ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 8, 2016

TUKUBALIANE KUTOKUBALIANA: Hakuna sababu ya kuendelea kucheka na nyani

Rais John Magufuli
WAHENGA wana msemo wao kwamba ukicheka na nyani, utavuna mabua.

Ni katika muktadha huo, bwana mmoja ambaye nimekuwa nikiona maandishi yake kwenye mitandao kwa jina la Malisa G. J, hivi karibuni aliandika maoni yake kuhusu hali ya uchumi kwa jinsi anavyoiona yeye, lakini akaacha pendekezo linalotaka ikiwezekana tuendelee kucheka na manyani hata kama tunavuna mabua! Kimsingi alikuwa anaangalia hatua anazochukua Rais John Magufuli za kubana matumizi, kupambana na ubadhirifu pamoja na ufisadi, na kuelezea faida zake na hasara zinazoweza kujitokeza kwa mtazamo wake.

Akamalizia hoja zake kwa kusema: “Sisemi Rais aendelee kubana matumizi au aache. Nachotaka kusema ni kuwa apime kati ya faida na hasara kisha afanye maamuzi kwa maslahi ya nchi...” Kwanza nianze kwa kuheshimu uchambuzi wake ambao kwa sehemu kubwa ni mzuri, lakini mgogoro wangu uko kwenye hitimisho lake.

Kwa kusema Rais apime faida na hasara ni kana kwamba mchambuzi huyo anaona kwa kuangalia anazoita hasara, basi Rais anaweza kuamua turudi kwenye matumizi holela ya rasilimali za umma, turudi kwenye kuachia ubadhirifu kujichimbia nchini mwetu na hata kuruhusu ufisadi uendelee kushamiri katika sekta ya umma!

Nilitarajia mchambuzi huyo ashauri pia namna ya kuondokana na hizo alizoona ni ‘hasara’ kutokana na hatua zinazochukuliwa na si kushauri kwamba Rais arudi kwenye mambo yanayoliangamiza taifa, mambo ambayo hayatuhakikishii kufika nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kama tulivyojipangia.

Katika uchambuzi wake, Malisa ameanza kueleza taarifa aliyosoma kwenye gazeti la Mtanzania la Julai 14, 2016 ikielezea kufungwa kwa hoteli kadhaa za kifahari kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa ni hatua ya serikali kuzuia mikutano kufanyika hotelini na badala yake ifanyike kwenye kumbi za serikali. Katika faida za kubana matumizi ambazo hata mimi baadhi nakubaliana naye, Malisa anasema mzunguko wa fedha utapungua na hivyo kusaidia sana kudhibiti mfumko wa bei.

Anasema sifa mojawapo ya fedha ni isiwe holela kwani ikiwa holela inasababisha mfumuko wa bei. Kwa hiyo anasema kwa hatua hiyo hata bei ya bidhaa na huduma zitashuka na kwamba ingawa hatua hiyo itawaumiza wafanyabiashara lakini itawasaidia walaji. Anafafanua kwamba mbali na kudhibiti uchumi, bidhaa na huduma zitapungua bei na kutoa mfano wa hoteli ambayo kama ulikua ukilala kwa Sh 100,000 kwa usiku mmoja, muda si mrefu utaweza kulala kwa Sh 40,000.

Kwamba mfuko wa saruji uliokuwa unanunua Sh 15,000 unaweza kushuka hadi Sh 8,000. Malisa anakiri kwamba hatua hizo za Rais zitaleta “nidhamu ya kazi” kwa kuwa mzunguko wa pesa utakuwa mdogo, hivyo itawalazimu watu kufanya kazi kwa bidii ili kupata pesa. Anakiri kwamba zama za kumuandikia mkuu wa idara muhtasari na kujifanya mlikuwa na kikao, halafu mkuu wa Idara anasaini mjilipe posho zimekwisha kwani sasa ni kazi tu.

Malisa ambaye pengine ni mwanauchumi kuliko mimi (sijui taaluma yake lakini mimi ni mwanahabari na mchambuzi) anakiri pia kwamba ubanaji wa matumizi katika sekta ya umma utasaidia kuimarisha sarafu yetu. Anasema moja ya mambo yaliyokuwa yakichangia kuporomoka kwa sarafu ni mfumuko wa bei lakini kwa pesa kupungua mitaani kutaimarisha thamani yake.

“Na pesa ikipotea maana yake itatafutwa. Na ikitafutwa basi uhitajikaji wake unaongezeka na uhitajikaji wa bidhaa ukiongezeka thamani yake pia inaongezeka,” anasema na kutabiri kwamba huenda kufika mwaka 2020 Dola moja ya Marekani inaweza kushuka hadi Sh 1,000 au hata chini ya hapo. Anataja faida nyingine kwamba kwa kuwa mzunguko wa pesa utakuwa mdogo, watu hawatafanya tena manunuzi ya kifahari nje ya nchi, kwa hiyo watanunua zaidi bidhaa za ndani na hivyo kusaidia kuimarisha sarafu yetu.

Faida nyingine anayotaja Malisa ni kuleta nidhamu ya matumizi kwa maana ya kwamba mtu hatotumia holela pesa kwani hajui kama kesho atapata tena. Anasema kwa hatua hii, Serikali ya Awamu ya Tano itapunguza pengo la kipato baina ya wenye nacho na wasiokua nacho kwani ‘madili’ ya kujilipa holela pesa za umma kama vile vikao na safari za kuzua yatakuwa sasa yamekoma.

Malisa anaamini, kama tunavyoamini wengi kwamba masikini wa Tanzania sasa wataanza kumiliki ardhi na bei ya ardhi na viwanja itaanza kuhimilika kwa watu wengi. Anasema hali ilivyokuwa ‘matajiri’ ndio waliokuwa wakisababisha ardhi kupanda kwa kuwa walikuwa wako tayari kununua kwa gharama yoyote. Kuhusu hasara za hatua hizo kwa mujibu wa Malisa ni pamoja na watu wengi kupoteza ajira kutokana na sekta nyingi za uzalishaji au za huduma yakiwemo mahoteli kufungwa.

Hasara nyingine anayoiona Malisa ni kwamba taasisi nyingi za fedha zitafilisika na kwamba tutegemee benki nyingi kufa na chache zitakazofanikiwa kuwepo zitapunguza wafanyakazi pamoja na kufunga baadhi ya matawi yake. Ni kwa mantiki hiyo Malisa anaona kana kwamba vitendo vya uhalifu vitaongezeka eti kwa sababu watu wengi watapoteza kazi, ‘dili’ zao za kifedha na wengine biashara zao zitayumba kutokana na wateja kupungukiwa na uwezo wa kifedha.

Hayo ndio yanayomfanya Malisa aone kama Rais anaweza kubadilisha kasi yake ya sasa na kurudi nyuma. Lakini asichokumbuka Malisa ni kwamba serikali iko katika mkakati mzito wa kufufua viwanda vilivyobinafsishwa na kujenga vingine. Hii maana yake ni kwamba ajira za uhakika zitaongezeka kwa Watanzania walio wengi hata kama kutakuwa na hali ya kuyumba yumba ni katika kipindi kifupi cha mpito. Anasema hasara nyingine ni baadhi ya benki kufilisika.

Hilo mbona ni jambo la kawaida na moja ya kanuni za biashara! La msingi ni kama benki zitakazobaki zitasaidia kunyanyua uchumi wa nchi yetu. Siamini kama shida yeti ni kuwa na benki lukuki isipokuwa benki zenye kukopesha kwa riba na masharti nafuu. Kubwa zaidi ambalo pengine ‘mchumi’ Malisa halioni ni kwamba hatua hii ya serikali itaifanya kupata mapato zaidi na kuyarudisha kwa wananchi kwa njia ya kuboresha huduma kama za barabara, kupeleka umeme hadi vijijini, huduma za afya, elimu na kadhalika.

Hizi huduma ndizo zitakazonyanyua na kuboresha maisha ya Watanzania. Uboreshaji wa huduma hizi, ndio namna ya kusaidia kusukuma uchumi, hususan katika kilimo kinachoajiri asilimia 70 ya Watanzania lakini kinachangia kiduchu tu katika pato la taifa. Hiki ni kilimo ambacho mbali na hitaji la pembejeo na huduma za maofisa ugani, lakini kinahitaji barabara nzuri, viwanda vya kusindika mazao (na hasa kama umeme utasambazwa zaidi) na masoko yanayofikika kwa urahisi.

Nimpe mfano huu Malisa. Kutoka Musoma mjini kwenda vijiji vya Bwai na Kurwaki, ni kama Dar na Kibaha au hadi Mlandizi (kwa wanaofahamu maeneo hayo), lakini kwa sababu ya ubovu wa barabara nauli ni Sh 3,000 au zaidi wakati ilipaswa kuwa wastani wa Sh 1,500. Mbali na nauli, pia inamchukua mtu muda mwingi kufika kulinganisha na anayetoka Dar kwenda Mlandizi, licha ya foleni atakazokutana nazo.

Endapo barabara hiyo itajengwa kwa lami kwa sababu serikali sasa itakuwa na uwezo huo, kwa mfano, bila shaka itakuwa ni chachu kubwa ya maendeleo ya wakazi wa vijiji hivyo. Watafikisha mazao yao ya kilimo, ufugaji na samaki kwenye soko lao kubwa la mji wa Musoma kwa haraka zaidi na nauli pungufu na hata wagonjwa wanaotakiwa kuwahishwa kwenye hospitali ya rufaa iliyoko mjini Musoma itakuwa ni rahisi na hivyo kuboresha zaidi afya zao na kuwahi kuendelea na kilimo.

Nchi kama Vietnam ambayo inasemekana miaka ya 1960 tulikaribiana katika uwezo wa kiuchumi zimefika zilipo sasa kwa sababu ya kutocheka na manyani na hivyo kusambaza zaidi huduma za kijamii. Vietnam ambayo inasemekana hata mbegu za korosho walitoa Tanzania miaka ya 70, kwa sasa wanatuzidi maradufu kwa kuzalisha korosho, sababu kubwa ikiwa ni kuimarisha viwanda vya ubanguaji, kiasi kwamba hata wakati mwingine korosho zetu ghafi zinakwenda kubanguliwa huko.

Mkulima wa korosho wa Vietnam, hata kama analima eneo dogo kuliko wa Tanzania, anazalisha kiwango kikubwa kutokana na kuboreka kwa huduma za ugani na anauza kwa bei kubwa kutokana na kusambaa kwa viwanda vya kubangulia.

Bila kupambana na manyani, Bwana Malisa, hatuwezi kufika huko daima. Manyani yametuachia mabua kwa kiasi cha kutosha na tumeyavumilia kiasi cha kutosha. Sasa lazima tusiyachekee. Changamoto (na siyo hasara kama anavyoita Malisa) zitakazotokea katika kipindi hiki cha mpito tutakabiliana nazo lakini Serikali ya Awamu ya Tano iko katika njia sahihi. Hakuna kutetereka na hivyo tuiunge mkono.

HABARI LEO

5 comments:

Anonymous said...

Asante sana mwandishi wetu kwa mawazo mapana pamoja na mchanganuo mkubwa wa Ndg Malisa. Yote yasemwayo yanawezekana. Tanzania haikuanza leo wala jana ina muda miaka 50 na marais awamu 4 tosha kabisa! hakuna sehemu iliyokuwa na uafadhali na labda niunge hapo hapo Manyani yametafuna ni mabua makavu yamebakia. Mabua haya yameenea sio ofisi za umma wa serikali! Tuna matatizo kuanzia kule tunakopata mazao Vijijini, kama unavyosema barabara ni nyingi mbovu ya kutisha, madaraja yanahitajika, vyama vya ushirika vimefilisika ni magofu ukiachilia mbali viwanda! Mwanakijiji ameuza mali zake na kushindwa kununua hata bati tano kuezekea nyumba kisa bei na umbali jinsi ya kubeba. Nyumba za nyasi ni asili zimeendelea kuota kila kukicha! Utashangaa hata ofisi ya mtendaji ni ya makuti kiashiria ni bendera ya kijani!

Pamoja na kutokucheka na nyani lakini basi jinsi ya kufika hapo tunapotaka ni mstati mrefu hadi kufikia kipindi cha miaka mitano aweza hata kujisikia vibaya mbona mambo hayaendi! Tutarajie miaka 25 kuanza na uafadhali. lazima tuwaelimishe watoto mashuleni kupata wataalamu wa viwanda> nasimama.

Anonymous said...

Mapinduzi matukufu. Nasema mapinduzi na sio mabadiliko, ndio yanayoendelea katika serikali ya Magufuli katika kuhakikisha Tanzania inaondokana na umasikini. Na hii ni kutokana na hulka yetu sisi kama watanzania tunahitaji kiongozi aina ya Maghufuli asikuwa na muhali na mtu na asiekuwa muoga hata kidogo kudiriki kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo licha ya wasi wasi na mashaka kutoka kwa baadhi ya watanzania wanojiita wasomi na baadhi ya wanasiasa ambao wanapinga na kubeza kwa chuki za kijinga wakijua fika Magufuli yupo kwenye right track. Tanzania tuna wasomi wengi lakini niseme wazi hawana tofauti na mtanzania asiesoma au bora huyo mtanzania asiesoma kwa sababu ni taabu sana kumsikia mtanzania asiesoma kaisabishia serikali upotevu wa mabilioni ya shillingi. Watanzania wengi tunavipaji iwe kwenye michezo,Elimu,sanaa nakadhalika lakini ni waoga mno wa kujaribu. Na ni moja ya sababu iliyopekekea watanzania wengi kuwa masikini na kuidumaza hata nchi yetu kimaendeleo. Na ndio maana tunasema Maghufuli ni mtanzania tofauti kabisa na kama atapata ushirikiano na ushauri wa maana basi Tanzania itakuwa ni nchi ya mfano Africa kimaendeleo katika kipindi kifupi sana kijacho. Hao wanaopiga kelele aah sijui Magufuli dikteta kwa kweli wanatia kichefu chefu. Vipi Magufuli awe dikteta na ni raisi mwenye term limit (kikomo cha kuongoza?). Kama kweli Maghufuli ni dikteta basi atakapomaliza muda wake wa miaka mitano wapinzani wanatakiwa kwenda kumshitaki kwa wananchi kuwa hafai ni dikteta na wawaache wananchi waamue. Lakini sio wapinzani kujijengea kesi majaji wawe ndio wao yakwamba wamesema magufuli ni dikteta basi wanataka watanzania wengine kuwaaminisha huo upuuzi wao na kujaribu kuwashawishi kuingia mitaani kufanya fujo kwa tuhumu za uongo na kipumbavu kabisa. Maghufuli si dikteta wala hatokuwa dikteta kwa kuitwa na akina Mbowe kama watanzania anaowatumikia wanaridhiswa na mziki wake wa kazi. Hata marekani wakati wanatapa tapa na hali ngumu ya maisha katika miaka ya 1920 hadi 1933 wakati alipoingia madarakani kwa kiasi kikubwa anaweza kuitwa ndio chimbuko la maisha bora ya mmarekani bwana Fredrick Delano Roosevelt (FDR) licha ya sifa kubwa ya kuiletea marekani maendeleo lakini tunaambiwa yakwamba watu weusi na wanawake katika utawala wake hawakuruhusiwa kupiga kura. Na alikuwa na amri nyingi au nguvu zake za kiraisi (Executive Orders) kuliko maamuzi ya bunge na ni kiongozi aliekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi marekani, lakini makubwa kuliko yote huyu ndie kiongozi wa marekani anaekumbukwa zaidi katika kuwatoa wamerekani kutoka katika hahi duni wakati wakiwa taabani kutokana na mtikisiko wa kiuchumi wakati huo(Great Economic Depression) na kuwajengea misingi ya kiuchumi ililoliletea heshima marekani kutokana na ujasiri na mikakati yake na nafikiri ukimwita huyu kiongozi mbele ya wamarekani kuwa ni dikteta wanaweza hata kukusweka ndani licha ya uvumilivu wao wa kusikiliza hoja ya upande wa pili kisiasa. Kwa hivyo wanaomwita Maghufuli dikteta kwa kipi? Kama si upumbavu.

Unknown said...

apongezwe sana rais magufuli kwa umahiri wake wa kuwajali watanzania walio wengi hasa masikini

Anonymous said...

Long live Magufuli. God bless you. Daring, bold, transparent and accountable leadership. This is what we missed for a long time.

Anonymous said...

Hatulihitaji Bunge. Limefanya nini miaka yote iliyopita kama sio ulaji sambamba na ule wa Serikali. Walikuwa partners in crime. Walaji tu wote.