ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 11, 2018

LISU KUFANYIWA UPASUAJI WA 20

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu leo atafanyiwa upasuaji mwingine katika mguu wake wa kulia, hii ikiwa ni mara ya 20 tangu alipoanza kutibiwa baada ya kushambuliwa kwa risasi mjini Dodoma, Septemba mwaka jana.

Akizungumza na Mwananchi jana ilipotaka kujua maendeleo ya afya yake, Lissu alisema madaktari wamebaini bakteria katika mguu wake wa kulia hivyo wameamua kumfanyia upasuaji ili kuwaondoa.

“Kesho nitafanyiwa upasuaji katika huu mguu wangu wa kulia ambao uliumizwa sana. Operesheni inafanyika baada ya madaktari kubaini bakteria katika mifupa hivyo wamesema wakiunga bila kuwatibu bakteria itakuwa ni tatizo,” alisema Lissu jana.

Lissu, aliyeko nchini Ubelgiji kwa matibabu, alifanyiwa upasuaji wa 19 Machi mwaka huu ikiwa ni mwendelezo wa matibabu aliyokuwa akifanyiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikopelekwa akitokea Dodoma baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana.

Lissu, ambaye pia ni rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema baada ya upasuaji huo wa leo, utafuata mwingine wa kuunga mfupa.

“Niseme tu naendelea vizuri sana. Ninawashukuru Watanzania kwa kunitibu, kwani wenye jukumu la kufanya hivyo wamekataa lakini Watanzania hawajanitupa,” alisema.

No comments: