Mkuu wa Shirika la Misaada ya Kibinadamu la Samaritan’s Purse lililotoa ndege iliyowasafirisha majeruhi watatu wa ajali ya basi la Shule ya Lucky Vincent kwenda Marekani, Franklin Graham.
MWEZI mmoja baada ya kupelekwa Marekani kwa matibabu zaidi, majeruhi watatu wa ajali ya basi la Shule ya Mchepuo ya Kiingereza ya Lucky Vincent ya jijini Arusha, wameripotiwa kuwa afya zao zimezidi kuimarika kiasi cha sasa kuanza kujihudumia wenyewe ikiwamo kuoga.
Majeruhi hao, Doreen Mshana, Sadia Awadh na Wilson Tarimo, walipata ajali Mei 6, mwaka huu wilayani Karatu huku wanafunzi wenzao 32, walimu wawili na dereva wakipoteza maisha.
Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM) na Mwenyekiti mwenza wa Shirika la STEMM, Lazaro Nyalandu, Alhamisi wiki hii alitoa taarifa hizo njema kupitia mtandao wake wa Facebook, akisema madaktari wamejiridhisha kuhusu maendeleo ya kupona kwa mifupa ya watoto hao.
Alisema Sadia na Wilson walipelekwa Kituo cha CNOS (Center for Neurosurgery Orthopedics and Spine) Jimbo la Dakota Kusini, ambako madaktari walijiridhisha na maendeleo ya kupona kwa mifupa, hivyo wakawatoa bandeji ngumu.
“Sadia na Wilson wameondolewa ‘Cast’ walizokuwa wamewekewa na sasa wanaweza kujiogesha wenyewe kwa mara ya kwanza tangu wafikishwe hospitalini,” alisema Nyalandu.
Kauli kama hiyo imetolewa pia na Muuguzi wa Hospitali ya Mount Meru, Symphrosa Silali aliyeongozana na majeruhi hao, akisema; “Jumatano (ya wiki hii) watoto wote walitolewa ‘mihogo’ na wanaendelea vizuri, hatua ambayo imewawezesha kutumia viwiko vya mikono vizuri, ikiwamo kuendelea na kufundishwa namna ya kukunja mikono na kuinyoosha.
“Watoto wote wanafanya mazoezi mara tatu kwa wiki, wapo wataalamu pia wanaowafanyia mazoezi ya namna gani wanaweza kukabiliana na vitu vilivyokuwa mbele yao ili waweze kuvisahau.
Lakini pia kuna mazoezi ya viungo yanayowezesha viungo vyao kuendelea kuzoea kutumia mikono, miguu yao. Lakini pia wanafundishwa kufanya vitu vidogo vidogo wenyewe kama kupiga mswaki, kuoga na kuvaa nguo.”
Hiyo ndiyo iliyokuwa ndoto ya Watanzania wengi na hata timu ya madaktari wa ndani na nje ya nchi na Mwinjilisti maarufu wa Marekani, Franklin Graham aliyebeba gharama za kuwasafirisha na kuwahudumia watoto hao na wauguzi wao katika kipindi chote watakachokuwa Marekani.
Na mara baada ya kufikishwa Marekani kwa ndege maalumu iliyokodiwa na Graham kutoka Shirika la Misaada ya Kibinadamu analoliongoza, Samaritan Purse; mwinjilisti huyo alisema; “Ninaamini Mungu ana mipango na watoto hawa, tunawaombea waweze kupona na kurejea katika hali yao ya kawaida.”
Ndiyo, pamoja na sala na maombi ya wengi, lakini pia uwezo wa Mungu, mkono wa Graham pia umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha matibabu ya watoto hao wa darasa la saba waliokuwa wanasafiri na wenzao kwenda Karatu kwa mtihani wa majaribio, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi baadaye mwaka huu.
Amehusika moja kwa moja na gharama za kukodi ndege ya kuwachukua watoto hao kwa gharama ya takribani dola za Marekani 350,000 (Sh milioni 735), lakini pia alilipia gharama nyingine zote, kuanzia za matibabu, chakula na malazi kwa wakati wote ambao wagonjwa hao na wasindikizaji wao watakuwa nchini Marekani. Aliguswaje na ajali ya Arusha?
“Niliposikia juu ya ajali ya basi la wanafunzi Tanzania, nilijua na kuona umuhimu wa Samaritan’s Purse kufanya jambo…ndivyo ilivyokuwa. “Ninaamini Mungu ana mipango na hawa watoto, na tunawaombea ili afya zao zizidi kuimarika,” Graham amekaririwa akisema kupitoa vyombo vya habari vya Souax.
