Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA, Eng Karim Mattaka, akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (wa pili kulia), kuhusu hatua za ujenzi wa gati ya Lindi, wakati Waziri huyo alipotembelea mradi kukagua maendeleo yake.
Muonekano wa Gati mpya ya Bandari ya Lindi ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia zaidi ya 90. Gati hiyo imegharimu kiasi zaidi ya shilingi bilioni 3 ikiwa ni fedha za Serikali kwa asilimia 100.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akipanda kwenye boti kuelelekea katika eneo la Kitunda mkoani Lindi, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa maegesho ya kivuko Mkoani humo. Waziri Prof. Mbarawa amewahakikishia wakazi wa Mkoani humo kuwa kivuko hicho kitawasili na kuanza kutoa huduma mwishoni mwa wiki hii.
Muonekano wa hatua ilipofikia Gati ya kuegeshea kivuko katika eneo la Kitunda Mkoani Lindi. Ujenzi wa Gati hiyo umefikia asilimia zaidi ya 90 na imejengwa kwa fedha za Serikali.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa (kushoto) akishiriki katika kuchanganya zege katika ujenzi wa barabara ya maegesho ya kivuko Mkoani Lindi, alipokagua maendeleo ya ujenzi wake.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa akiongea na wakazi wa Mkoani Lindi, mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi maegesho ya Kivuko. Waziri Prof. Mbarawa amewahakikishia wakazi hao kuwa kivuko kitawasili katikatia ya wiki na kuanza kazi mwishoni mwa wiki.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA) kwa kukamilisha ujenzi wa gati ya Lindi na kuwataka kutafuta masoko ili bandari hiyo iweze kunufaisha Serikali na wananchi wa Mkoa huo.
Prof. Mbarawa ametoa kauli hiyo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati hiyo mkoani Lindi ambapo amesema mradi umekamilika kwa asilimia 92 na kukamilika kwa gati hiyo kutarahisisha biashara na kukuza uchumi kwa wananchi kwani meli kubwa zitaanza kutia nanga katika bandari hiyo.
“Napenda kuwapongeza sana TPA kwa kazi kubwa mliyoifanya kukamilisha mradi huu, ni wakati sasa mkatafute masoko ili mpate faida na kurahisisha usafirishaji kati ya mkoa huu na visiwa vinavyozunguka” amesema Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa ameongeza kuwa pamoja na kukamilisha mradi huo TPA itunze miundombinu hiyo na kuifanyia ukarabati wa mara kwa mara ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Karim Mattaka, amemuhakikishia Waziri Prof. Mbarawa, kuwa Mamlaka itazingatia maelekezo yake na kuahidi kusimamia sehemu ndogo iliyobaki ili iweze kukamilika kwa wakati na viwango vilivyokubaliwa.
Mhandisi Mattaka ameongeza kuwa ujenzi wa gati hiyo imegharimu kiasi cha shilingi zaidi ya bilioni 3 na fedha hizo zimefadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika hatua nyingine Waziri Profesa Mbarawa, amesema Kivuko kwa ajili ya Lindi na Kitunda kitawasili mapema katikati ya wiki ili kianze kutoa huduma kwa wakazi wa mkoa huo.
Aidha ameauagiza uongozi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kuhakikisha wanatafuta fedha na kujenga majengo ya abiria kwa upande wa Lindi na Kitunda ili kupunguza changamoto inayowakabilia abiria hasa nyakati za mvua.
Naye Mkandarasi wa Kampuni ya Hematec, Emmanuel Lyimo amesema mpaka sasa ujenzi uko kwenye hatua za mwisho na ambapo ndani ya siku chache mradi huo utakamilika na kukabidhiwa kwa ajili kuanza kutoa huduma.
Waziri Prof. Mbarawa amemaliza ziara yake ya siku mbili kwenye mikoa ya Mtwara na Lindi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya Bandari na Vivuko.
No comments:
Post a Comment