Dodoma. Hoja ya mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kuhusu kutoendelezwa kwa miradi ya gesi asilia, jana iliibuka tena wakati wa kujibu hoja zilizoibuliwa na wabunge kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu, kiasi cha kumlazimisha Spika Job Ndugai kuagiza suala hilo lipatiwe majibu sahihi katika Bunge lijalo.
Mapema jana wakati mawaziri wakijibu hoja zilizoibuka katika hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alielezea kuwa suala hilo liko kwenye Ilani ya Uchaguzi na kwamba miradi hiyo haijatelekezwa kama Nape alivyoonyesha hofu juzi.
Lakini wakati wa kupitisha vifungu vya bajeti hiyo, suala hilo liliibuliwa tena na mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobale aliyesema Serikali ya Awamu ya Nne ilianzisha miradi ya uendelezaji wa miradi ya gesi, lakini ilienda sambamba na mradi wa LNG mkoani Lindi. Alisema kuanzia mwaka jana inaonekana kama mradi huo umesimama na kwamba hawaoni maendeleo.
“Lakini kilichokuwa kibaya zaidi gesi imegunduliwa mpakani na Msumbiji na wao wameanza kufanya LNG na gesi ni bidhaa inayoweza kuhama sehemu moja kwenda kwingine. Kwakuwa Msumbiji wameshaanza utekelezaji wanaweza wakachukua gesi tukija kustuka hakuna. Naomba maelezo ya kina mradi umekwamia wapi,” alisema.
Akijibu hoja hiyo, Dk Kalemani alisema mradi wa LNG haujakwama popote na kwamba ni kweli Msumbiji wana mradi kama huo lakini mradi wa Tanzania uko palepale.
Alisema mazungumzo yalifanyika juzi baina ya Serikali na kampuni ya Statoil na mengine jana na hivyo kumtoa wasiwasi mbunge huyo.
Majibu hayo yalimfanya Spika wa Bunge Job Ndugai kusema kuwa katika bajeti ya mwakani hawataki kusikia kuwa bado wanajadiliana.
“Maana kwa kweli gesi ni uchumi mkubwa. Gesi itatusaidia sana kwa hiyo sisi mwakani hatutaki kusikia,” alisema.
“Kwa hiyo maneno yako tunayachukua mwaka huu, mwakani kama bado mnajadiliana kidogo patakuwa moto.”
Hata mbunge mwingine alipojaribu kutaka maelezo zaidi ya suala hilo, Spika Ndugai alisema Bunge limeshatoa maagizo na hivyo hakuna haja ya kuendelea kujadili.
Juzi, Nape aliibua hoja hiyo, akisema walinadi ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwamba gesi itakuwa mkombozi katika uchumi.
Alisema kura nyingi alizozipata Rais John Magufuli ni kwa sababu ya makubaliano hayo, lakini anaona kama mradi wa Stieglers Gorge unachukua nafasi ya gesi.
No comments:
Post a Comment