ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 6, 2016

‘Sheria ya Huduma za Habari imeinyemelea Haki ya Uhuru wa Mawazo ya wananchi’

Twaweza ni taasisi ya kiraia inayoshughulikia maswala ya elimu pamoja na utawala bora.

Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari una umuhimu wa kipekee katika swala la msingi la haki ya uhuru wa mawazo kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 18 (a) - na 18(b) ya Katiba:

18.-(1) Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.
(2) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.

Jana jioni, tulipata fursa ya kushuhudia mjadala mzito Bungeni kuhusu Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari.

Baada ya mjadala huo, tulipata orodha ya marekebisho (Schedule of Amendments) ya muswada huo. Idadi ya marekebisho ni 28, yakijumuisha pia vifungu vipya vinne.

Kati ya hivyo vifungu vipya, viwili vimegusa kwa kiasi fulani, mambo ya msingi ya haki ya uhuru wa mawazo:
  • Kifungu kipya cha 10 kimeruhusu uwezekano wa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mkurugenzi wa Habari kwa Waziri wake na kwa Mahakama Kuu
  • Kifungu kipya cha 27 kimeainisha utaratibu wa Kamati ya Malalamiko ya Baraza Huru la Habari, kuyapokea na kuyashughulikia malalamiko ya waathirika wa utangazaji na huduma za habari.
 Vifungu viwili vimegusia maswala ya kiutendaji au kiutawala zaidi:

  • Kifungu kipya cha 31 kimeainishi mamlaka ya Baraza Huru la Kabari kuunda Sektreatriat yake
  • Kifungu kipya cha 60 kinawalinda wachapishaji dhidi ya kosa la kuchapisha maudhui ya kichochezi au uasi ikiwa hawakuwa na taarifa za maudhui hayo.
Tunasikitika kuona kwamba mambo kadhaa ya msingi hayakurekebeishwa ili kuilinda ipasavyo Haki ya Uhuru wa Mawazo. Baadhi ya mambo haya ni kama ifuatavyo:
1. Bodi ya Ithibati ya Wanahabari imebaki. Tulipendekeza kifungu chote kifutwe. Lakini katika mjadala Bungeni jana yalitolewa mapendekezo mawili ambayo, kama yalipokelewa, yangeweza  kupunguza makali ya kifungu hiki:
  • Bodi iwe Bodi ya Ithibati ya Wahariri (na siyo ya Wanahabari kwa ujumla wao)
  • Muundo wa Bodi ya Ithibati - Baraza huru la Habari liweze kuwachagua wajumbe angalau wawili wa Bodi bila pingamizi la Waziri
2. Kisha – Bado ni kosa kutangaza mambo yenye kashfa, hata kama mambo yenyewe ni ya kweli. Kosa linafutwa pale tu matangazo hayo yana manufaa kwa umma.

3. Tafsiri ya makosa mbalimbali, haswa katika kifungu cha 47 na kifungu cha 49 inabaki kuwa pana mno na kuathiri uhuru wa mwananchi kutangaza maoni yake. Ni kosa kwa mfano, ‘kuchochea manung’uniko na kutoridhishwa miongoni mwa wakazi au kwa wakazi wote wa Jamhuri ya Muungano.’ (kifungu 49(1)(d)).

Kwa ujumla, marekebisho machache ya Sheria ya Huduma za Habari yamepunguza makali ya mbano wa Haki ya Uhuru wa Mawazo. Lakini, kwa mtazamo wetu, haki hii ya msingi ya Watanzania wote, imenyemelewa na sheria hii mpya.

Imetolewa na Twaweza
5 Novemba, 2016 Dodoma Tanzania
---- Ends ----
For more information:
Risha Chande, Senior Communications Advisor, Twaweza
e: rchande@twaweza.org | t: (+255) (0) 656 657 559     

Notes to Editors

  1. Hotuba ya Kamati ya Bunge kuhusu Muswada wa Habari: http://tanzania-24.blogspot.com/2016/11/hotuba-ya-kamati-ya-bunge-kuhusu.html?m=1
  2. Twaweza inafanya kazi ya kupima uwezo wa watoto kujifunza, wananchi kuwa na utayari wa kuleta mabadiliko na serikali kuwa wazi na sikivu zaidi katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Twaweza ina programu, wafanyakazi na ofisi katika nchi zote tatu, na utaratibu unaoheshimika kimataifa wa kujifunza, ufuatiliaji na tathmini. Programu zetu muhimu ni pamoja na Uwezo, ambayo ni tathmini kubwa ya kila mwaka ya wananchi barani Afrika inayopima viwango vya watoto vya kujifunza kwenye maelfu ya kaya, na Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu ya mkononi. Pia tunashiriki kwenye masuala ya umma na sera, kupitia ubia wetu na vyombo vya habari, juhudi za kimataifa zinazoshughulikia masuala ya uongozi kama vile mpango wa Ushirikiano na Serikali wazi (OGP).
  3. Tovuti: www.twaweza.org Facebook: Twaweza Tanzania Twita: @Twaweza_NiSisi

No comments: