Mkuu wa Idara ya Utafiti na Machapisho wa Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Profesa Fortunata Makene akitoa neno la ukaribisho kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Tausi Kida wakati wa mkutano wa awamu ya pili ya kuangalia Tabia nchi, Uboreshaji kilimo, na mahusiano yake na biashara kwa jumuiya ya Afrika Mashariki (PACT EAC2), uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ESRF jijini Dar es Salaam.
WATAALAMU na wanazuoni wamekubaliana haja ya kupitia mpango wa maendeleo endelevu wa viwanda, SIDP (1996-2020), ili kwenda na wakati kwa kubadili kilimo na kuiweka nchi katika njia bora ya kufikia uchumi wa viwanda.
Kauli hiyo imetamkwa kwa namna tofauti na wataalamu hao ambao wamekutana jijini hapa kuangalia uhusiano uliopo kati ya viwanda, mabadiliko ya tabia nchi na kilimo; na ni namna gani sera ya viwanda inaweza kupitiwa upya kuakisi mahusiano haya.
Warsha hiyo iliyoandaliwa na ESRF na CUTS International imelenga katika kuelezea umuhimu wa kuangalia mahusiano ya sera ya maendeleo ya viwanda na mabadiliko ya tabia nchi, usalama wa chakula na biashara.
Wakijadili mada mbalimbali zilizowasilishwa katika semina hiyo iliyofanyika ESRF, wataalam hao walitambua umuhimu wa pekee wa kupitia upya sera hiyo ili iweze kuonesha muunganiko fasaha uliopo kati ya viwanda, kilimo na biashara; na hatua/mikakati ipi iwepo kukinga adhma hii ya viwanda dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Wamesema kwamba kwa kuunganisha sera ya maendeleo endelevu ya viwanda na uchakataji wa bidhaa za kilimo na kilimo chenyewe kunaleta mwanya wa kuweka msingi imara katika mchakato wa maendeleo na hasa viwanda. Pia, kwa kuwa na sera madhubuti, nchi itaweza kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya Viwanda, hususani viwanda vinavyotegemea maligafi za sekta ya kilimo.
Katika mkutano huo ilikubalika haja ya kuwa na mikakati ya utetezi kwa kuangalia tafiti zitakazofanywa juu ya kinachojiri katika maendeleo kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia nchi, usalama wa chakula na biashara. Zaidi ya yote, pia wadau waliona kuna haja kubwa ya kuwa na tafiti itayoweza kuonesha ni kwa kiasi gani sera ya SIDP (1996-2020) imeweza kuchangia katika ukuaji wa viwanda Tanzania, na changamato zipi imekumbana nazo ambazo zinapaswa kutatuliwa na kuanishwa wakati wa mapitio ya sera hii.
Akiwasilisha hoja yake ndugu Solomon Baregu, Mtafiti wa ESRF na Meneja wa Mradi wa PACT EAC 2, amesema kwa kuangalia hali halisi ya sasa ipo haja kwa wataalamu kutambua changamoto zinazojitokeza katika maendeleo endelevu ya viwanda na kukiangalia kilimo kama msingi wa uimarishaji wa viwanda.
Aidha alisema kwamba kwa kuangalia hali ya sasa ipo haja kubwa ya kubadili kilimo cha Tanzania ili kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha viwanda kwa kuvipatia mali ghafi ya kutosha na yenye ubora.
Alisema ni vyema kuelewa uhusiano uliopo katika sera za maendeleo ya viwanda na kilimo ili kuwa na mpango mahsusi wa utetezi kwa lengo la kuimarisha viwanda.
Katika mkutano huo washiriki pia walipitia mambo mbalimbali na hatua zinazochukuliwa kupitia sera ya mpango wa maendeleo wa viwanda unaomalizika 2020.
Mkurugenzi Msaidizi wa idara ya Ushirikishaji Kikanda kutioka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bi. Sekela Mwaisela akisoma hotuba ya ufunguzi kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo wakati wa mkutano wa awamu ya pili ya kuangalia Tabia nchi, Uboreshaji kilimo, na mahusiano yake na biashara kwa jumuiya ya Afrika Mashariki (PACT EAC2), uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano ESRF jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa mambo yaliyojitokeza kwenye mazungumzo ya tafiti ni umuhimu wa kuoanisha sera mbalimbali katika kilimo na viwanda kuzihuisha na kuzipa mwelekeo wenye maana kama chachu katika kuimarisha uchumi wa viwanda.
Walisema ipo haja ya kuangalia sera hizo ili ziwe msaada katika kuimarisha kilimo na kutoa ushindani kwa viwanda vinavyotegemea bidhaa za kilimo ili kujiimarisha.
Aidha katika mazungumzo kwenye mkutano huo imeelezwa kuwa ingawa serikali kupitia wizara zake mbalimbali na Ofisi ya Makamu wa Rais wamechukua hatua kadhaa kuwa na matokeo bora katika utetezi wa bidhaa za viwanda zinazotokana na kilimo, kukosekana kwa uangalizi na utekelezaji wa pamoja kumeleta shida kwa wananchi.
Sera ya sasa ya maendeleo endelevu ya viwanda (SIDP) imetengenezwa mwaka 1996 na itaisha 2020 lakini bado ipo haja ya kuweka mahusiano katika utekelezaji wa mpango huo wa maendeleo, kwani kwa mazingira ya sasa hakuna mahusiano na kuna vikumbo katika sera mbalimbali.
Wamesema kwamba sera hiyo haitoi mwanya wala mahusiano kati ya viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, mabadiliko ya tabia nchi, biashara na usalama wa chakula.
Mtafiti wa ESRF na Meneja wa Mradi wa PACT EAC 2, Solomon Baregu akiwasilisha namna bora ya kufanya utafiti wenye lengo la kuoanisha mpango wa maendeleo endelevu ya viwanda na mabadiliko ya tabia nchi na kilimo wakati wa mkutano huo wa kuzungumzia mradi wa PACT-EAC2 uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ESRF jijini Dar es Salaam.
Aidha walisema kwamba mpango wa pili wa maendeleo (2016/17-2020/21) unaonesha haja ya kuweka Tanzania katika njia ya viwanda kwa kuijengea nchi uwezo wa kuzalisha katika kilimo na pia katika ufugaji.
Haja ya kubadilisha Kilimo inatokana na ukweli kuwa ni moja ya sekta zinazoingiza kipato cha kigeni kwani inachangia asilimia 29.1 ya pato la taifa, huku ikichangia asilimia 30 ya fedha za kigeni.
Aidha ndio chanzo pekee cha uhakika cha biashara ikitoa asilimia 65 ya mahitaji ya viwanda (ghafi) na asilimia 90 ya chakula cha taifa huku ikiajiri asilimia 66.9 ya nguvu kazi ya Taifa.
Ndugu Peter Lanya, aliekua Makamu Mwenyekiti wa TCCIA, akitoa ufafanuzi zaidi alisema kwamba kunatakiwa mabadiliko katika sera hiyo ili kuupa usasa kwa kuwekeza kwenye mahusiano ya kilimo, mali ghafi kama taifa likitaka kuendelea kuelekea uchumi wa viwanda.
Naye ndugu, Joseph Kihaule, Afisa Mkuu wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Raisi, alisema kwamba kuna haja ya kubadilika katika kilimo ili kuweza kufanya vyema huku akisema mazungumzo ya kimataifa ya kupata muafaka, hususani yahusuyo mabadiliko ya tabia nchi, ni muhimu yakaunganishwa na sera mbalimbali ili kuimarisha kilimo na upatikanaji wa chakula.
Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa TCCIA, Peter Lanya akizungumzia SIDP 1996-2020 wakati wa mkutano wa awamu ya pili ya kuangalia Tabia nchi, Uboreshaji kilimo, na mahusiano yake na biashara kwa jumuiya ya Afrika Mashariki (PACT EAC2), uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ESRF jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa idara ya Ushirikishaji Kikanda kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Bi. Sekela Mwaisela.
Awali akifungua semina hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na uwekezaji (viwanda) Adelhelm Meru alishukuru taasisi za ERSF na CUTS International kwa kuona umuhimu wa kuwa na mkutano huo wanne wa kitaifa kuzungumzia mradi wa PACT-EAC.
Katika hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi msaidizi Wizara ya Viwanda Ushirikishaji Kikanda, Bi. Sekela Mwaisela alisema kwamba wizara inatambua haja ya kuweka pamoja viwanda na uchakataji wa mazao ya kilimo kwa kuwa inasaidia kuweka sawa maendeleo ya viwanda.
Alisema kwamba kazi iliyofanywa na ESRF inaiweka wizara hiyo katika nafasi bora zaidi ya kufanya mabadiliko ya muhimu kufikia mwaka 2020.
Alisema sera hiyo iliyoanza 1996-2020 imepita katika maeneo matatu ambayo yalilenga kuimarisha uwezo wa viwanda (1996-2000), matumizi ya teknolojia (2000-2010) na uimarishaji wa viwanda 2010-2020.
Alisema SIDP imesaidia kuimarisha viwanda na sasa lazima kuwepo na uangalizi ili kuwepo na mahusiano mazuri kati ya sera zote zinazotegemewa kuwezesha maendeleo endelevu ya viwanda.
Afisa Mkuu wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Joseph Kihaule akichangia maoni katika mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa ESRF jijini Dar es Salaam.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Tausi Kida katika hotuba yake iliyosomwa na Prof. Fortunata Makene amesema ipo haja kubwa ya kuwepo kwa mabadiliko katika SIDP kutokana na mahusiano yake na sekta nyingine hasa yenye uhusiano na kilimo.
Katika mkutano huo wa awamu ya pili ya kuangalia Tabia nchi, Uboreshaji kilimo, na mahusiano yake na biashara kwa jumuiya ya Afrika Mashariki (PACT EAC2), Dk Kida alisema kwamba taasisi yake imefurahi kutoa mchango kwa ajili ya kusaidia kuimarisha viwanda nchini.
Alisema mkutano huo unaoangalia namna ya kuboresha sera ya viwanda, SIDP (1996-2020), kabla ya utafiti utakaoanza baadae ni muhimu katika kuona kwamba kilimo kinaboreshwa sanjari na SIDP kwa kuweka mahusiano ambayo awali yalikosekana katika sera ya SIDP.
Pichani juu na chini sehemu ya washiriki wakichangia maoni wakati wa mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa mikutano ESRF jijini Dar es Salaam.
Alisema kwa taifa la Tanzania ili lisonge mbele ni vyema masuala muhimu katika SIDP yakaangaliwa ili kutekeleza mipango ya maendeleo ya viwanda kwa kuhusisha na uchakataji wa mazao ya kilimo.
Aidha alisema katika utafiti utakaosaidia kuboresha SIDP majukumu ya biashara ya kimataifa katika maendeleo ya viwanda na tabia nchi haviwezi kudharaulika.
Alisema utafiti utakaofanywa utasaidia kuongeza ‘nyama’ zaidi katika mikakati ya maendeleo kwa kufanya utetezi kwenye mabadiliko ya tabia nchi, biashara na usalama wa chakula kwa kufanya mabadiliko makubwa katika uchakataji bidhaa za kilimo kwa kutambua pia makubaliano ya kimataifa ambayo Tanzania ni mshiriki, hususani UNFCCC na WTO.
Picha juu na chini washiriki kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi walioshiriki kwenye mkutano huo.
Picha ya pamoja ya washiriki.
No comments:
Post a Comment