ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 9, 2017

Vigogo wa upinzani watema cheche Z’bar

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa akisalimiana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad baada ya mkutano wa uzinduzi wa kampeni za Jimbo la Dimani uliofanyika Fuoni, Unguja Zanzibar jana. Picha na Habari Mseto Blog

By Haji Mtumwa, Mwananchi hmtumwa@mwananchi.co.tz


Zanzibar. Vigogo wawili wa siasa za upinzani nchini, Edward Lowassa na Maalim Seif Sharif Hamad jana walitumia fursa ya kumnadi mgombea ubunge Jimbo la Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhan kulalamikia utawala uliopo madarakani kuwa unaendesha mambo kibabe.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani na Maalim Seif aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Serikali iliyopita, waligombea urais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar, mtawalia.

Maalim Seif alia na JK

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni za mgombea huyo kwenye Skuli ya Fuoni, Zanzibar, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu CUF, alisema chanzo cha mgogoro wa Zanzibar kuhusu Uchaguzi Mkuu uliopita ni Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Alidai kwamba Kikwete ndiye aliyefifisha matakwa ya Wazanzibari walio wengi ya yeye kuwa Rais wao.

Alisema kazi kubwa ilikuwa imekamilika ya kuhakikisha Wazanzibari wanakuwa na Rais wamtakaye.

Maalim alisema hata wafanye kitu gani, mwaka huu msumari umewaganda na kuahidi kuwa hivi karibu Wazanzibari watafurahia mambo yao mazuri.

Alisema mipango imara ya kuhakikisha kuwa mambo hayo yanakaa sawa inakwenda vizuri na kuahidi kuwa wakati wowote matunda hayo yataonekana.

Lowassa ashangaa hali ngumu

Akihutubia mkutano huo, Lowasa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alieleza kushangazwa kwake na hali ya kiuchumi baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 akisema nchi imeingia katika hali ngumu ya maisha.

Alisema wananchi walitarajia kuwa uchaguzi ni njia mojawapo ya kupatikana kwa maendeleo lakini imekuwa kinyume na hilo.

Alisema hali hiyo inatokana na uongozi uliopo kuendesha Serikali kibabe, badala ya kufuata sheria na utaratibu husika.

Alisema kiongozi mkuu wa Serikali amekuwa akichukua uamuzi unaoumiza wananchi na hata viongozi ikiwamo kuwashusha madaraka na wengine kuwafukuza kazi.

Alisema hadi sasa kuna msururu mkubwa wa viongozi waliofukuzwa kazi na kufunguliwa kesi kibabe, kitendo ambacho kimekuwa kinawakatisha wananchi tamaa ya maendeleo.

“Si jambo la kufurahisha na kupendeza hasa kwa kiongozi mkuu wa nchi kuwafanyia wananchi wake ubabe eti kwa kuwa ameshika madaraka, napenda ujue kuwa hali hiyo ni kuwatia hofu katika kujiletea maendeleo,” alisema.

No comments: