ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, November 3, 2016

Wazee wamkomalia ofisa wa TRA



File Photo
By Shija Felician, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Kahama. Sakata la wizi wa Sh50 milioni nyumbani kwa ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kodi wa Kahama limechukua sura mpya baada ya Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru) kualikwa kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

Umoja wa Wazee Kahama (Uwaka), umepinga uamuzi wa kumhamisha kituo cha kazi ofisa huyo badala yake umetaka Takukuru kuchunguza tukio hilo na kuchukua hatua za kisheria iwapo kosa la jinai litabainika kutendeka.

Katibu wa Uwaka, Paul Ntelya akizungumzia tukio hilo alisema: “Siyo jambo la kawaida mtumishi wa Serikali kuhifadhi kiasi kikubwa cha fedha kama hicho chumbani kwake. Lazima achunguzwe alizipata wapi na kwa nini alizihifadhi ndani badala ya benki.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Murilo Jumanne wiki iliyopita alithibitisha ofisa huyo aliyetambuliwa kuwa ni Kefakeika Agwanda kuibiwa fedha hizo na mtu anayedaiwa kuwa mkewe. Jumanne alisema mtuhumiwa alitiwa mbaroni jijini Mwanza akiwa na fedha taslimu Sh47 milioni.
MWANANCHI

No comments: