ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 30, 2016

PROFESA MBARAWA: SERIKALI HAIJAKURUPUKA KUNUNUA NDEGE ZA BOMBADIER Q400

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiendesha ndege kwa kutumia kifaa maalum cha kufundishia marubani (simulator) kwenye chumba cha mafunzo kwenye Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Mkuu wa chuo cha Taifa cha Usafirishaji Profesa Zacharia Mganilwa akizungumza na wadau wa sekta ya usafiri wa anga (hawapo pichani) katika uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani uliofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa wadau wa sekta ya usafiri wa anga (hawapo pichani) katika uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani uliofanyika jijini Dar es salaam.
Wadau wa sekta ya usafiri wa anga wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa katika uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani uliofanyika jijini Dar es salaam.

Na Abushehe Nondo na Sheila Simba-Maelezo
Serikali imesema kuwa iliamua kununua ndege mbili za abiria aina ya Bombadier Q400 kutoka nchini Canada kutokana na uhitaji wa huduma ya usafiri wa anga kwa safari za ndani ya nchi na mazingira halisi ya viwanja vya ndege vilivyopo nchini.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani katika chuo cha Taifa cha usafirishaji(NIT) 

Mbarawa alisema kuwa Serikali haikukurupuka katika kufanya maamuzi ya aina ya ndege za kununua badala yake imezingatia vigezo na malengo mahsusi ya kuhudumia usafiri wa ndani na kuboresha usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

“Serikali imeamua kununua aina hii ya ndege za Bombadier Q400 kutokana na hali halisi ya Viwanja vya ndege nchini kuwa vya Changarawe na lami kwa baadhi, huku lengo ni kutoa huduma za usafiri wa ndani” Alisema Profesa Mbarawa.

Mbarawa aliwataka Watanzania kuelewa nia ya Serikali yao ni kuhudumia wananchi hivyo watu wasipotoshe ukweli kuhusu ndege hizo kwani zimezingatia mambo mbalimbali ikiwemo suala la usalama na ufanisi katika uendeshaji wake.

Aliongeza kuwa ndege hizo zina uwezo wa kutua katika viwanja vingi hapa nchini kwani zinaweza kutua katika viwanja vyenye urefu wa kilomita 1.5 ambavyo ndio vingi nchini tofauti na aina nyingine ambazo hutua kwenye viwanja vyenye urefu zaidi ya kilomita mbili.

Prof. Mbarawa alibainisha sababu nyingine kuwa ni aliongeza uwezo mdogo wa ndege hizo katika kutumia mafuta ukilinganisha na aina zingine ambapo kwa safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza zitakuwa zikitumia Tani 1.7 za mafuta tofauti na aina nyingine zinazotumia hadi Tani 2.8 kwa safari moja.

Waziri Mbarawa pia alitumia fursa hiyo kukanusha uvumi ulionezwa kuwa ndege hizo zimenunuliwa katika kampuni ndogo isiyokuwa na sifa na kubainisha kuwa suala hilo siyo la kweli kwani kampuni hiyo imefanya biashara na nchini nyingi ikiwemo Ethiopia yenye ndege t19 aina ya Bombadier Q400 zilizotengezwa na  Kampuni hiyo.

Mpaka sasa tayari Serikali imeshafanya malipo ya ununuzi wa ndege hizo kwa asilimia 40 ambapo ndege hizo zinatarajiwa kuwasili nchi tarehe 19 septemba mwaka huu ambapo zitaanza safari ya kutoka nchini Canada tarehe 15 septemba mwaka huu kupitia nchini Uingereza.

Akizindua mafunzo hayo ya wakufunzi wa  marubani, Waziri Mbarawa aliwaasa Marubani ambao watahitimu mafunzo hayo  kuhakikisha wanazingatia suala na nidhamu na uadilifu katika sekta hiyo ya usafiri wa anga.

“Hatutaki kuwa na marubani ambao wana uwezo wa kazi lakini sio waadilifu,hakikisheni mnawafundisha marubani wanafunzi kuzingatia nidhamu na uadilifu katika sekta hiyo ya anga ambapo wakati mwingine Rubani anajijua anakasoro lakini bado anang’ang’ania kurusha ndege” alisema Prof.Mbarawa.

Aidha amesema kuwa Serikali itashirikiana na chuo hicho katika kutoa kozi za urubani ili kuakabiliana na changamoto ya ukosefu wa marubani nchini. 

No comments: