ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 28, 2017

TUME YA UCHAGUZI YAVITAKA VYOMBO VYA HABARI NCHINI KUIGA WENZAO WA KENYA

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani (kulia) akifafanua jambo wakati akizungumza na Mtangazaji wa Azam Tv, Nurdin Selemani kupitia kipindi cha Mizani ya Wiki kilichorushwa jana Jumapili.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media, Tido Mhando baada ya kushirikia kwenye kipindi cha Mizani ya Wiki kinachorushwa na Azam Tv Jumapili usiku.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhani (kushoto) , akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media Tido Mhando Ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 na Taarifa ya Tathmini Baada ya Uchaguzi huo.Picha na Hussein Makame.

Na Mwandishi Maalum
MKURUGENZI wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Ramadhan amevitaka vyombo vya Habari vya Tanzania viige mfano wa wenzao wa Kenya kwa kutumia muda mwingi kutoa Elimu ya Kupiga kura. Akizungumza kwenye kipindi cha Mizani ya Wiki kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha AZAM Jumapili usiku, Ramadhan alisema moja ya mambo aliyojifunza katika Uchaguzi Mkuu wa Kenya ni jinsi vyombo vya Habari vilivyoshiriki katika Uchaguzi huo na kuchangia watu wengi kujitokeza kupiga kura..

“Natamani na sisi vyombo vya hapa nyumbani viige wenzao wa Kenya ambao walitoa muda mwingi kwa kutoa Elimu ya Mpiga kura,” alisema Ramadhani. aliongeza kuwa baadhi ya mambo ambayo amejifunza kwa Tume Huru na Mipaka ya Kenya (IEBC) katika uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni ni usambazaji wa vifaa katika vituo vya kupigia kura. Alifafanua kuwa licha ya kuwa Kenya wana vituo vichache takribani 40,000 vya kupigia kura ukilinganisha na vya Tanzania ambako kuna vituo 65,000, lakini alisema walifanya vizuri kwenye kusambaza vifaa.

Eneo lingiine ambalo lilimvutia ni namna wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi katika Kituo cha kupigia kura wanavyokuwa na uelewa mkubwa kuhusu taratibu za kupiga kura. Kuhusu kuruhusu wafungwa na Wakenya walioko nje kupiga kura, Kailima alisema kwa sasa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi hairuhusu jambo hilo na akaongeza kuwa Tume haina pingamizi iwapo wabunge watatunga sheria inayoruhusu makundi hayo kujiandikisha na baadaye kupiga kura. “Tume ya Uchaguzi haina mamlaka ya kuamua ni nani apige kura, ila tunaongozwa na katiba pamoja na sheria,” alisema.

Akizungumza utaratibu wa kupiga kura uliotumika Kenya, alisema ni mzuri lakini akaongeza kuwa utaratibu unaotumiwa na NEC uko wazi ukilinganisha na ule uliotumiwa na IEBC. “Utaratibu wetu ni mzuri zaidi kwani unatoa fursa ya mawakala kujiridhisha kwamba mtu aliyeenda kupiga kura ndiye mwenyewe, unapunguza kelele,” alisema .

Akilinganisha teknolojia iliyotumiwa na IEBC, Ramadhan alisema inawezeshwa mtu akipiga kura inahesabiwa jambo ambalo ilisababisha IEBC kutangaza matokeo ya awali ambayo hayajathibitishwa na akaongeza kuwa hilo ni jambo la hatari kwa kuwa matokeo ya pili yakibadilisha matokeo ya awali inaweza kuleta sintofahamu. Alisisitiza kwamba mfumo ambao unatumiwa na NEC bado pia ni mzuri kwa kuwa unalenga kutangaza matokeo ambayo yameshathibitishwa na yanaleta amani kwa jamii.

“Uchaguzi ulipita tulitangaza matokeo ya urais ndani ya saa 72 kwa hiyo tuliwahi kuliko wenzetu wa Kenya.”

No comments: