Kwa hali ilivyo unaweza kusema ukahaba jijini Dar es Salaam umehalalishwa.
Hivi sasa wanawake wanaofanya biashara hiyo na wateja wao wamekuwa wakifanya ngono kwa malipo kweupe na katikati ya makazi ya watu bila kificho, huku ikionekana kuwa ni mfupa mgumu kwa Serikali kutokana na sheria kutotambua kama ni halali au la na bali wanaokamatwa hushtakiwa kwa uzururaji.
Timu ya waandishi wa gazeti hili, ilitembelea maeneo maarufu kwa biashara hiyo hasa baa na kushuhudia wanawake wanaojiuza na wateja wao wakifanya ngono katika vichochoro vya karibu, katika viti ndani ya baa hizo na kwenye magari.
Kadhalika, waandishi walibaini kuwa baadhi ya wanawake wanaojiuza wameolewa waume wao wanajua kuwa wake zao wanajiuza lakini wamewaruhusu ili kutafuta fedha.
Hali ilivyo Kinondoni, Temeke, Ilala
Katika biashara hiyo, makahaba hao wamebuni mbinu za kuhakikisha hawakosi wanunuzi ikiwamo kuweka mitego katika klabu ambazo hupiga nyimbo za zamani au za ‘watu wazima’ kama ambavyo wenyewe huziita.
Katika moja ya klabu hizo iliyopo Mikocheni, mwandishi wetu ameshuhudia makahaba tele wakisaka wateja kwa kila aina ya mbinu, baadhi wakiwa wamevaa vizuri lakini ‘kimitego’, wengine wakiwa wameketi na wakati mwingine kucheza muziki unaopigwa ‘live’ huku wakiwawinda wazee ambao hutoa dau kubwa kuliko vijana.
“Huwa ninakuja kudanga (kuweka mtego) hapa. Wengi ni wazee wenye fedha zao. Hapa ukiopoa wateja wawili kwa usiku mmoja aah, siyo mbaya inalipa, mzee ukimwambia akupe Sh50,000 anatoa,” alisema mmoja wa makahaba ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Mwingine ambaye pia hakutaka kutaja jina lake, huweka mitego yake katika klabu nyingine inayopiga muziki wa zamani katikati ya jiji, alisema: “Kujiuza si lazima usimame barabarani. Wengine wanakosea ‘timing’ kwa kutojua maeneo yanayolipa. Si kwamba mimi ninapenda muziki wa wazee lakini hapa biashara nzuri, ndiyo maana sikosekani kila wikiendi, yaani hapa pana uhakika wa maisha siyo huko kwa vijana ambako ukipata wa kukupa Sh20,000 shukuru.”
Tabata
Saa mbili usiku katika baa maarufu iliyopo eneo la Sanene, Segerea katika maegesho ya magari, makahaba wakiwa wamevalia nusu utupu walilisogelea gari pindi mmoja wa waandishi wetu alipokuwa akiegesha.
Raha ya makahaba hao ilidhihirika pale walipomulikwa taa za gari, kwani huwa wanaamini hapo ndipo mteja anapowaona vizuri. Hata hivyo, mwandishi wetu anaposhuka na mabinti hao kubaini kwamba pia ni mwanamke, walisonya na kutukana.
Akiwa hapo, alishuhudia katika moja ya ngazi za maghorofa, makahaba na wateja wao wakikamilisha biashara yao, chini ya usimamizi wa walinzi kwa ama ujira wa fedha au wakati mwingine ngono.
Katika baa nyingine maarufu iliyopo maeneo ya Tabata Bima, mapema ya saa mbili usiku, mwandishi mwingine alishuhudia wanaume na wanawake kila mmoja akiwa ‘bize’. Mwandishi alipofika, alitafuta eneo katika sehemu ya maegesho na kukaa ndani ya gari kwa muda ambako alishuhudia eneo hilo kugeuzwa ‘gesti’ kwani alishuhudia kahaba mmoja akikokotana na mteja wake hadi nyuma ya gari moja ambako ‘walimalizana.’
Mmoja wa makahaba hao (jina linahifadhiwa ambaye mwandishi anafahamu kuwa ameolewa), alisema mumewe anafahamu biashara hiyo na wamekubaliana. “...anajua (anamtaja jina) hana neno, natafuta maisha, yeye mwenyewe hana kazi,” alisema.
Msichana mwingine mdogo aliyekuwa akirandaranda katika maeneo hayo akiwa amevaa nguo za kuonyesha maungo alipoulizwa kwa nini anafanya vitendo hivyo kwa uwazi na katika maeneo ya makazi ya watu, alijibu; “biashara ni popote.
“Wewe vipi... mnatufuatilia sana mbona,” alisema baada ya kuona maswali yakiongezeka.
Wakazi walalamika
Wakazi wanaoishi jirani na baa maarufu zilizokithiri kwa kuwa na makahaba walisema mambo hayo ni kama yapo katika milango ya nyumba zao, huku wakihofia kuharibika kwa maadili ya watoto wao.
Mmoja wa wakazi wa Sokota, Wilaya ya Temeke, Mussa Mkotya alisema ingawa anapenda kusikiliza muziki wa zamani katika baa, sasa hivi ameacha kutokana na kukithiri kwa ukahaba.
“Napata wakati mgumu kuja eneo hili kutokana na kukithiri kwa makahaba, hata mke wangu akinisubiri hapa anaonekana kama anajiuza,” alisema Mkotya.
Mmoja wa wahudumu wa chakula katika baa moja maarufu Tabata, Faraji Hussein alisema anachukizwa na tabia za makahaba hao lakini hiyo ni biashara kubwa hapo.
“Wengi wanafika hapa kufuata huduma hii, wateja ni wengi hasa siku za mwisho wa wiki kwa kuwa makahaba pia wanakuwa wengi. Tunakerwa lakini utafanya nini na haohao ndiyo wateja, tunawahudumia hivyohivyo,” alisema Faraji.
Mkazi wa Tabata, Sanene, Mama Janeth alisema wasiwasi wake ni kwa mabinti wake wawili ambao wapo katika umri wa kupevuka.
“Kwa bahati mbaya mume wangu shughuli zake ni za kusafiri, hivyo watoto wanabaki na dada wa kazi na kaka yao mmoja, wasiwasi wangu ikiwa wanatoka usiku na kukutana na mambo hayo.”
Bodaboda wavuna
Madereva wa bodaboda katika maeneo mbalimbali walisema wanafaidika na biashara hiyo ya ukahaba kwa sababu wanapata wateja wengi, pia wanatumika kama walinzi wao.
Mmoja wao anayefanya shughuli zake Mbagala Sabasaba aliyejitambulisha kwa jina la Majanga alisema licha ya kumkera, vitendo hivyo vinamuongezea kipato kwa wateja wa ‘chapchap’ ambao wakati mwingine hawapeleki mbali.
“Wengi hutaka niwapeleke kwenye faragha kidogo, au gesti, nikimsubiri napata buku tatu, nikimuacha buku tatu (Sh3,000),” alisema na kuongeza:
“Kwa siku kuanzia saa mbili usiku naingiza kati ya Sh30,000 hadi Sh60,000 kukiwa na muziki, ”alisema Majanga.
Mwenzake wa Tabata Camp, Bashiri Kangili alisema mara kadhaa anapowarudisha nyumbani makahaba hao, humlipa ngono badala ya nauli.
Mfupa mgumu kwa Polisi
Alipoulizwa kuhusu kukithiri kwa ukahaba jijini, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema wamekuwa wakiwakamata lakini kesi zao haziwezi kuendelea kutokana na kukosa ushahidi wa kuwatia hatiani.
Alisema suala hilo huwa ni makubaliano ya watu wawili na hakuna sheria inayozuia watu kuwa wapenzi, hivyo kuwabana inakuwa shida kisheria.
“Wa kulaaniwa hapa ni wanaume, ambao wamekuwa wakinunua hii huduma, kama wao wataacha makahaba hawatakuwa na mtu wa kumuuzia, ” alisema Sirro.
Alitaka jamii kwa kushirikiana na mamlaka husika zitoe elimu ya kutosha kuhusu madhara ya vitendo hivyo badala ya kukaa kimya kusubiri polisi kuwakamata na kusababisha usumbufu kwa jamii.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Lucas Mkondya na alisema changamoto kubwa ni kupata ushahidi kama kweli watu hao wanajiuza.
“Kazi yetu si kukamata watu waliosimama barabarani au kwenye maegesho ya magari, kufanya hivyo tunakiuka haki za binadamu. Hatuwezi kufika na kuwakamata tu, iwapo tutawapandisha kizimbani tuna ushahidi gani kuhusu huyo mtu?” alihoji.
Alisema mfanyabiashara yeyote wa baa ana leseni, hivyo wanapopita katika lindo usiku wanachoangalia ni wahalifu na siyo raia wema.
“Huwezi kufika na kuanza kubughudhi wateja wake bila sababu, lakini kama anaruhusu biashara hiyo sina uhakika kwani hawa nao wana ushindani wa biashara, huenda wanachafuliana.”
Imeandikwa na Julieth Kulangwa, Harriet Makwetta, Kalunde Jamal na Florence Majani.
1 comment:
alivyo sema mtu hapo juu ukisoma hii habari yote ni kwamba wanaume walaumiwe wanaununua bidha hii na mimi nakubaliana naye.kwa nini wananunua bidha hii.maadili yapo wapi.majanga kweli katika nchi hii; na jipu hili kweli ni jipu donda ndugu haliwezi likapasuliwa litarudi tena.
fikiria mume anamruhusu mkewa kujiuza umme wake uko wapi yeye kuambiwa kicha cha familia kipo wapi.si bora angekuwa shoga tuu.mfyuuu.
Post a Comment