ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 11, 2015

UCHAGUZI WA BURUNDI WAAHIRISHWA TENA


Askari wakiimarisha ulinzi wakati wa uchaguzi wa wabunge nchini Burundi.
Taaswira za hali ya amani nchini Burundi.

Msemaji wa Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, Gervais Abayeho amesema kuwa, uchaguzi wa rais nchini humo uliopangwa kufanyika julai 15 umeahirishwa tena kwa mara nyingine na badala yake utafanyika Julai 21 mwaka huu.

Uchaguzi huo umekumbwa na utata baada ya makundi ya upinzani nchini humo kuandamana na kupinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu. Upinzani unadai kuwa rais Nkurunziza anakiuka katiba ya taifa na mapatano ya Arusha yaliyokomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa mujibu wa Msemaji wa rais, Gervais Abayeho uchaguzi huo umeahirishwa kufuatia shinikizo la viongozi wa kanda ya Afrika mashariki na Kati.

Viongozi hao wakiwemo Mwenyekiti na Mwenyeji wa Jumuiya, rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, na Yoweri Museveni wa Uganda, rais wa Kenya Uhuru Kenyatta walipendekeza uchaguzi uahirishwe kufuatia mgogoro wa kisiasa nchini Burundi.

Shinikizo hilo la kuahirisha uchaguzi lilitokana na Umoja wa Afrika, na Umoja wa Mataifa, jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki, pamoja na kikosi cha kimataifa kuhusu eneo la maziwa makuu.

Umoja wa Mataifa umesema kwamba, idadi kubwa ya watu waliokimbia walisema nchi hiyo inakumbwa na msukosuko mkubwa wa kisiasa.

Zaidi ya raia laki moja wa Burundi wamekimbia nchi hiyo tangu mwezi Aprili

Zaidi ya raia laki moja wa Burundi wamekimbia nchi hiyo tangu mwezi Aprili wakati kulizuka ghasia kupinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu

Hii ilikuwa ni mara ya tatu kwa uchaguzi huo kuahirishwa baada ya tume ya uchaguzi kuahirisha uchaguzi kwa majuma matatu kutokea Juni 26 hadi Julai 15 mwaka huu na sasa kusogezwa tena mbele hadi Julai 21 mwaka huu.

NA BBC

No comments: