ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 11, 2015

Wasanii kumfanyia ‘send-off’ JK


Ni tamasha maalum la kumpongeza, kuagana naye

Dar es Salaam. Shirikisho la Muziki Tanzania linaandaa tamasha maalum la kumuaga na kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kuinua tasnia ya muziki kwa kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake.
Rais wa shirikisho hilo, Ado Novemba alisema jana wakati akizungumzia hotuba ya Rais Kikwete juzi wakati wa kuvunja bunge mjini Dodoma kuwa tamasha hilo limepangwa kufanyika kabla ya Oktoba.
Kikwete alisema kwenye hotuba yake jinsi alivyowekeza akili, nguvu zake katika kukuza tasnia hiyo sanjari na michezo nchini.
Novemba alikubaliana na kauli ya Kikwete, akisema tasnia yao imepiga hatua kubwa kwa kipindi cha miaka kumi, hivyo kuwafanya vijana wengi wajiajiri kupitia muziki na pia kuutambulisha kama kazi inayoingiza kipato kwa mtu mmoja mmoja na pato la Taifa.
“Tumemwandalia tamasha la kumpongeza na kumuaga, tunajua anatupenda wasanii na ataendelea kutupatia mwongozo hata akiondoka, kuna vitu vingi kama wasanii tumepanga kuvifanya kwake, kwani mchango wake kwetu ni mkubwa na ameonyesha mfano hata kwa viongozi wanaokuja nini wanatakiwa kufanya ili kukuza vipaji vya Watanzania,” alisema Novemba na kuongeza: “Alipoingia madarakani, 2005 wasanii tulikuwa tunalipwa kiasi kidogo cha fedha, kwa sasa hali inaridhisha kwa baadhi yetu ijapokuwa kuna wengine bado malipo yao ni madogo. Lakini muziki wetu umetambulika na kukua kiasi cha kujulikana nje ya Afrika.”
Hata hivyo, alisema iwapo Kikwete ataondoka madarakani bila kusuluhisha suala la malipo ya mrabaha kwa wasanii, itakuwa vigumu kwao kufanikiwa miaka ijayo.
“Tunamwomba, kabla hajaondoka madarakani atufikirie namna atakavyoweza kukamilisha suala la mrabaha, redio na runinga waanze kutulipa stahiki zetu kwa kukamilisha hilo sanaa itaingiza pato.
Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifamba alisema hotuba ya Rais Kikwete juzi imefungua macho kwa Watanzania, wasanii na hata makampuni makubwa kuhakikisha yanageukia kuwekeza katika sanaa kuliko kuegemea kwenye soka.
“Nimefarijika kusikia Kkikwete akiitaja sanaa ya muziki na filamu kwamba ni kati ya vitu vilivyoitangaza nchi, hii imewafariji wengi, lakini tunapaswa kujifunza kitu, hasa kwa hayo makampuni makubwa ambayo siku zote yamekuwa yakiwekeza kwenye soka yageuke pia sanaa,” alisema Mwakifamba.
“Nchi kama Cameroon, Ghana, Afrika Kusini, soka liliwatangaza, lakini Tanzania imetangazwa na muziki pamoja na filamu. Lazima haya makampuni yaangalie namna nyingine ya kuwekeza fedha zao kwenye Sanaa zenye matokeo chanya na si soka ambalo kila siku linatuangusha,” aliongeza.
Mwakifamba alisema makampuni yanawaga mabilioni ya fedha kila kukicha, lakini bado soka limeshindwa kukua nchini.
“Si kama nawaponda, mimi naona ikiwa wataamua kuwekeza kwenye filamu au sanaa kwa kutafuta vifaa vya kisasa, maprodyuza wakubwa na hata kijiji cha kutengenezea filamu, tutafika mbali, vivyo hivyo wakiwekeza kwenye muziki tutavuna fedha nyingi za kigeni,” alisema.
CREDIT:MWANANCHI.

No comments: