Na Aron Msigwa - MAELEZO
Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
umekanusha tuhuma zilizotolewa na baadhi
ya wafanyakazi waendeshaji wa chuo hicho kwenye baadhi ya vyombo vya habari
kuwa unaendesha vitendo vya dhuluma, uonevu na upendeleleo katika ulipaji wa
mishahara na kuwasahau watumishi hao
jambo linalokwamisha ufanisi wa chuo hicho.
Taarifa ya kanusho dhidi ya tuhuma hizo iliyotolewa na
Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Utawala na
kusainiwa na Prof.Preksedis Marco Ndomba
leo jijini Dar es salaam imeeleza kuwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam
kinaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia Utumishi
Umma nchini na kamwe hakina mamlaka ya
kumwonea, kumdhulumu wala kutoa upendeleo kwa mtumishi yeyote kwa kuwa
suala hilo liko nje ya misingi iliyoanzisha chuo hicho.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kama ilivyo kwa vyuo vingine vya
umma suala la maslahi hasa nyongeza za mishahara na marupurupu mengine ya
watumishi wa vyuo hususan Chuo Kikuu cha Dar es salaam linapangwa na
kuidhinishwa na Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na siyo uongozi wa
chuo hicho.
Aidha, mishahara ya watumishi wa chuo hicho hupangwa
kulingana na kanuni na taratibu za Serikali na kuongeza kuwa wanataaluma wa
Chuo hicho hupewa mishahara yao kutokana na Muundo wa Pamoja wa Utumishi wa
Wanataaluma wa Vyuo Vikuu vya Umma wa mwaka 2014 na Sheria ya Kazi na mahusiano
kazini ya mwaka 2004 na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009.
Kuhusu tuhuma za kuwepo kwa tofauti ya mishahara miongoni
mwa watumishi wa Chuo hicho imeeleza kuwa hilo inatokana na tofauti ya vyeo
waliyonayo watumishi hao na kuongeza kuwa wao kama viongozi wa chuo hicho
hawana mamlaka ya kuwapangia mishahara watumishi wala kutengeneza nyaraka za
mishahara.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam
hupokea nyaraka za mishahara kwa watumishi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina na
kuzitekeleza na kuwataka watumishi hao kutambua kuwa tofauti ya vyeo waliyo
nayo inawafanya walipwe mishahara tofauti.
Kupitia taarifa hiyo uongozi wa chuo hicho umeeleza kuwa
hakuna upendeleo katika nafasi za
uongozi chuoni hapo kwa kuwa nafasi zote hujazwa kwa kufuata hati idhini ya
chuo, pia hupatikana kwa kushindanishwa
kwa waombaji kwa sifa zao na inapotokea mtumishi katika nafasi ya Mkurugenzi
uendeshaji anastaafu kazi Menejimenti ya
chuo humwomba mwanataaluma kutoka chuoni hapo kukaimu nafasi hiyo wakati
taratibu za kuitangaza nafasi hiyo ili kumpata mkurugenzi mpya zikiwa
zinaendelea.
Kwa upande wa tuhuma ya kuwepo kwa matumizi mabaya ya mali
za chuo hasa magari kwa safari zisizohusiana na chuo hicho imefafanua kuwa Chuo
Kikuu cha Dar es salaam kina Sera, Kanuni na miongozo mbalimbali inayodhibiti
matumizi ya magari na mali za umma ikiwemo ujazaji wa vitabu maalum vya
makabidhiano ya magari " Log Book".
Taarifa imebainisha kuwa UDSM hudhibiti matumizi ya magari
yake kwa
kuyawekea maandishi ubavuni na kwamba magari hutakiwa kuegesha chuoni baada ya matumizi
saa 12 jioni na wafanyakazi wanaoyatumia kinyume na miongozo iliyowekwa
wanachukuliwa hatua za kinidhamu.
Aidha, ili kuboresha maslahi ya watumishi wa chuo hicho
hasa upandishwaji wa vyeo ndani ya chuo muundo wa Utumishi wa wafanyakazi waendeshaji
hutumika pia maboresho hufanyika kupitia vikao rasmi vya ajira kulingana na
matakwa ya sheria ya kazi.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa Menejimenti ya chuo hicho
baada ya kubaini kuwepo kwa changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa
muundo wa Utumishi wa Waendeshaji iliamua kuuhuisha na kuuwasilisha kwa Msajili
wa Hazina ili ufanyiwe kazi.
Pia kikao cha Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es salaam
kilichofanyika Februari 12, 2016 pamoja na mambo mengine kilielekeza Chama cha
Wafanyakazi UDSM kwa kushirikiana na Uongozi wa chuo kuandika muhtasari
unaoaininisha changamoto za watumishi zilizopo ili ziwasilishwe katika Ofisi ya
Msajili wa Hazina.
No comments:
Post a Comment