ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 11, 2018

MAGONJWA 10 YASABABISHAYO MAUMIVU YA TUMBO KWA MJAMZITO

LEO nitakufahamisha sababu 10 zinazosababisha maumivu ya tumbo wakati wa miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito kwani ni mojawapo ya matatizo yanayolalamikiwa na kinamama wengi wajawazito.

Kuna matatizo mengi ambayo yanasababisha maumivu kwa mtu mwenye ujauzito, hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba hali yoyote ambayo husababisha maumivu kwa mgonjwa asiyekuwa na ujauzito inaweza pia kutokea kwa mjamzito, ingawa historia na uchunguzi vinaweza kuwa tofauti.

Kwa asili kutathmini maumivu ya tumbo kwa mama mjamzito kuna changamoto kwa sababu kichefuchefu, kutapika na maumivu ya tumbo hujitokeza mara nyingi kwa wajawazito wengi.

MIMBA NJE YA MFUKO

Mgonjwa ambaye mimba imetunga nje ya mfuko kipimo cha ultrasound ni lazima kitumike na kitaonyesha mambo mengi na ni pamoja na majimaji na uchafu ndani ya mfuko huo wa uzazi.

Mimba iliyotunga nje ya mfuko ni tatizo linaloongoza kusababisha maumivu kwa kinamama wengi. Tatizo hili linaweza kubainika kwa kutumia kipimo cha Ultrasound na kipimo cha homoni HCG.

Hata hivyo, tatizo hili linatibiwa kama dharura kwa mama kufanyiwa upasuaji.

KIINITETE KUJIPANDIKIZA

Lakini pia kiinitete kinapojipandikiza katika kuta za ndani za mfuko wa uzazi kinaweza kusababisha maumivu makali ya tumbo kwa mjamzito, ambayo huchukua muda wa siku moja hadi mbili na kiasi kidogo cha damu ukeni hutoka.

Mara nyingi kiasi hiki ni kidogo na hutokea kati ya siku sita hadi kumi na mbili baada ya tarehe inayohisiwa mimba kutungwa, mara nyingi kipindi hiki hukaribiana na siku ambayo mwanamke alikuwa anatarajiwa kuingia katika siku zake za hedhi. Hivyo, wagonjwa mara nyingi hufanya makosa kwa kufikiri kuwa wameingia katika siku zao kama kawaida.

MFUKO WA UZAZI KUTANUKA

Mfuko wa uzazi unapotanuka wakati mtoto anakua tumboni unaweza kusukuma viungo vingine kando ndani ya tumbo na kusababisha maumivu, kunaweza kujitokeza upungufu wa damu na kitu kinachoitwa kitaalamu Leukocytosis, mambo ambayo ni kawaida kwa mjamzito na vikawa siyo viashiria vya upungufu wa damu au maradhi.

KINACHOSHIKILIA MFUKO WA UZAZI

Sababu nyingine ya maumivu husababishwa na kitu kinachoitwa kitaalamu ‘round ligament’.

Ligament hii ndio inayoshikilia mfuko wa uzazi. Mfuko wa uzazi unavyozidi kukua, ligament hii huvutika na kusababisha maumivu makali kwa mama mjamzito.

Mara nyingi daktari hutoa dawa za maumivu kwa mama mjamzito na husaidia kwa tatizo hili.

KUTOKA KWA MIMBA

Sababu nyingine ya maumivu ya tumbo kwa mjamzito ni kutoka kwa mimba. Mimba inaweza kutoka yenyewe au kutolewa kwa makusudi. Tatizo hili huambatana na maumivu pamoja na kuvuja damu.

Utoaji wa mimba usiokuwa salama unaongoza kusababisha vifo vya kinamama katika nchi zinazoendelea.

UVIMBE KWENYE MIRIJA MIRIJA YA MAYAI

Wakati mwingine uvimbe huu wa kwenye mirija ya mayai hupasuka au kujizungusha. Hata hivyo, unaweza kupungua na usipopungua unaweza kuondolewa kwa njia ya upasuaji hasa wakati wa muhula wa pili wa ujauzito.

KUJIZUNGUSHA KWA MIRIJA YA MAYAI

Hii hujitokeza mara chache. Uvimbe kwenye mfuko wa uzazi pia husababisha maumivu hasa unapokuwa mkubwa. Tatizo hili linaweza kusababisha ujauzito kutoka hasa katika miezi ya awali.

KIDOLE TUMBO

Kidole tumbo (appendicitis) pia kinaweza kusababisha maumivu ya tumbo kwa mjamzito na hujitokeza kwa uwiano sawa kama wanawake ambao hawana ujauzito. Matibabu ya ugonjwa huu ni upasauji. Mara nyingi wanawake wengi hupata uchungu baada ya upasuaji.

Kutokana na mabadiliko ya homoni wanawake wengi hupata tatizo la mawe kwenye mfuko wa nyongo. Tatizo hii huweza kugunduliwa kwa njia ya kipimo cha Ultrasound. Matibabu hutegemea na dalili na uchunguzi wa daktari.

UVIMBE MFUKO WA NYONGO

Uvimbe unaoitwa kitaalamu inflammation kwenye mfuko wa nyongo ni tatizo la ghafla linalosababisha maumivu makali ambalo pia hujitokeza wakati wa mimba.

Tatizo hili mara nyingi husababishwa na mawe kwenye mfuko wa nyongo. Dawa za kuua bakteria hutumika katika matibabu ya ugonjwa huu.

MAAMBUKIZI NJIA YA MKOJO

Wanawake wengi wakati wa ujauzito hupata maambukizi kwenye njia ya mkonjo mara kwa mara. Hii ni kutokana na mabadiliko yanayojitokeza wakati huu wa ukuaji wa mimba.

UCHUNGUZI

Ultrasound hutumika katika uchunguzi wa maumivu ya tumbo wakati wa ujauzito. Kongosho, mfuko wa nyongo na kidole tumbo vyote huonekana kwa mama mjamzito. Vipimo vinavyotumia mionzi vitumike tu pale inapohitajika kwa mama mjamzito.

Dokta wa Uwazi Simu: 0754 391743 GPL

No comments: