ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 18, 2018

Jecha Salim Jecha Ang'atuka Tume ya Uchaguzi Zanzibar

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha amemaliza muda wake wa majukumu ya tume hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kilichoanzia Aprili 30,2 013 hadi Aprili 29, 2018 ambapo yeye na wajumbe wa tume hiyo wamekabidhi ripoti yao ya kazi.

Akitoa taarifa yake kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, Jecha amesema kuwa tume inaamini kwamba, mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa majukumu yake hasa ya kiuchaguzi yalitokana na ushirikiano wa wadau mbalimbali na wananchi kwa jumla.

"Ndani ya miaka mitano tume imeweza kuendesha jumla ya chaguzi ndogo nne, zikiwemo chaguzi ndogo tatu za Udiwani na chaguzi moja ya uwakilishi pamoja na kusimamia uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25,2015 na ule wa marudio yake Machi 20, 2016. Tume imefanya mapitio ya majimbo ya uchaguzi na kubadilisha mipaka ya majimbo ya uchaguzi, majina ya majimbo na kuongeza idadi ya majimbo kutoka 50 hadi 54", ameeleza Jecha.

Pamoja na hayo, Jecha ameendelea kwa kusema "Tume imeweza kufanya uandikishaji wa wapiga kura kwa awamu mbili na kuliendeleza daftari la kudumu la wapiga kura sambamba na kuendesha programu mbalimbali za elimu ya wapiga kura kupitia vyombo vya habari, mikutano ya wadau, uchapishaji wa vipeperushi, majarida na makala mbalimbali".


Aidha, Mwenyekiti huyo amemueleza Dkt. Shein kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imechaguliwa kuwa kiongozi wa Uchaguzi Mkuu wa nchini Congo utakaofanyika mwezi Disemba mwaka huu.

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein ameipongeza Tume hiyo kwa kutekeleza vyema majukumu yake ndani ya miaka mitano kwa kuendesha chaguzi zote .

"Tume hii inastahiki pongezi kwa kuifanikisha vyema kazi waliyopewa ikiwa ni pamoja na kuendesha chaguzi zote ukiwemo uchaguzi Mkuu, chaguzi ndogo na ule uchaguzi wa marudio ambazo zote hizo zilifanywa kwa ufanisi mkubwa", amesema Dkt. Shein.

Wajumbe wa tume hiyo ambao wamemaliza muda wao ni Mwenyekiti mwenyewe Jecha Salim Jecha, Jaji Abdul-hakim Ameir Issa, Balozi Omar Ramadhan Mapuri, Nassor Khamis Mohammed, Ayoub Bakari Hamad, Haji Ramadhan Haji na Salmin Senga Salmin ambao wote hao waliapishwa rasmi  Mei,4, 2013.

No comments: