ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 6, 2016

CHADEMA YACHAMBUA SIKU 120 ZA MAGUFULI

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezichambua siku 120 za Rais John Magufuli tangu ashike wadhifa huo kikidai kuwa uongozi wake umetawaliwa na ukiukwaji wa haki, demokrasia na utawala bora.
Aidha, Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana hivi karibuni imeitisha mkutano wa Baraza Kuu utakaofanyika Machi 13 jijini Mwanza ambao utatoa msimamo wa jinsi chama hicho kikuu cha upinzani kitakavyoidai haki badala ya kuiomba na kuweka mkakati wake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Kasoro zilizotajwa kushikia hatamu katika siku hizo zilizotimia jana ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendesha uchaguzi kwa upendeleo na haki kutotendeka Zanzibar baada ya kufutwa kwa uchaguzi, kuingiliwa kwa uchaguzi wa wenyeviti wa halmashauri na mameya, kuthibiti Bunge na uundwaji wa kamati na viongozi wake, polisi kuzuia mikutano ya hadhara na wabunge na madiwani wa Chadema kukamatwa kwa sababu zisizo za msingi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliitaka mamlaka husika kutangaza tarehe ya uchaguzi wa meya wa Jiji la Dar es Salaam, siku saba kabla ya kufanyika kwake.
“Hatutaomba tena kumpata meya wa Jiji la Dar es Salaam, tutadai kumpata. Serikali isifikiri wao ndiyo wanapanga tarehe. Mara nyingi wamekuwa wakitushtukiza ila kwa mujibu wa kanuni tarehe inapaswa kutangazwa siku saba kabla ya uchaguzi. Siku hiyo tutachagua meya na kama asipochaguliwa tusilaumiane,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, demokrasia imekuwa ikikua kwa kasi licha ya kuwa na changamoto kadhaa lakini miezi minne ya utawala wa Rais Magufuli, demokrasia hiyo inatoweka taratibu.
Kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, alisema wagombea walioshinda kihalali kwa kupigiwa kura na wananchi hawakupewa fursa ya kuongoza jambo ambalo linaweza kuathiri masuala ya kisiasa, kiuchumi na kiutawala ndani ya nchi.
Akizungumzia Bunge, Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema kumekuwa na udhibiti wa mhimili huo kutekeleza wajibu wake wa kikatiba, kisheria na kikanuni wa kuisimamia Serikali na jambo hilo limefanyika katika maeneo matatu; kuzuia urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja ya kupitia Televisheni ya Taifa (TBC), jambo alilodai kuwa limefanywa kibabe na Serikali ya CCM bila kujali kuwa “televisheni hiyo ni mali ya wananchi siyo chama tawala.
“Aidha, Serikali ya CCM imeingilia kwa kiwango kikubwa uundwaji wa uongozi wa kamati za Bunge zinazosimamia fedha za umma. Hapa kuna (Hesabu za Serikali) PAC na (Hesabu za Serikali za Mitaa) Laac,” alisema Mbowe.
Alisema kamati hizo zinapaswa kuongozwa na Kambi ya Upinzani Bungeni lakini CCM ilijiwekea utaratibu wa kuwapangia wapinzani viongozi wa kuongoza kamati hizo mbili.
“Tunastahili kuwa na mamlaka kamili ya kuchagua viongozi wa kamati hizi. Serikali pia imedhibiti uundwaji wa kamati za Bunge... Katika Bunge hili, Serikali na uongozi wa Bunge wametengeneza kamati bila kuthamini ujuzi, uzoefu na taaluma za wabunge. Hii itafanya Bunge kukosa meno,” alisema Mbowe.
Alidai kuwa polisi kwa maelekezo ya Serikali, imezuia mikutano ya siasa tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
Alisema mikutano inayoruhusiwa ni ya wabunge tu, si ya viongozi wala vyama vya siasa ambavyo vinahitaji kushukuru wananchi baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
“Leo ni miezi minne baada ya uchaguzi bado tunazuiwa kufanya mikutano. Licha ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kulitolea ufafanuzi suala hili bado tunazuiwa kufanya mikutano,” alisema Mbowe.
Alisai kuwa polisi imewafungulia mashtaka viongozi mbalimbali wa Chadema, wakiwamo wabunge na madiwani kwa kudai masuala ya msingi kuhusu haki zinazokiukwa.
Alisema mkutano wa Baraza Kuu utakaokuwa na wajumbe zaidi ya 600, wakiwamo wabunge na wenyeviti wote wa chama hicho utatoa msimamo na mwelekeo.
Akitolea mfano wa uchaguzi wa meya wa Jiji la Dar es Salaam alisema: “Kuongoza Dar es Salaam si mapenzi ya Mbowe ni wananchi. Woga kwetu ni mwiko na kauli ya amani bila haki haiwezekani. Tunaiambia Serikali na dola kwamba amani itapatikana tukiheshimiana na haki kuchukua mkondo wake kwa kufuata utawala wa sheria na Katiba.”
Alipoulizwa kuhusu madai ya Chadema, Waziri wa Habari, Nape Nnauye aliwataka viongozi wa chama hicho kutangaza hadharani kuwa wanamkubali Rais Magufuli kabla ya kuchambua siku 120 za utawala wake.
“Hawa Chadema walimkataa Magufuli, walisema hawamtambui na hata bungeni walimsusia, leo wanawezaje kuchambua kazi zake?” alihoji Nape.
Nape ambaye pia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, alisema Watanzania wanajua kazi nzuri ya Dk Magufuli na kuwataka Chadema wauchambue utawala wake baada ya kumkubali.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene alisema haoni kama kuna ukiukwaji wa haki za binadamu katika utumbuaji wa majipu kwani umelenga kusaidia wananchi wa hali ya chini.
“Hata hivyo, kama kuna anayeona ameonewa hajazuiwa kwenda mahakamani kupinga na kupata haki yake. Ni lazima Serikali ifanye kazi yake,” alisema.
Kuhusu umeya, Mwambene alisema CCM haina kosa katika hilo, bali inafuata kanuni na taratibu akisema Chadema inajua kilichotokea na inachofanya sasa ni kutafuta visingizio tu na wala si kingine.
“Mbona waliposhinda umeya Ubungo CCM hawakuenda mahakamani? Waache taratibu zifanye kazi,” alisema.

3 comments:

Anonymous said...

This is where the Oposition risks loosing its credibility. Magufuli has responded to most of the governance shortcomings that ordinary citizens were complaining against. The Oposition should give credit where it is due. It just goes to show how poorly they would have performed had they earned the trust of our people. Fortunately, Tanzanians know better. Thank God for Magufuli.

Anonymous said...

Huyu Mbowe na chadema yake ni jipu lilikwisha iva muda mrefu sana wananchi wanatakiwa kulitumbuwa mapema kutafuta chama m'badala cha upinzani. Upizani kuikosoa serikali sawa lakini sio huu ukosoaji wa chadema kwani wao sasa hawaikosoi serikali kwa manufaa ya watanzania na taifa isipokuwa ni dhahiri chadema wanapigania maslahi yao binafsi . Si kweli kwamba upizani sasa wanapigania maslahi ya taifa kwa sababu mtu anaeipigania maslahi ya Tanzania na watanzania kwa asilimia 200% tayari ameshapatikana na watanzania wameshamkubali na hawanashaka nae hata kidogo katika utendaji wake wanachotakiwa wao wapinzani ni kumuunga mkono katika jitihada zake za kuikomboa Tanzania kuondokana na janga la umasikini. Sasa kuendelea kwa upizani kushindwa kumuunga mkono muheshimiwa Maghufuli ambae katika utendaji wake wa kazi unaona kabisa yakwamba hayupo pale ikulu kuitumikia CCM bali yupo pale kuwatumikia watanzania ni ishara dhahiri yakwamba viongozi wa chadema na ukawa kwa sasa hawapiganii maslahi ya watanzania ispokuwa wanapigania maslahi ya Mbowe, Lisu, Lowasa,na wapambe wengine . Yaani unaona kabisa hawa watu wa upizani kitendo chao cha kutoitambua serikali ya Magufuli kama vile wanaishikiza serikali iwakatie kitukidogo ili wafanye hivyo inawezekana ilitokea huko nyuma katika serikali zilizopita lakini kwa serikali hii ya Magufuli ya awamu ya tano kitu hicho msahu. Wananchi wanatakiwa waachiwe wafanye shughuli zao za maendeleo na kuponya majaraha ya kisiasa yaliosababisha mgawanyiko wa mawazo na kiitikadi mda mfupi mara baada ya uchunguzi mkuu kwani kwa kiasi fulani wamekamilisha zoezi moja muhimu sana katika historia ya nchi yetu. Na Kwa upizani kutaka Kuwarejesha tena wananchi katika maandamano ya nchi nzima mara baada ya uchaguzi mkuu kwa kisingizio cha kuwapongeza kwa kuwachagua ni moja ya njia ya upizani wanaotaka kuitumia kuwashawishi wananchi kutoshiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi yao,yaani ni roho mbaya inayowasumbua ukawa na chadema yakwamba wamekosa kushika dola basi wananchi na watanzania nao wakose maendeleo. Kwani kama ni maandamano ya kuwashukuru wananchi kwa kuwachagua basi CCM wanahaki zaidi ya kufanya hivyo. Utaona yakwamba Mbowe na viongozi wenzake wa upizani hawana tofauti na wale viongozi wengine wa kiafrika walizozitumbukiza nchi zao katika umwagikaji wa damu kwa kukataa kushindwa uchaguzi Mungu bariki Tanzania tuna stable Government. Inafahamika waafrica sisi taabu sana kukubali kushindwa lazima tutatoa visingizio kuhalalisha tabia hiyo chafu na ujinga wetu wa kutokubali kushindwa. La kushangaza zaidi wakati wapizani wabara wakiishinikiza CCM Zanzibar kukubali matokeo ya uchaguzi Zanzibar, huku wao wenyewe wanashindwa kumtambua raisi halali wa serikali ya muungano aliechaguliwa na wananchi. Sasa utaona wapinzani wa kisiasa Tanzania hasa Tanzania bara wanalitumia suala la Zanzibar kisiasa zaidi yaani kwa kuwa hawana hoja ya msingi kuwaambia wananchi kule bara.

Anonymous said...

mimi ningekuwa mbowe badala ya kutumia mda mwingi kuiponda selikali ningetumia huo mda kuimarisha chama na kujikosoa pale tulipokosea,majungu awaachie waamba taarabu