Anasema mara baada ya kupata taarifa za ajali hiyo ya Arusha na msaada unaohitajika, alihangaikia vibali vya kuiruhusu ndege kusafiri kwa saa 24 kutoka Marekani hadi Tanzania na kwa `Nguvu za Mungu’ kila jambo lilifanyika pasipo na vikwazo.
“Tunafanya haya yote kwa Jina la Yesu Kristo…lakini hatubagui dini, kwani wote ni wamoja, watoto wa Mungu,” anasema. Ilivyokuwa Timu ya madaktari ikiongozwa na Dk Steve Meyer wa STEMME, iliwasiliana na Dk Steven Joyce, Mkurugenzi mwenza wa Hospitali ya Mercy inayowatibu watoto hao na kuhakikishiwa kuwa, wako tayari kufadhili tiba ya watoto hao kama watafikishwa Marekani.
Ndipo yakaanza mawasiliano kwa njia ya simu baina ya mashirika, serikali ya Tanzania na wadau wengine yaliyozaa matunda baada ya saa 60 na kupata uhakika wa safari hiyo. Baada ya kuzungumza na uongozi wa hospitali ya Mercy, alimgeukia Mbunge Steve King, mtu wa karibu wa Graham aliyemuunganisha na mwinjilisti huyo aliyepiga simu kwa Dk Meyer kumweleza atabeba gharama za safari na mambo mengine.
Franklin Graham ni nani hasa? Franklin ambaye Julai 14 mwaka huu anatarajiwa kutimiza umri wa miaka 65, ni mtoto mkubwa wa Mwinjilisti bilionea, Bill Graham, mwasisi wa taasisi ya Billy Graham Evangelistic Association (BGEA) ambayo tangu mwaka 2001 inaongozwa na Franklin. Akiwa na umri wa miaka 22 mwaka 1974, aliokoka akiwa hotelini huko Yerusalemu.
Mwaka huohuo, alimuoa Jane Cunningham na mpaka sasa amebahatika kuzaa naye watoto wanne, William Franklin Graham IV (Will) aliyezaliwa mwaka 1975, Roy Austin Graham (1977), Edward Bell Graham (1979) na Jane Austin Graham Lynch (Cissie) (1986).
Graham na mkewe wamebahatika kupata wajukuu 11. Alikomazwa katika imani ya dini na wasaidizi muhimu wa baba yake, Bill Graham; Roy Gustafson na John Wesley White. Na baada ya kuiva, aligeuka mhubiri, akipata sifa kila uchao.
Tangu mwaka 1989, Graham amehubiria neno la Mungu watu milioni 126 katika mikutano mbalimbali ya kidini duniani. Mara baada ya kuokoka mwaka 1974, Graham aliungana na Bob Pierce,mwanzilishi wa shirika la Samaritan's Purse na kufanya naye kazi kwa wiki sita huko barani Asia.
Akiwa huko, Graham alipata nguvu zaidi ya kuigeukia dunia ili kutoa misaada zaidi ya kibinadamu, dhamira aliyoiendeleza hata baada ya kifo cha Pierce naye kukabidhiwa rasmi nafasi ya kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika kuanzia mwaka 1979. Tangu wakati huo, shirika lake limefanya kazi katika nchi zaidi ya 100 duniani.
Shirika hilo hutoa misaada kwa waathirika wa migogoro, maafa, njaa na milipuko ya magonjwa sehemu mbalimbali dunia lakini pia husaidia chakula, maji, sehemu za makazi ya muda, matibabu na huduma nyingine za misaada ya kibinadamu.
Mbali ya kuhubiri na kusimamia misaada ya kibinadamu, Franklin pia ni mtunzi wa vitabu vya `kiroho’, baadhi vikiwa A Wing and a Prayer (2005), All for Jesus (2003), Kids Praying for Kids (2003), The Name (2002), Living Beyond the Limits: A Life in Sync with God (1998), Rebel With A Cause: Finally Comfortable Being Graham (1995), Miracle in a Shoe Box (1995) na Bob Pierce: This One Thing I Do cha mwaka 1983.
Huyo ndiye Bill Graham, mwinjilisti aliyeongeza nguvu katika kufanikisha matibabu ya majeruhi watatu wa ajali ya basi la shule la Lucky Vincent ya jijini Arusha. Mbali ya misaada ya hali na mali kutoka kwa Watanzania, hospitali ya Mercy na pia gharama nyingine zilizobebwa na Graham kutokana na ajali hiyo, Bodi ya wadhamini ya Shirika la STEMM (Siouxland Tanzania Educational Medical Ministries) limeamua kuwaenzi watoto 32 waliopoteza maisha katika ajali ya Karatu kwa kuwasomesha majeruhi hao hadi elimu ya chuo kikuu.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment