Mkulima Elidephonce Bilohe ambae ni kada wa CCM
Dar/Mikoani. Kada wa CCM, Elidephonce Bilohe (43), mkulima anayeomba kupitishwa na chama chake kuwania urais, amesema anatumia usafiri wa mabasi ya umma kuzunguka mikoani kusaka wadhamini.
Wakati Bilohe akitumia usafiri huo, wagombea wenzake wanatumia au walitumia mabasi waliyokodi na kuyafanyia maboresho ndani, magari madogo na ndege kutafuta wadhamini 450 kutoka mikoa 15 inayotakiwa kwa mujibu wa taratibu za CCM.
Akizungumza na Mwananchi jana, Bilole alisema ameshafika mikoa tisa ambayo ni Dodoma, Kigoma, Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Morogoro na Dar es Salaam, tangu alipochukua fomu hiyo Juni 9.
“Huko kote nimekuwa nikienda kwa kutumia usafiri wa mabasi ya abiria na daladala. Kwa kweli nimepata ushirikiano mzuri kutoka kwa makatibu wa CCM, nawashukuru sana,” alisema.
Bilohe alisema atakwenda mikoa 15 tu kama inavyotakiwa na chama chake, tofauti na watiania wengine ambao baadhi wamekwenda zaidi ya mikoa 20.
“Kwenda mkoa mmoja natumia siku mbili ama tatu kufika na kupata wadhamini. Gharama ni nyingi sana, lakini kwa kuwa nimeshaamua kuwatumikia Watanzania nitakwenda,”alisema.
Alisema Watanzania wamekuwa wakimtia matumaini katika safari yake hiyo na kuwaomba wamuombee ili aweze kuifanikisha kwa mafanikio.
“Naomba Watanzania wenzangu mniombee katika safari hii. Nitawavusha kuwapeleka kwenye nchi ya ahadi,” alisema Bilohe aliyejiunga na chama hicho mwaka 2003.
Alisema kuwa atazirudisha fomu hizo Juni 30 au Julai Mosi kulingana na ratiba yake ya kukusanya wadhamini.
Jumla ya makada 39 wamejitokeza kuwania nafasi hiyo na Bilohe ndiye mgombea pekee aliye na elimu ndogo ya darasa la saba, tofauti na sheria ya nchi inayotaka mgombea wa nafasi hiyo ya juu kisiasa awe na shahada.
Bilohe ni mmoja wa makada wachache waliojitokeza kuomba ridhaa ya CCM ambao hawajawahi kushika madaraka makubwa serikalini au ya kisiasa.
Katika kinyang’anyiro hicho kuna mawaziri wakuu watatu, mawaziri 12 wa sasa, Jaji Mkuu mstaafu, maofisa wa juu wa Idara ya Usalama wa Taifa, maofisa waandamizi wa Serikali ambao wamestaafu na wabunge.
Membe asisitiza uadilifu
Mkoani Pwani, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe amesema kiongozi anayetaka kuwa rais mwaka huu ni lazima alingane kiuadilifu na viongozi wanne wa urais waliotangulia kuiongoza Tanzania kwani hao wote hawakujilimbikizia mali na wanachukia ubadhirifu, rushwa na ufisadi.
Membe alirejea kauli yake kuwa ana sifa zote za kumrithi Rais Jakaya Kikwete na hivyo ameitaka Kamati Kuu kutolikata jina lake ili Tanzania isonge mbele kiuchumi na kiutamaduni.
Membe alipata wadhamini 21,000 na kusema kuwa mkoa huo umevunja rekodi kwa kutoa idadi hiyo ikilinganishwa na mikoa 26 aliyokwishapita.
Waziri huyo alisema akipata urais tu, utakuwa mwisho wa mauaji ya watu wenye ulemevu wa ngozi na kwamba ataanza kumsaka muuaji wa kwanza wa albino na akimkamata tu utakuwa mwisho wa tabia hiyo kwa wengine.
Kadhalika, Membe alisema endapo CCM itampitisha na kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao na kushinda, jambo la kwanza ni kufufua viwanda na kujenga vipya ili kuweza kuzalisha ajira za kutosha.
Alisema atakuwa mkali katika kukataza viongozi kujihusisha katika ulaji rushwa huku akibainisha baadhi ya vipaumbele kuwa ni utawala bora na uchumi wa viwanda.
Akizungumza na wakazi wa Manispaa ya Morogoro mtaa wa Makongoro mjini hapa mara baada ya kukabidhiwa fomu za wadhamini 950, Membe alisema kuwa Kamati Kuu ya CCM haitakuwa imefanya makosa wala kujuta endapo itamteua kupeperusha bendera ya chama hicho, akiwa na lengo kuu kuzalisha ajira kwa vijana kwa kufufua viwanda vilivyokufa sambamba na kujenga vipya.
Lowassa avunja rekodi
Mkoani Arusha, Edward Lowasa ameendelea kuvunja rekodi ya idadi ya watu wanaojitokeza kumdhamnini baada ya kupata wadhamini 120,392 jana.
Rekodi hiyo ya Arusha imezipiku ile iliyowekwa na mkoa ya Iringa alikodhaminiwa na wanachama 58,562.
Mbunge huyo wa Monduli aliwasili jijini Arusha saa 9:00 alasiri na kupokelewa kwa mbwembwe zilizoambatana na nyimbo mbalimbali za wasanii kadhaa nchini. Lowassa aliongozana na mkewe Regina na viongozi kadhaa wa CCM.
Mara baada ya kuwasili uwanjani hapo, Lowassa alifanyiwa maombi rasmi na wazee wa kimila wa jamii ya Wamaasai, maarufu kama Malwaigwana.
Katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Arusha, Isaack Joseph alisema waliomdhamini waziri huyo mkuu wa zamani ni wanachama hai kutoka wilaya zote saba za kichama mkoani Arusha.
Kwa CCM, mkoa wa Arusha una wilaya za Arusha Mjini, Karatu, Longido, Monduli, Ngorongoro, Arumeru Mashariki na Arumeru Magharibi.
Marupu adhaminiwa na wanafunzi
Katika hatua nyingine, mgombea mwingine, Maliki Marupu amesema amelazimika kutumia mkoa maalumu wa vyuo vikuu kupata wadhamini ili kukwepa changamoto ya fedha za kuzunguka katika mikoa mbalimbali.
Marupu ambaye ni mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu Mzumbe alilieleza Mwananchi jana kuwa anatarajia kukamilisha idadi ya wadhamini 450 kwenye Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro.
Alipoulizwa kama haoni kuwa kwa kutumia mkoa huo wa vyuo vikuu pekee atakuwa amekosa sifa kwa kushindwa kutembelea mikoa mingine 14 zaidi inayotakiwa, Marupu alisema hata hao wanafunzi wanaunda mkoa wa vyuo vikuu kuna mikoa yanayotoka, hivyo haoni shida kumdhamini.
Marupu, mwenye umri wa miaka 34, alisema endapo angefuata mikoa ya kijiografia ingekuwa shida kwake kutokana na kukosa fedha.
Alisema katika mzunguko wake alipata changamoto za watu walioko katika ofisi za wilaya wakisubiri kudhamini wagombea kwa malipo ya Sh20,000 au 30,000, hivyo akaamua kuwakwepa na kudhaminiwa na wanafunzi wenzake.
Mwanafunzi huyo alisema licha ya kukamilisha idadi ya wadhamini, atakwenda nyumbani kwao Ukerewe kutafuta baraka za wazee kabla ya kuwasilisha fomu zake Dodoma.
Makada nane warejesha fomu
Jumla ya makada wanane wamerudisha fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais, huku Boniface Ndengo akisema amekumbana na tatizo la kuombwa fedha na wanachama kwa ajili ya wamdhamini.
Wengine waliorejesha fomu jana ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani.
Akizungumza mjini hapa mara baada ya kurejesha fomu hizo, Ndonge alisema katika mchakato wa kukusanya wadhamini amebaini wananchi wa kawaida nao ni zao la rushwa. “Unafika mahali wananchi wanakataa kukudhamini kwa sababu hauna pesa ya kuwapa. Mimi niliwaambia sina fedha ila ninataka kuwatumikia. Waliniambia mbona fulani katoa kiasi fulani wewe hutoi,”alisema.
Alilalamikia makada wenzie waliochukua fomu kuandikwa mara nyingi katika vyombo vya habari na wengine kutopewa nafasi.
Ndonge alisema alifanikiwa kupata wadhamini 602 katika mikoa 20 aliyoenda.
Katika hatua nyingine, Waziri Chikawe aliwaomba msamaha waandishi wa habari kuwa hataweza kuzungumza nao kutokana na kukimbilia majukumu mengine.
Kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho mwisho wa kuchukua fomu na kurudisha ni Julai 2 saa 10:00 jioni. Kazi hiyo ilianza Juni 3.
Wazee wa CCM bado
Kufanyika kwa kikao cha Baraza la Ushauri wa Wazee wa CCM kunasubiri uwepo wa wajumbe wake muhimu ambao kwa sasa wako safarini.
Kikao cha wazee hao ndio kitakuwa msingi wa uamuzi wa Kamati Kuu kuwapata wanachama watano ambao majina yao yatapelekwa kupigiwa kura na Halmshauri Kuu na Mkutano Mkuu wa CCM.
Kikao hicho cha Baraza la Usahauri linaloundwa na wenyeviti na makamu wenyeviti wastaafu wa CCM kipo chini ya uenyekiti wa Ali Hassan Mwinyi, ambaye aliongoza Serikali ya Awamu ya Pili, huku katibu wake akiwa Pius Msekwa.
Wengine wanaounda baraza hilo linalotambuliwa na katiba ya CCM ni Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour, Rais msataafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu, John Malecela na Amani Abeid Karume ambaye ni Rais mstaafu wa Zanzibar.
Katika mahojiano na gazeti hili jana kuhusu mkutano wao, Msekwa alisema: “Kikao hakijafanyika, wazee wapo safarini. Wengine wapo huko, wengine kule, mimi nipo Dodoma, nitarejea Dar es Salaam baada ya vikao vya Bunge kumalizika.”
Alipotakiwa kueleza kama kwa mazingira hayo kikao hicho kitafanyika lini, Msekwa alisema: “Kikao kitafanyika tu, kipo kwenye ratiba. Watu wenye busara husubiri ratiba ikamilike, iko ratiba nasi tunafuata ratiba.”
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment