ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 19, 2017

WCF YATOA MUONGOZO WA TATHMINI YA UGONJWA NA AJALI KWA MADAKTARI


Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Emmanuel Humba, akifungua mafunzo ya siku tano kwa madaktari 70 kutoka hospitali 35 za umma na binafsi jijini Dar es Salaam kuhusu namna  ya kufanya tathmini ya ugonjwa na ajali, kabla ya kumlipa fidia mfanyakazi aliyeathirika. Wakwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba na katikati ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini wa Mfuko huo, Dkt. Abdulsalaam Omar

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, WCF, Bw. Masha Mshomba, (aliyesimama),akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tano kwa madaktari kuhusu namna ya kufanya tathmini ya ugonjwa na ajali apatayo Mfanyakazi mahala pa kazi ili taratibu za fidiwa zifanyike. Mafunzo hayo yaliyowaleta madaktari 70 kutoka hospitali 35 za umma na binafsi za jijini Dar es Salaam, yameanza leo Juni 19, 2017. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya WCF, Bw. Emmanuel Humba, na katikati ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini wa Mfuko huo, Dkt. Abdulsalaam Omar
 Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini wa Mfuko huo, Dkt. Abdulsalaam Omar, akizungumza kwenye mafunzo hayo
 Sehemu ya madaktari wanaohudhuria semina hiyo
 Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba, (kushoto) akiteta jambo na Daktari Bingwa wa upasuaji na majeruhi wa Taasisi ya Mifupa MOI, Dkt. Robert Mhina
 Dkt. Daniel Estomiah Kimaro, kutoka hospitali ya Bochi akizunguzma kwenye mafunzo hayo
 Mtaalamu mbobezi wa masuala ya afya na kazi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili jijini Dar es Salaam, (MUHAS), Yahya Kishashu, (kushoto), na Daktari bingwa wa upasuaji na majeruhi, kutoka MOI, Dkt.Robert Mhina, wakiwasilisha mada juu ya magonjwa yatokanayo na kazi pamoja na ajali mahala pa kazi.
 Bw. Masha akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo
 Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshomba, (kushoto), Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw.Anselim Peter, Mkuu wa Kitengo mcha Sheria cha Mfuko, Bw. Abraham Siyovelwa, na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Bi. Laura George, wakibadilishana mawazo wakati wa mapumziko ya chai.
 Afisa Uhusiano wa WCF, Bi. Zaria Mmanga, akigawa taarifa mbalimbali zihusuzo mafunzo hayo
 Meneja Madai wa WCF, Bi. Rehema Kabongo, (katikati), akizungumza jambo na Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Bi. Laura George, (kulia) na kushoto ni Afisa Uhusiano wa WCF, Bi. Zaria Mmanga


 Maafisa wa juu wa WCF, bw. Stephen Goyayi, (Kushoto) na Bw. james Tenga, wakiwa kwenye mafunzo hayo

Picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi na uongozi wa WCF

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi, WCF, umetoa muongozo utakaotumiwa na madaktari na watoa huduma za afya, wakati wa kufanya tathmini ya ugonjwa na ajali kwa mfanyakazi aliyepata madhara mahala pa kazi.
Muongozo huo ni miongoni mwa masuala mbalimbali watakayojifunza madaktari wapatao 70 kutoka hospitali 35 za umma na binafsi za jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mafunzo hayo,  Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw  Masha Mshomba, alisema kuwa  madaktari ni wadau muhimu sana  katika kufanikisha shughuli za Mfuko huo.
“Tunataka hawa  madaktari wawe na ujuzi wa kutosha utakaowawezesha kufanikisha azma yetu, na tumeamua kuwa mafunzo ya aina hii yatakuwa endelevu ikiwa ni pamoja na kuwapatia muongozo utakaowasaidia kutekeleza majukumu yao ya kufanya tathmini,” alisema.
Alisema kuwa katika jitihada za kuendeleza mafunzo hayo, Mfuko huo una mpango wa kushirikiana na vyuo vikuu nchini katika kutoa huduma hiyo.
Kuhusu wafanyakazi walioripoti matukio ya ajali kazini  kwenye Mfuko huo hadi hivi sasa, alisema jumla ya kesi 670 za wafanyaakzi walioumia na kuhitaji matibabu zimepokelewa.
Alisema kuwa  wengi wa wafanyakazi waliopatwa na matatizo hayo kazini wanatoka sekta mbali mbali kama migodi, viwanda na usafirishaji. Aliwaomba wafanyakazi walioumia wakiwa kazini kuwasiliana na Mfuko huo ili kuweza kusaidiwa.
Alibainisha kuwa Mfuko umeingia mkataba na watoa huduma za afya kwenye hospitali na  vituo vya  afya  zaidi ya 6,000 nchi nzima ambapo zitahudumia wafanyakazi hao.
Alisema huduma za matibabu zinatolewa kwa mfanyakazi atakayeumia au kuugua kutokana na kazi. Huduma hizo ni ya gari la kubeba wagonjwa, kumuona daktari,upasuaji, uuguzi, dawa, kurudia matibabu itapobidi na kupatiwa viungo bandia.
Alibainisha kuwa wajibu wa mfanyakazi ni pamoja na kuifahamu sheria ya fidia kwa wafanyakazi, (sura 263 marejeo ya mwaka 2015), kutoa taarifa kwa wakati kwa mwajiri au Mkurugenzi Mkuu pindi atakapopatwa na ajali kazini au kubainika kuwa na magonjwa yanayotokana na kazi.
Aliwaomba wafanyakazi hao kutoa ushirikiano pindi wanapotakiwa kufanyiwa uchunguzi wa matibabu, kuzingatia maelekezo yatolewayo na Mamlaka mbali mbali  kuhusu usalama mahali pa kazi, kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbali mbali kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi , kutunza kumbukumbu binafsi zinazohusu masuala ya kazi.
Akifungua mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya WCF, Emmanuel Humba aliwashauri madktari hao kufanya kazi zao kwa weledi zaidi ili kuongeza tija na ufanisi kwa lengo la kuiwezesha sekta hiyo kuongeza wigo wa upana wa  huduma.
Bw. Humba alisema kuwa  azma ya mfuko huo kuwa na mtandao mkubwa wa watoa huduma za afya nchi nzima ambao watasaidia Mfuko kutoa fidia stahiki kwa mfanyakazi aliyepata maradhi au majeraha wakati akitekeleza wajibu wake kazini.
“Nyie ni wadau muhimu sana katika kutuwezesha sisi kufanya kazi zetu vizuri ninawaombeni  mzingatie yote mtakayofundishwa kwenye mafunzo haya  na kuongeza weledi  wenu ,” alisema.
Alisema kuwa watoa huduma hao ndio tegemeo kubwa la kupata taarifa sahihi za mgonjwa pindi anapopata matatizo akiwa kazini, kwani  ndipo utaratibu wa malipo au fidia unapoanzia.
“Lazima mjue kuwa pakitokea tatizo lolote la mfanyakazi kulipwa fidia tutanzia kwenu ili kutupa taarifa sahihi kuhusu wagonjwa wa aina hiyo,” alifafanua.
Aidha Bw Humba aliwataka madaktari hao kusaidia kuwaelimisha wateja wao juu ya huduma mbali mbali zinazotolewa na mfuko huo.
“Mara nyingine unaweza kukutana na mgonjwa akakuuliza kuhusu huduma zinazotolewa na Mfuko huu, ndio maana tumewaita hapa kuwaelezeni  yote, tunaomba mtusaidie kuwaelimisha,” alisisitiza.
Mwenyekiti huyo, aliutaka uongozi wa Mfuko  huo kuangalia namna ya kuyafanya mafunzo hayo kuwa endelevu .
“Ninashauri uongozi wa mfuko kuwa na mafunzo  endelevu ya aina hii, ili kuwakumbushia watoa huduma wetu  waweze kuendena na wakati,” alisema.
Alidokeza kuwa  hadi sasa Mfuko umekwisha endesha mafunzo ya aina hiyo sehemu mbali mbali nchini na kushirikisha madaktari wapatao 359.
“Tulianza  kutoa mafunzo ya aina hii mwaka 2015 ambapo tumewashirikisha madaktari kutoka  Kanda ya Mashariki, Ziwa, Kaskazini na Nyanda za Juu Kusini,”alisema

No comments: