ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 13, 2015

TAIFA STARS YAWASILI BORG EL ARAB, KUWAVAA MISRI KESHO

Msafara wa timu ya Taifa ya Tanzania (taifa Stars) inayodhaminiwa na kampuni ya bia ya Kilimanjaro Premium Lager tayari umewasili salama katika eneo la Borg El Arab jijini Alexandria na kufikia katika hoteli ya Panacea tayari kwa mchezo wake wa kesho.

Taifa Stars ambayo ilikuwa kambini nchini Ethiopia kwa takribani wiki moja, iliondoka jana usiku Addis Ababa  na kuwasili uwanja wa ndege wa Cairo majira ya saa 8 usiku, kisha kuunganisha kwa usafiri wa basi mpaka Borg El Arab takribani masaa matatu.



Kocha mkuu wa Taifa Stars Mart Nooij, atakiongoza kikosi chake katika mazoezi ya mwisho leo saa 1 usiku katika uwanja wa Borg El Arab kwa saa za Misri, sawa na saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.



Akiongelea mchezo wa kesho, Nooij amesema anashukuru kikosi kimefika salama nchini Misri na kipo katika hali nzuri, vijana wana ari na morali ya hali ya juu, anaamini kesho timu itfanya vizuri katika mchezo huo dhidi ya wenyeji Misri.




Nooij amesema mchezo wa kesho ni muhimu kwake, na kikosi chake kitacheza mpira wa kasi na pasi za haraka haraka, huku safu ya ushambuliaji ikihakikisha inatumia vizuri nafasi itakazozipata.



Aidha kuelekea katika mchezo huo wa kesho, kiungo Amri Kiemba ameungana na wachezaji wengine waliokuwa kambini Addis Ababa kuchukua nafasi ya Mrisho Ngasa ambaye alishindwa kuungana na timu kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wake.



Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia tayari amewasili jijini Alexandria kwa ajili ya kuipa sapoti Taifa Stars katika mchezo huo wa kesho.



Mchezo kati ya Misri na Tanzania utachezwa kesho saa 2 usiku kwa saa za Afrika Mashariki na kati katika uwanja wa jeshi la Misri (Borg El Arab) uliopo takribani kilometa 70 kutoka jijini Alexandria na kilometa 200 kutoka jiji la Cairo.



IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: