Na Afisa habari Mufindi.
Jumla ya shilingi milioni 150 zimetolewa kwa sharti la mikopo kwa vikundi vya wanawake na Vijana wa halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, ikiwa ni asilimia 10 ya Fedha iliyokusanywa na halmashauri hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu tangu kuanza kwa mwaka wa fedha 2016 – 2017 mapema mwezi Julai mwaka huu.
Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Dkt. Riziki Shemdoe amesema jumla ya vikundi vilivyokopeshwa fedha hizo ni 89 ambapo vikundi 42 ni vya vijana vikiwa na jumla ya shilingi milioni 75 wakati vikundi 58 ni vya wanawake navyo vimewezeshwa kiasi kama hicho.
Akibainisha vigezo sita vilivyozingatiwa wakati wa utoaji wa mikopo hiyo, kuwa ni pamoja na uhai wa kikundi kinachoomba mkopo, uwepo wa katiba kwa kikundi husika, hati ya utambulisho ya kikundi, kiwango cha Fedha kinachoombwa kisizidi milioni 03, takwimu nzuri ya urejeshaji mikopo kwa vikundi vivyokopa siku za nyuma huku waombaji wote wakitakiwa kupitisha maombi katika ngazi za vijiji na kata.
Dkt. Shemdoe ameongeza kuwa kabla ya kukabidhi hudi kwa vikundi hivyo, Ofisi yake itataoa mafunzo maalum kwa vikundi vyote ili kuvijengea uwezo wa kuendesha shughuli za kijasiriamali katika vikundi ili viweze kufanya shughuli hizo kwa mafanikio na kupata faida pamoja na kufanya marejesho kwa wakati ili fedha hizo na nyingine zitakazo endelea kutengwa zitumike kuvikopesha vikundi vingine katika robo inayofuata.
Mkurugenzi huyo amevitaka vikundi hivyo kuzingatia kuwa pesa hizo si za mgao bali ni mkopo na wanapashwa kuzifanyia biashara kadri ya maandiko yaliyowasilishwa katika Ofisi yake na endapo kikundi chochote kitaenda kinyume na masharti yaliyokubalika, Ofisi yake haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika.
Aidha, Dkt. Shemdoe, ameahidi kuendelea kutenga asilimia 10 ya Fedha zitakazo endelea kukusanywa na halmashauri yake kwa ajili ya wanawake na vijana kwa kila robo huku akitoa rai kwa vikundi vingi zaidi kuendelea kuundwa na kukidhi sifa stahiki ili viweze kukoposhwa katika awamu zinazofuata.
No comments:
Post a Comment