Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akiwa na Wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa, wakati wa hafla fupi ya kumuaga Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Uingereza Sir Amyas Morse ambaye amemaliza muda wake wa uhudumu wa miaka sita katika Bodi hiyo. Hafla hiyo ilihusisha pia kukaribishwa kwa Bw. Kay Scheller Rais wa Ofisi Kuu ya Ukaguzi ya Ujerumani anayechukua nafasi ya Uingereza. Mabadilishano hayo yalikuwa ni sehemu ya Kikao cha 70 cha Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa ambayo ipo chini ya Uenyekiti wa Prof Mussa Assad, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kutoka Tanzania. Kutoka kushoto ni: Bw. Kay Scheller ( Ujerumani), Sir Amyas Morse ( Uingereza), Katibu Mkuu Ban Ki Moon ( UN), Prof Mussa J. Assad( Tanzania) na Bw. Shashi Kant Sharma ( India)
Mwenyekiti wa Bodi ya Ukazuzi ya Umoja wa Mataifa, Prof. Mussa Assad akizungumza wakati wa hafla ya kuiaga Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali ya Uingereza ambaye amemaliza ujumbe wake wa miaka sita katika Bodi. Mwenyekiti alitumia fursa hiyo kumshukuru Sir Amyas Morse kwa ushirikiano na weledi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Bodi.
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Prof. Mussa Assad akiongoza kikao cha 70 cha Bodi ya Ukaguzi ya Mashirika na Mifuko iliyochini ya Umoja wa Mataifa pamoja na shughuli nyingine zinazohusiana na Umoja wa Mataifa, Kikao hicho cha 70 kilifanyika siku ya Jumanne hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi kutoka kushoto , Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa n Hesabu za Serikali ya India, Bw. Shashi Kant Sharma, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Uingereza, Sir Amyas Morse, na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Tanzania, Prof. Mussa Juma Assad, wakitia saini zao katika ripoti 11 za ukaguzi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa zilizorejewa na kupitishwa na Bodi hiyo wakati wa mkutano wake wa sabini (70), uliofanyika siku ya jumanne hapa Makao Makuu ya Umoja huo, New York, Marekani. Ripoti hizo ni matokeo ya kazi kubwa ya Bodi hiyo.
Ujumbe wa Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ( CAG) muda mfupi kabla ya kuanza rasmi kwa kikao cha 70 cha Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa. Kutoka kushoto Bw. Isaya Jeremiah, Naibu Mkurugeni Ukaguzi wa Nje, Bw. Jerome Francis, Naibu Mkurugenzi Ukaguzi wa Nje, Bw. Salhina Mkumba, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Nje, na wa mwisho ni Bw. Athuman S. Mbuttuka, Naibu Mkaguzi Mkuu anayesimamia ukaguzi wa Hazina na Umoja wa Mataifa.
Na Mwandishi Maalum, New York
Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa, ambayo Mwenyekiti wake ni Mkaguzi na Mdhibiti n Mkuu wa Hesabu za Serikali, ( CAG) Profesa Mussa J. Assad jana ( Jumanne) imerejea na kuidhinisha ripoti kumi na moja za Mashirika, Mifuko na shughuli mbalimbali za Umoja wa Mataifa.
Katika kikao hicho cha 70 kilichofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, pamoja na kuidhinisha ripoti za Mashirika na Mifuko iliyochini chini ya Umoja wa Mataifa, pia Bodi ilipokea taarifa mbalimbali za kiutendaji zinazohusiana na majukumu ya Bodi hiyo.
Wajumbe wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa, ni Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu wa Serikali ya India, Bw. Shashi Kant Sharma, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Uingereza, Sir Amyas Morse, na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof. Mussa J. Assad.
Pamoja na kupitia na kuridhia ripoti hizo kumi na Moja, na kupokea taarifa za kiutendaji, shughuli nyingine iliyofanywa na Bodi ya Ukaguzi ilikuwa ni pamoja na kuiaga Ofisi ya Ukaguzi ya Uingereza baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka sita ya uhudumu katika Bodi hiyo.
Hafla ya kuagwa kwa Ofisi ya Ukaguzi ya Uingereza ilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Ban Ki Moon pamoja na wadau mbalimbali ambao ni wateja wa Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa.
Nafasi ya Ofisi ya Ukaguzi ya Uingereza imechukuliwa na Ofisi ya Ukaguzi ya Ujerumani ambayo imekaribishwa rasmi kuwa mjumbe wa Bodi hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo ya kuiaga ofisi ya Ukaguzi ya Uingereza na kuikaribisha Ofisi ya Ukaguzi ya Ujerumani, Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Mussa Assad amemshukuru Sir. Amyas Morse kwa mchango wake yeye binafsi na Ofisi yake kwa uwajibikaji mkubwa na weledi wa hali ya juu ambao umefanikisha utekelezaji wa mamlaka na majukumu ambayo Bodi hiyo imekabidhiwa na Umoja wa Mataifa.
Akiikaribisha Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Ujerumani, Prof. Assad ameelezea matumaini yake ya kufanya kazi kwa karibu na ushirikiano wa hali ya juu na mjumbe huyo ili kwa pamoja waweze kutekeleza majukumu na mamlaka waliyokabidhiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa, ilianzishwa mwaka 1946 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kukagua hesabu za Mashirika, Mifuko na Taasisi nyingine zilizo chini ya Umoja wa Mataifa, ili pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba Taasisi hizo zinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Umoja wa Mataifa ikiwa ni pamoja na matumizi yenye tija na adilifu ya bajeti kulingana na mamlaka ya Mashirika na Taasisi hizo.
Bodi ya Ukaguzi inatekeleza majukumu yake kama chombo huru na taarifa zote za ukaguzi huwasilishwa kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na wateja ambao wanakaguliwa na Bodi hiyo.
No comments:
Post a Comment