihadhara. Kwa hiyo anatambulika na kuheshimika kama mmoja wa Waafrika wanaotoa mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko na maendeleo ya jamii zao. Sifa za namna hii ni nguzo muhimu kwa mtu anayetajwa kuwa na vigezo vya urais.
Udhaifu wake
Udhaifu wa Dk Slaa uko kwenye eneo la uchujaji wa taarifa anazopewa juu ya masuala mbalimbali na hata kuzifanyia maamuzi sahihi. Kwa kipindi kirefu nimekuwa nikimfuatilia kiongozi huyu na kugundua kuwa hapendi kutumia muda mrefu kuchuja taarifa anazoletewa kabla ya kuzitolea matamko au kuzichukulia msimamo. Hali hii imesababisha mara kadhaa (si nyingi) asikike akitoa taarifa za masuala ambayo yalikuja kuonekana kinyume au hayakuwa sahihi. Kwa mfano, katika kampeni za mwaka 2010 aliwahi kushutumu kuwa “…lori moja katika Wilaya ya Tunduma limekamatwa na masanduku ya kupiga kura”. Alipewa taarifa hizi na wasaidizi wake na kuzitangaza. Kwa bahati mbaya hazikuwa taarifa sahihi.
Pili, kuna wakati aliwahi kutangaza kwamba mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alikuwa ameonekana katika Hoteli ya Lakairo Jijini Mwanza akiwa anapanga mikakati ya kuiba kura na wana CCM wenzake. Ilikuja kuthibitika kuwa wakati, tarehe na muda alioungea, Kikwete hakuwa mkoani Mwanza
Na tatu, akiwa katika mkutano wa hadhara mjini Shinyanga, Dk Slaa aliwahi kutangaza kuwa aliyekuwa mkuu wa mkoa huo alikuwa amefariki dunia. Hali hiyo ilileta mshtuko kwa wananchi na wanafamilia, lakini baadaye ilithibitika kuwa mkuu huyo wa mkoa alikuwa hai. Taarifa hii Dk Slaa aliitangaza baada ya kuambiwa na msaidizi wake alipokuwa jukwaani.
Tabia ya Dk Slaa ya kuwaamini sana wasaidizi wake si jambo zuri na linaweza kuwa na madhara makubwa, ikiwa hataanza kujipa muda na kuchuja taarifa kabla ya kuzitoa ili kumuondoa kwenye dhana ya kujenga “masuala tata” au kutuhumiwa na wapinzani wake kisiasa, kwamba hasemi ukweli.
Lakini pia, tabia ya namna hii inaweza kumsababishia mara kadhaa afanye maamuzi yasiyo sahihi kwa sababu tu ya kuambiwa mambo yasiyo kweli na akaweka imani mbele kuliko utafiti na kujiridhisha kwanza. Sehemu ya udhaifu niliyoitaja hapa, imewahi pia kutajwa na Mhadhiri Maarufu wa Chuo Kikuu na kwa bahati mbaya yakawa yamegongana na mawazo yangu juu ya Dk Slaa.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Kisiasa na kwa wananchi, Dk Slaa ndiye mwana Chadema anayekubalika kuliko viongozi wote wa chama hicho. Naamini kuwa vikao vya kitaifa vya chama chake vitaitumia hii kama sababu muhimu ya kumpa fursa ya kugombea urais ili kuwasogezea wananchi chaguo muhimu.
Pili, Dk Slaa amegombea urais mwaka 2010 na kuibuka nafasi ya pili akipitwa na mgombea wa CCM tu. Kumpeleka kuchuana na wenzake ndani ya Ukawa huenda kukaifanya pia Ukawa izingatie suala hilo na kumuona kama mgombea muhimu kwa wakati wa sasa.
Nini kinaweza kumwangusha?
Kwa mtizamo wangu, ni jambo moja tu ndilo huenda linaweza kumfanya Dk Slaa asivuke vizingiti ndani ya Chadema, jambo hili ni ikiwa Chadema haitapewa fursa ya kuweka mgombea urais ndani ya Ukawa.
Tukumbuke kuwa ndani ya Ukawa kuna vyama vingine kama CUF, NCCR na NLD ambamo pia katika baadhi ya vyama hivyo kuna wagombea wenye sifa nzito na za kupigia mfano na huenda kushinda za Dk Slaa. Ikiwa Chadema haitapewa fursa ya kuweka mgombea urais kwa sababu ya kutoa nafasi hiyo kwa vyama vingine, ni dhahiri kuwa nafasi ya Dk Slaa kugombea urais mwaka huu itakuwa imefikia mwisho.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Mambo matatu yanaweza kuwa mezani kwa Dk Slaa ikiwa hatagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama chake:
Jambo la kwanza ni kuendelea kusimamia ukuaji wa Chadema. Dk Slaa amekuwa ndiye Katibu Mkuu wa chama hicho aliyepata mafanikio kuliko makatibu wakuu wengine waliowahi kusimamia chama. Ikiwa hagombei urais nadhani ataendelea na jukumu kubwa la kukijenga chama chake kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Jambo la pili linaloweza kuwa mezani ni kugombea ubunge. Dk Slaa alifanya kazi kubwa sana katika mabunge yaliyopita, hususani Bunge la 2005 – 2010. Itakuwa jambo la kusikitisha sana kama hagombei urais halafu hagombei pia ubunge. Haya yatakuwa matumizi mabaya ya rasilimali watu zilizoko kwenye vyama vya upinzani “misuse of human resources in opposition political parties”. Vyama vya upinzani vinapaswa kuachana na kasumba za zamani za kujijengea watu fulani kama “presidential materials” tu na kusahau kuwa watu hao wana jukumu kubwa la kusimamia serikali moja kwa moja kama hawagombei urais.
Na mwisho, namuona Dk Slaa kama Waziri Mkuu mahiri na thabiti kabisa kwenye serikali ya Ukawa, ikiwa vyama hivyo vitashinda uchaguzi wa mwaka huu na kuongoza serikali na ikiwa hatokuwa mgombea urais na au Rais Mteule, atakuwa na sifa za kipekee, uzoefu wa kutosha wa kibunge, masuala ya kitaifa na kimataifa na bila shaka anaweza kabisa kuongoza serikali imara kama Waziri Mkuu.
Hitimisho
Nilipokuwa nafanya utafiti juu ya Dk Slaa pia sikupata matatizo yoyote, ilikuwa ni kazi nyepesi sana kwa sababu nimemfahamu na kumfuatilia kwa kipindi kirefu kilichopita. Kiongozi huyu ana mambo mengi sana ya kuiga kutoka kwake, misimamo yake, utendaji kazi wake, uadilifu, weledi wa masuala ya kijamii na usimamizi.
Haya yote yanamvusha katika wasiwasi wa Watanzania kuwa huenda vyama vya upinzani havina viongozi thabiti wa kuongoza dola. Mimi nasema viongozi hao wapo na Dk Slaa ni mfano mojawapo. Kwa yote haya, namtakia kila la heri kiongozi huyu, kwamba safari yake kisiasa iwe na mafanikio mema kwa jamii na taifa letu.
Mwananchi

No comments: