ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 6, 2016

RAIS WA VIETNAM KUFANYA ZIARA YA KWANZA YA KITAIFA NCHINI

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga (Mb.) (kulia), akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ziara ya kitaifa ya siku 4 ya Rais wa Vietnam nchini, Mhe.Truong Tan Seng kuanzia tarehe 08 hadi 11 Machi, 2016. Ziara hiyo itakuwa ni ziara ya kwanza ya kuja Tanzania pia Afrika. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga naye akisikiliza kwa makini mazungumzo ya Waziri na Waandishi wa Habari.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza kwa makini Balozi Mahiga (hayupo pichani). 
Bi. Mindi Kasiga naye akitolea ufafanuzi ratiba nzima ya ziara ya Rais huyo wa Vietnam.
Sehemu nyingine ya waandishi wa Habari wakinukuu baadhi ya pointi wakati mkutano ukiendelea. Picha na Reginald Philip 



Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Mhe. Truong Tan Sang atakuwa Rais wa kwanza kufanya ziara ya kitaifa nchini Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Rais Sang atawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere siku ya Jumanne tarehe 08 Machi 2016 saa mbili usiku na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ambapo mapokezi rasmi yatafanywa siku ya pili na mwenyeji wake, Rais Dkt. Magufuli katika Viwanja vya Ikulu.


Akiongea na Waandishi wa Habari Ofisini kwake leo, Waziri Mahiga alieleza kuwa Rais Sang atafutana na mke wake, Mama Mai Thi, Mawaziri watano na Wafanyabiashara 51 katika ziara hiyo. Dkt. Mahiga alieleza kuwa Serikali inaupa uzito wa pekee ugeni huo kwa sababu ni ziara ya kwanza ya kitaifa katika Awamu ya Tano kufanywa na Mkuu wa Nchi. “Wakuu wa Nchi kadhaa walishakuja hapa nchini lakini kwa ziara za kikazi, sio za kiserikali, hivyo Vietnam imetupa heshima kubwa sana”. Waziri Mahiga alisema.

Rais Sang ni mara ya kwanza kufanya ziara katika Bara la Afrika na Tanzania ambapo pia atazuru nchi ya Msumbiji baada ya kuondoka hapa nchini tarehe 11 Machi 2016.

Dkt. Mahiga aliwambia Waandishi wa Habari kuwa Tanzania ina mambo mengi ya kujifunza kutoka Vietnam namna ilivyopiga hatua kubwa ya maendeleo katika kipindi kifupi, licha ya kuendesha vita kubwa ya mapambano ya kupigania uhuru dhidi ya Ufaransa na baadaye dhidi ya Marekani. Alisema nchi hiyo imepiga hatua katika sekta za viwanda, kilimo, mawasiliano na uvuvi. Kwa upande wa kilimo, nchi hiyo ni ya kwanza kwa kuuza kahawa aina ya robusta na korosho duniani ingawa mbegu za mazao hayo zimechukuliwa Tanzania. 

Aidha, Vietnam ni maarufu duniani kwa kuuza samaki aina ya sato ambao walichukuliwa kutoka Ziwa Victoria.

Waziri wa Mambo ya Nje alieleza kuwa ili Tanzania nayo ifike ilipo Vietnam ni lazima ifuate mambo matatu ambayo Vietnam inayazingatia. Mambo hayo ni kufanya kazi kwa bidii katika mazingira ya aina zote, utekelezaji wa maamuzi wanayofanya na kuwekeza katika mafunzo ya ufundi, miundombinu kama ya umeme, barabara, reli, bandari na mabemki kwa ajili ya mitaji na huduma nyingine za kifedha.

Katika ziara hiyo, Rais wa Vietnam pamoja na mambo mengine atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake; Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein; Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai; Kuongea na wafanyabiashara na kutembelea eneo la uwekezaji la EPZA, Ubungo Jijini Dar es Salaam.

No comments: