ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 30, 2016

TAMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU DHIDI YA MAUAJI YA ASKARI WA JESHI LA POLISI

Mtandao wa Watetezi wa Waki za Binadamu (THRDC) kwa niaba ya wanachama wake tunalani vikali maujai ya askari wa jeshi la polisi huku tukisisitiza kwamba askari wa jeshi la polisi wanaofanya kazi katika misingi na sheria ni watetezi wa haki za binadamu kama walivyo watetezi wengine. 

Kutokana na taarifa rasmi ya jeshi la polisi ni kwamba mnamo tarehe 23/08/2016 saa moja usiku maeneo ya Mbagala Mbande kata ya Mbande Temeke, majambazi ambao idadi yao haikuweza kufahamika wakiwa na silaha za moto walivamia benki ya CRDB tawi la Mbande ambapo waliwashambulia na kuwaua askari wanne wa Jeshi la Polisi waliokuwa kazini na kuwajeruhi raia wawili waliokuwa jirani na eneo hilo. 
 
Askari waliofariki katika tukio hilo ni E,5761 CPL Yahaya, F,4660 CPL Hatibu, G9524 PC Tito na G.9996 PC Gastone na raia waliojeruhiwa ni Ally Chiponda na Azizi Yahaya wote wakazi wa Mbande. 

Katika tukio hilo, majambazi hayo yalifanikiwa kupora silaha mbili za SMG na risasi sitini (60) na hakuna pesa au mali za benki iliyoibiwa, ni dhahiri kwamba walikuwa na kusudio la kujipatia silaha kwa ajili ya kufanya uhalifu na si vinginevyo kama baadhi walivyotaka kupotosha. 
Ikumbukwe kuwa majambazi mara kadhaa mwaka jana katika maeneo mbalimbali chini, mfano Kituo cha Stakishari Dar es Salaam na Kituo cha Polisi Ikwiriri , vilivyamiwa na majambazi kwa lengo la kuchukua silaha kwa ajili ya uhalifu.
 
Aidha, Tunalipongoza Jeshi la Polisi kwa kuweza kuwafikia majambazi hao huko Mkuranga bila kuumiza raia. Pia tunatoa pole kwa familia za askari wote watano waliopoteza maisha wakiwa kazini. 

Askari anaekamilsha idadi ya askari waliouwawa kufika watano ni Askari Thomas Njiku,Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Ujambazi alieuwa Vikindu wilayani Mkuranga wakati akiongoza kikosi maalum cha kuwasaka watu waliosadikiwa kuwa ni majambazi waliotekeleza tukio la kihalifu la Mbade,Mbagala.
 
Tunawasihi Watanzania kutoipokea dhana inayotaka kujengwa na wanasiasa kuwa hatukemei matukio haya dhidi ya polisi. 

Kumbukeni kuwa Mtandao wa Watetezi umekuwa ukitoa matamko mbali mbali kukemea mauaji ya askari wa jeshi la polisi, na tumekuwa mara kwa mara tukisisitiza kwamba askari wa jeshi la polisi ni watetezi wa haki za binadamu, kwa kuwa jukumu lao la kwanza ni kulinda mali za watu na usalama wa binadamu. 

Mtandao unatambua kuwa askari wa jeshi la polisi pia ni ndugu zetu, kaka zetu na baba zetu hivyo madhila wanayokumbana nayo ni yetu sote.
 
Mfano, katika repoti ya hali ya watetezi wa haki za binadamu kwa mwaka jana(2015) , Mtandao uliweza kuwa na kipengele maalumu kilichozungumzia haki za polisi na hali ya usalama kwa polisi wakiwa kama watetezi wa haki za binadamu.

 Katika ukarasa wa 18 wa repoti hiyo Mtandao uliweza kurekodi matukio ya uvamizi na mauaji ya jeshi la polisi zaidi ya kumi (10) na wengine watano (5) wakiachwa wamejeruhiwa. Kwa maana hii tukio lilitokea Mbagala ni muendelezo wa matukio ya kiuhalifu yanayoendelea nchini. 
 
Kumekuwa na changamoto kutoka kwa Jamii kuwatambua askari wa jeshi la polisi kama watetezi wa haki za binadamu, na hii ni kutokana na ukweli kwamba baadhi ya askari wamekuwa wakitumia vibaya madaraka yao kukandamiza haki za wananchi. 

Hali ilivyo sasa inaweza kuharibu dhana nzima ya polisi kuwa ni walinzi wa raia na mali zao, kwani vitendo wanavyofanya polisi dhidi ya raia hasa wafuasi wa vyama vya siasa na viongozi wao ni sababu kubwa ya kuharibu uhusiano mzuri kati ya polisi na raia.
 
Mtandao unatambua kwamba jeshi la polisi ni mamlaka muhimu sana katika kustawisha amani na ulinzi wa nchi kama litakuwa huru, bila kuingiliwa na wanasiasa na kuegemea upande wowote. 

Mtandao unapenda kuona kwamba Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa weledi na kwa mujibu wa sharia na katiba ya nchi. Aidha, Mtandao unaona pamoja na migongano mbali mbali ya kazi za polisi na za wanasiasa ( hasa nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya), ni vyema polisi wakaangalia misingi ya kimataifa ya haki za binadamu ili kuhakikisha usawa mbele ya jamii ili kurudisha mahusiano mazuri baina ya polisi na jamii wanayoitumikia.
 
Sambamba na hayo, Mtandao pia umesikikitishwa na kauli ya Mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam Mhe Paul Makonda aliyotoa tarehe 25 agosti 2016 wakati wa kuaga miili ya askari wanne waliouwawa huko Mbande Mkoani Dar es Salaam. Mtandao unakemea matamshi ya aina hiyo kutoka kwa kiongozi yoyote Yule, kwakuwa matamshi kama haya yanakwenda kinyume na misingi ya utawala bora na haki za binadamu na yanaweza kuwa sehemu ya kupoteza amani ya Taifa. Kitendo cha kukejeli haki za binadamu na kuamuru askari polisi wapige tu bila kujali taratibu za kisheria kinakwenda kinyume na misingi ya utawala bora.
 
Tunapenda viongozi wa serikali watambue kwamba kazi ya kulinda na kutetea haki za binadamu ni ya kikatiba na ndiyo maana kupitia Katiba yetu tuna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyoundwa kwa lengo la kuhakikisha viongozi wanaheshimu misingi ya utawala bora na haki za binadamu. Watetezi wa haki za binadamu wanatambulika kote duniani na wanalindwa kisheria mfano, kimataifa tuna Tamko la watetezi wa haki za binadamu la mwaka 1998. 
 
Madhara ya Uhusiano Mbaya kati ya Polisi na Raia
Ili Jeshi la Polisi liweze kufanya kazi yake vizuri ya kupambana na uhalifu hawana budi kuhakikisha wanakuwa karibu na wananchi. Madhara ya kutokuwa na mahusiano mazuri kati ya Jeshi la Polisi na raia ni makubwa. 
 
• Mojawapo ya madhara ni pamoja na kukua kwa makosa ya jinai na polisi kukosa taarifa za waalifu toka maoneo mbalimbali.
• Hali ya makosa ya jinai Tanzania imezidi kukua katika kiwango kikubwa. Kukua kwa makosa ya jinai ni zao la kutokuwa na mahisiano mazuri kati ya raia na polisi.
Wito wetu;
• Mtandao unatoa pole kwa Jeshi la Polisi pamoja na familia za askari hao na tunatoa wito kwa askari wengine wa jeshi la polisi kuendelea na kazi zao kwa weledi huku wakiboresha mahusiano mazuri na wananchi.
• Tunaishauri serikali kuliongezea nguvu Jeshi la polisi na kuboresh utalaamu katika kufanya kazi zao
• Tunawasihi askari wa Jeshi la wananchi kuheshimu mipaka ya kazi zao na kuheshimu haki za binadamu na katiba ya nchi katika kutekeleza kazi zao za kila siku
• Tunaishauri serkali kuwe na mabadiliko katika mfumo wa jeshi la polisi kuanzia kwenye mfumo wa kisheria ambao utatoa wajibu na uwajibikaji na kuheshimu haki za binadamu
• Tunaomba umma kutoa taarifa kwa jeshi la polisi na vyombo vya usalama hasa pale wanapohisi kuna tukio linalo ashiria uvunjaji wa amani na usalama.
• Tunaiomba serikali yetu kuipa kipaumbele jeshi la polisi katika kuboresha vitendea kazi vyao,nyumba za kuishi na mishahara bora ili kukidhi hali ya maisha ya sasa.
• Tunawaomba wadau wengine wa Haki za Binadamu pamoja na mashirika mengine ya maendeleo kukemea vikali tukio hilo. Tunashauri viongozi wa siasa waache kuingilia kazi za polisi ili kuepuka migogoro
 
PICHANI  JUU :Wakili wa THRDC akiwaonyesha waandishi wa habari(hawapo pichani) repoti ambayo ilitolewa na THRDC juu ya hali ya Watetezi wa Haki za Binadamu kwa mwaka jana(2015) ,ambayo ina kipengele maalumu kilichozungumzia haki za polisi na hali ya usalama kwa polisi wakiwa kama watetezi wa haki za binadamu katika ukarasa wa 18 wa repoti hiyo, http://thrdc.or.tz/download/situation-report-2015/

 
Imetolewa na Onesmo Olengurumwa
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
 
Imewasilishwa na Bennedict Ishabakaki
Wakili wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
 
30/08/2016

No comments: