Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu aliyesimama akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi wa Mradi wa kuijengea jamii uwezo katika kuibua na kutekeleza mpango shirikishi
Madiwani, na Wakuu wa Idara na Vitengo wakisikiliza kwa makini maelezo kuhusu walengwa wa Mradi wa kuijengea jamii uwezo katika kuibua na kutekeleza mpango shirikishi
Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Juma Mwanga, na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Bi Rustika Turuka
Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akisikiliza kwa makini maelezo kuhusu mradi huo
Madiwani,Wakuu wa Idara na Vitengo wakisikiliza kwa makini maelezo ya Mradi wa kuijengea jamii uwezo katika kuibua na kutekeleza mpango shirikishi
Shirika la Health Actions Promotion Association (HAPA) la Mkoani Singida kwa ushirikiano na Shirika la The Foundation For Civil Society la Jijini Dar es salaam linatarajia kuendesha mradi wa miaka mitatu kwa vijiji vyote vya Wilaya ya Ikungi kwa lengo la kuijengea jamii uwezo na mbinu shirikishi kama fursa na vikwazo katika maendeleo.
Mradi huo utaanza na Vijiji 10 vya majaribio (Pilot Villages) kutoka katika kata nne na kila kata itakuwa na Vijiji ama viwili ama Vitatu ambapo uchaguzi wa Vijiji hivyo vya majaribio umezuingatia utayari wa jamii husika katika shughuli za maendeleo pamoja na gharama za uendeshaji wa mradi ili kupata matokeo chanya kwa uendelezaji wa mradi husika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa Uongozi wa Wilaya hiyo unaendelea kushirikisha wadau mbalimbali katika kusaidia kutekeleza shughuli za maendeleo, kwani kwa uhabarisho wa mafunzo ya kujenga uwezo wa jamii na Halmashauri yataendelea katika kuimarisha juhudi za Wilaya zinazoendelea kuchukuliwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo pia itakuwa ni fursa kwa jamii kuwa na Uwezo na Nyenzo muhimu katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ufanisi.
Amesema kuwa Wilaya ya Ikungi inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kujiletea maendeleo ambapo endapo zitapatiwa upembuzi yakinifu zitapunguza kadhia zinazowakumba wananchi ambapo amezitaja changamoto hizo ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa Vituo vya Afya na Zahanati (Kata na Vijiji) ambapo kwa sasa Wilaya ina vituo 39 tu vya kutolea huduma za Afya ambapo upungufu ni Asilimia 60, Ujenzi na Uboreshaji wa miundombinu ya shule za msingi ambapo kuna nyumba za walimu 387 ambapo upungufu ni nyumba 854, Ujenzi na Uboreshaji wa majosho na mifugo kwani kwa sasa yapo majosho 30 huku kati ya hayo majosho 20 ni mabovu.
Dc Mtaturu alisema kuwa Zipo Asasi mbalimbali ambazo zimesajiliwa kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi lakini zimegeuka na kuwa Asasi zinazofanya kazi za kisiasa tofauti na usajili wao ambapo amesema serikali haitasita kuzichukulia hatua ikiwemo kuzifuta Asasi hizo ili ziache kupotosha wananchi.
Dc Mtaturu alisema kuwa Mradi huo unaotolewa na Shirika la HAPA ni lazima uzingatie matakwa ya kutoa elimu kwa wananchi ili wafahamu kuwa wana nafasi kubwa ya kufanikisha maendeleo yao katika jamii hivyo waache kupotoshwa na baadhi ya wanasiasa kuwa maendeleo yataletwa na serikali pekee.
Msimamizi wa Mradi wa HAPA Noel Makyao amewataja walengwa wa Mradi huo kuwa ni wananchi wote wa kijiji cha Mradi wa majaribio, Wawakilishi 100 kutoka kila kijiji ambao watachaguliwa ili kuendesha zoezi la kutengeneza bajeti ya mpango wa kila mradi ulioibuliwa na jamii kwa siku tatu mfululizo na watu mashuhuri, wakuu wa madhehebu ya dini na makundi mengine wapatao 20.
Alisema kuwa Jumla ya gharama zote za kutekeleza mradi wa mbinu shirikishi ya kujenga uwezo wa jamii katika kuibua, Kupanga, Kutekeleza na kupima matokeo ya Mradi katika vijiji kumi vya majaribio kwa robo mbili zitakuwa shilingi milioni hamsini (50,000,000/=).
Makyao alisema katika awamu hii ya vijiji kumi vya majaribio jumla ya watu wapatao 25,511 watafikiwa kati ya lengo la watu 25,334 zaidi ya watu 177 ya walengwa wa mradi.
No comments:
Post a Comment