ANGALIA LIVE NEWS

Monday, January 9, 2017

Tanzania yatabiriwa majanga, kashfa za ngono


IMEANDIKWA NA KATUMA MASAMBAIMECHAPISHWA: 09 JANUARI 201

MRITHI wa aliyekuwa mtabiri bingwa marehemu Shehe Yahya Hussein, Maalim Hassan Yahya Hussein ametabiri mambo 20 yatakayoikumba nchi na dunia kwa mwaka huu ikiwemo kuimarika kwa uchumi wa Tanzania.

Aidha, ametabiri viongozi wa dini na kisiasa kukumbwa na kashfa mbalimbali ambazo zitasababisha maanguko katika nyadhifa zao, huku akitabiri baadhi ya viongozi wa waliovihama vyama vyao kurejea na pia kifo cha chama kimoja maarufu cha siasa hapa nchini.

Maalim Hussein ambaye ni mtoto wa Shehe Yahya aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akitoa utabiri wa matukio mbalimbali yatakayojitokeza mwaka.

Alisema mwaka huu umeanza siku ya Jumapili na kwa mujibu wa utabiri siku hiyo inashabihishwa na sayari ya jua ambapo kinyota ni nyota ya Simba ambayo asili yake ni moto, pia inaonesha kuwa ni ya ufalme, utawala na uongozi wa dini na kisiasa.

“Mwaka huu hautakuwa na rabsha nyingi lakini hautaki uharaka wa mambo. Kikubwa ni kwamba mambo huenda polepole na yanahitaji subira kwa wanaotaka mafanikio,” alisema Maalim Hussein.

Alisema mwaka huu utakuwa mgumu wa mambo, mabishano ya kisiasa, kijamii na mataifa mbalimbali kuhasimiana. Hata hivyo, kwa mujibu wa Maalim Hussein mambo yatakuwa mepesi kwa wale watakaomtegemea Mungu kwa imani za dini zao. Aidha, alisema mwanzo wa mwaka huu utakuwa mwema katika masuala ya kilimo kitakachoongeza mazao. “...kuna wanasiasa walisema serikali itangaze kuna njaa, lakini Serikali haina haraka ya kufanya hivyo, huu ni mwaka wa neema sana na mazao yatakuwa mengi,” alisema.

Alisema kinyota mwaka huu unamaanisha kuwa utagubikwa na mikasa ya kutikisika kwa ndoa, kashfa za ngono na fumanizi na kwamba watakaokumbwa na madhila hayo ni viongozi wa kisiasa, watawala, mawakili, wanasheria, wasanii, wanamichezo na waandishi wa habari.

Akizungumzia matukio yatakayojitokeza, alisema Rais Magufuli atapata nishani ya juu ya dunia kutoka kwa Rais wa moja ya mataifa makubwa kutokana na uongozi wake.

Aidha, kutatokea majanga mengi ya moto nchini na duniani pia yatatokea mafuriko yatakayosababisha vifo na madhara mengine.

Kutokea kwa mabadiliko makubwa katika tasnia mbalimbali na viongozi wake kushindwa uchaguzi, kuondolewa kwa nguvu au kukataliwa na wananchi.

“Natabiri mwaka huu kutatokea kashfa kubwa za ngono au fumanizi zitakazowahusisha viongozi wa kidini, kisiasa au wasanii maarufu zitakazosababisha viongozi hao kufedheheka na kuanguka kabisa,” alisema.

Kwa mujibu wa Maalim Hussein, mwaka huu unatawaliwa na nyota ya Simba hivyo unaashiria vifo vya ghafla vya viongozi wakubwa na wasanii maarufu na wana siasa, kidini ambavyo vitatokana na msongo wa moyo au shinikizo la damu.

Akifafanunua kuhusu viongozi waliovihama vyao alisema utabiri haumlengi mtu moja kwa moja lakini kuna viongozi mbalimbali ambao walivihama vyama vyao duniani.

Kwa hapa nchini baadhi ya viongozi wakubwa waliovihama vyao vyao ni Mawaziri Wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, Kingunge Ngombale Mwiru, pamoja na baadhi ya wenyeviti wa mikoa ambao waliotoka CCM na kwenda Chadema.

Viongozi wengine waliohama ni aliyekuwa Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali ambaye alitoka NCCR Mageuzi, kwenda ACT Wazalendo na baadae kujiunga na CCM, aliyekuwa Katibu Mwenezi wa NCCR Mageuzi, David Kafulila kuhamia Chadema na aliyekuwa mgombea ubunge wa CUF jimbo la Mafia, Mohammed Albadawi kuhamia CCM.

Aliongeza, wimbi la vifo lililoikumba tasnia ya habari mwaka jana litaendelea mwaka huu, huku akifafanua utabiri huo kutohusiana na kauli iliyotolewa na Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo, Anthony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako ambaye alisema, waandishi wa habari waliomuandika watakufa ifikapo mwezi Machi mwaka huu.

Alisema kauli iliyotolewa na Mzee wa Upako inaashiria kuporomoka kwa kiongozi huyo na kwamba hayuko karibu na Mungu kama anavyodhani, kwani mtu ambaye yuko karibu na Mungu hawezi kuwa analewa hadi alfajiri.

Mambo mengine aliyotabiri ni nchi kadhaa kuingia katika migogoro ya kimahusiano na siasa itakayosababisha vita baina yao, ajali nyingi kuwakuta wanasiasa, watawala na viongozi wa dini na kuanguka kwa vyama tawala katika nchi mbalimbali.

Maalim Hussein alisema, kuna chama maarufu cha siasa kitakufa, huku akifafanua kuwa japo hakijulikani lakini nyota zinaonesha kuondoka kwa chama hicho chenye umaarufu.

Alisema CCM itashika hatamu zaidi itakayoleta maendeleo makubwa kwa chama hicho na taifa kwa ujumla.

Viongozi wa nchi kadhaa duniani kutoa matamshi ya ajabu yatakayowashangaza wananchi wao kiwango cha kusababisha kuanguka au kuuawa kwa viongozi hao.

Utabiri huo unaonesha viongozi wa dini watatoa matamshi ya kutatanisha ambayo yanaweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani na utulivu.

“Viongozi wa kidini na kisiasa kuendelea kukumbwa na kashfa za ngono na ulevi zitakazosababisha muanguko wao. Aidha, utabiri unaonesha pia kuwa viongozi wa tasnia ya sheria watakumbwa na muanguko huo,” alisema.

Mengine ni kuzama kwa meli kwenye moja ya bahari kuu za dunia na ndege moja ya taifa kubwa duniani kuanguka na kusabaisha vifo, hali ya uchumi duniani kuimarika na viongozi wa kidini, kisiasa na taasisi za serikali, kujiuzulu nyadhifa zao kutokana na kashfa mbalimbali.

Hata hivyo, alisema vifo na maafa hayo yanaweza yasitokee iwapo watu wataacha uharaka wa kufanya mambo kama nyota ya mwaka huu inavyoonesha na pia kumrudia Mungu kwa kila jambo.

HABARI LEO

1 comment:

Anonymous said...

Huyu mtabiri ni mzuri sana. Anaweza kutabiri kuwa kesho kutakuwa na jua, au kwamba ikifika usiku watu watakwenda kulala, au kwamba usipokula unaweza kupata au kusikia njaa.